May 06, 2024 10:43 UTC
  • Rais wa Iran: Matukio ya Gaza yamefichua sura halisi ya Magharibi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, matukio ya Gaza yamefichua sura halisi ya Wamagharibi na kuonyesha mgongano uliopo kati ya kambi ya watu sharifu, na tabaka la wanafunzi wenye uelewa wa vyuo vikuu na mrengo wa uovu wa viongozi wakorofi na wanaokanyaga sheria, haki na uhuru wa binadamu wa nchi za Magharibi.

Sayyid Ebrahim Raisi ameyaysema hayo mapema leo katika kikako cha baraza la mawaziri mjini Tehran. Ameeleza masikitiko yake makubwa kwa yanayojiri sasa katika vyuo vikuu vya Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi, na kusema ukiukaji wa hadhi ya wanafunzi, wahadhiri, vyuo vikuu na vituo vya sayansi, utafiti na elimu, sheria, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kalamu na utetezi wa haki za binadamu ni majanga ambayo yamefichua sura halisi ya ustaarabu wa Magharibi mbele ya macho  ya walimwengu na kuthibitisha usahihi wa misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba madai ya Wamagharibi kuhusu kutetea haki za binadamu na uhuru ni ya uongo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema, Wamagharibi wanajinadi kama watetezi wa maadili na haki za binadamu kwa kuficha nyuso zao za kidhalimu na zilizodhidi ya haki za binadamu nyuma ya kaulimbiu za hadaa na udanganyifu. Ameongeza kuwa, matukio ya Gaza yameondoa pazia katika uso huo wa Wamagharibi, na hapana shaka kwamba msimamo imara wa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla, utatoa mwanga na kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo.

Sayyid Ebrahim Raisi pia ameashiria uungaji mkono wa harakati ya wasomi na wanataaluma wa Iran kwa harakati dhidi ya Uzayuni na kusema kuwa, ujumbe wa mshikamano na uungaji mkono wa wanafunzi wa vyuo vikuu na maprofesa wa Iran kwa harakati za hivi sasa za wanafunzi na maprofesa wa Marekani na Magharibi umewaimarisha zaidi katika kutetea haki za taifa la Palestina linalokandamizwa.

Zaidi ya watu 2,000 wametiwa mbaroni hadi sasa tangu yalipoanza maandamano ya kupinga vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza, maandamano ambayo yanafanyika kwa anuani ya "Vuguvugu la Mshikamano na Gaza", yaliyoanzia katika Chuo Kikuu cha Columbia mjini New York na kuenea kwenye vyuo vingine vya Marekani.

Maandamano hayo ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani yameibuka kutokana uungaji mkono wa kila hali wa serikali ya Joe Biden kwa Israel na mauaji ya mtawalia yanayoendelea kufanywa na jeshi la utawala huo dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Tags