May 06, 2024 07:12 UTC
  • Askari 3 wa Israel waangamizwa katika shambulio la HAMAS

Wanajeshi watatu wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameangamizwa katika shambulizi la ulipizaji kisasi lililofanywa na Mujahidina wa Brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS.

Shirika la habari la IRNA limenukuu ripoti ya shirika la SAMA inayosema kuwa, wapiganaji wa Qassam jana Jumapili walishambulia mkusanyiko wa wanajeshi wa Israel katika kivuko cha Kerem Shalom na viunga vyake, kwa kutumia mfumo wa maroketi ya masafa mafupi wa Rajoom. 

Shirika la habari la Palestina SAMA, limemnukuu msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari, akithibitisha habari za kuuawa askari watatu wa Kizayuni na kujeruhiwa wengine zaidi ya 11 katika shambulio hilo.

Izzuddin al-Qassam hapo awali ilikuwa imetangaza habari ya kufanya shambulizi la mlolongo wa maroketi dhidi ya kambi za kijeshi za Israel karibu na vitongoji vya Karam Abu Salem, kusini mwa mpaka wa Ukanda wa Gaza.

Osama Hamdan, mjumbe wa ngazi za juu wa HAMAS na pia msemaji wa harakati hiyo nchini Lebanon amesisitiza kuwa, operesheni ya wanamuqawama wa Palestina katika eneo la Kerem Shalom imetuma ujumbe wa tahadhari kwa Wazayuni kwamba, chokochoko zozote za utawala huo pandikizi zitajibiwa kwa nguvu na matokeo yake yatakuwa mabaya.

Wanajihadi wa Qassam katika operesheni ya kijeshi

Takriban watu elfu 34,654 wameuawa shahidi huko Gaza tangu tarehe 7 Oktoba mwaka jana, wakati utawala haramu wa Israel ulipoanzisha vita dhidi ya Wapalestina wa ukanda huo.

Haya yanajiri siku chache baada ya wanamapambano wa Brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la HAMAS kufanya shambulizi jingine la kuvizia na kuangamiza wanajeshi zaidi ya 10 wa Kizayuni mashariki mwa Khan Yunis, Gaza.

Tags