Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran aahidi uungaji mkono endelevu kwa Muqawama
Israel imefikia katika hali ya mkwamo, na Jamhuri ya Kiislamu itaendelea daima kuunga mkono mapambano halali na ya haki dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel.
Haya yamesemwa na Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi, Kamanda wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa umepita zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uanzishe vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza. Ameongeza kuwa, viongozi wa utawala wa Israel wamegonga mwamba na wameshindwa kuandaa mkakati wa kina kwa ajili ya Gaza baada ya vita kwa sababu wanakabiliwa na changamoto mpya.
Kamanda wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Muqawama bado uko hai na utaendelea kuwa hai na umetoa vipigo vikali kwa utawala wa Kizayuni miezi kadhaa iliyopita.
Kamanda wa Jeshi la Iran amegusia pia Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya Oktoba 7 mwaka jana iliyotekelezwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) dhidi ya Israel na kusema tukio hilo ni alama muhimu ya mabadiliko.