HRW: Watoto 10 wauawa katika maandamano ya uchaguzi Msumbiji
(last modified Wed, 27 Nov 2024 03:16:28 GMT )
Nov 27, 2024 03:16 UTC
  • HRW: Watoto 10 wauawa katika maandamano ya uchaguzi Msumbiji

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kuwa askari usalama wa Msumbiji vimewauwa watoto wasiopungua 10 na kujeruhi makumi ya wengine wakati wakijaribu kuzima maandamano ya wiki kadhaa kufuatia uchaguzi wa rais uliokumbwa na utata.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema askari usalama wa Msumbiji waliwazuilia mamia ya watoto wengine, baadhi yao kwa siku kadhaa kinyume na sheria za kimataifa, tangu matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa mwezi mmoja uliopita.

Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika imekumbwa na machafuko baada ya mgombea wa chama tawala kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 9 licha ya madai ya upinzani ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi huo uliokosolewa na waangalizi wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na timu kutoka Umoja wa Ulaya.

Mamlaka ya Msumbiji haijatoa maelezo kuhusu ni watu wangapi wameuawa au kuzuiliwa katika maandamano hayo, lakini imesema baadhi ya maandamano hayo yaligeuka na kuwa ya vurugu, na kwamba ilibidi yadhibitiwe na askari usalama.

Daniel Chapo alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa Oktoba 24, akiendeleza utawala wa nusu karne wa chama cha Front for the Liberation of Mozambique, yaani tangu uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa wakoloni wa Kireno mwaka 1975.