May 06, 2024 07:28 UTC
  • Kambi ya Muqawama, ngao kuu ya kuzuia hujuma za utawala wa Kizayuni katika eneo

Vikosi vya mapambano na Muqawama vya Bahrain vimefanikiwa kuvilenga vituo muhimu sana vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel; na kwa kuungana na makundi mengine ya kambi ya Muqawama, kuwa sehemu ya ngao kuu ya kuzuia hujuma na uchokozi wa utawala huo ghasibu katika eneo.

Saraya Al-Ashtar, tawi la kijeshi la Muqawama wa Kiislamu wa Bahrain limetangaza kuwa limeshambulia kwa kutumia ndege isiyo na rubani kituo muhimu cha utawala wa Kizayuni katika mji wa Umm al-Rashrash (Bandari ya Eilat) kusini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Muqawama wa Kiislamu la Bahrain ulitoa taarifa siku ya Jumamosi, tarehe 4 Mei na kutangaza kuwa: shambulio hilo la ndege isiyo na rubani lilitekelezwa kwa madhumuni ya kuonyesha mshikamano na uungaji mkono kwa wananchi wanamuqawama wa Ukanda wa Gaza, na kwamba operesheni hizo za mashambulio dhidi ya utawala haramu wa Israel hazitasitishwa hadi utakapoondolewa mzingiro na kukomeshwa mashambulizi ya utawala huo dhidi ya wananchi wanamuqawama wa Palestina katika ukanda wa Ghaza.

Wiki iliyopita pia Saraya Al-Ashtar, tawi la kijeshi la Muqawama wa Kiislamu wa Bahrain lilitoa taarifa na kutangaza kuwa limefanya shambulio la ndege zisizo na rubani lililolenga bandari ya utawala wa Kizayuni ya Eilat.
 
Tangu ilipoanza operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa makundi mbalimbali ya Muqawama katika eneo hili yamekuwa bega kwa bega na makundi ya Palestina na kuyaunga mkono katika mapambano yao dhidi ya utawala wa Kizayuni. Makundi ya Muqawama katika nchi za Iraq, Lebanon, Yemen na hivi sasa Bahrain yamekuwa yakivishambulia vituo hasasi na muhimu sana vya kijeshi na kijasusi vya utawala wa Kizayuni na hivyo kudhihirisha uadhaifu wa Wazayuni.
Muqawama wa Kiislamu wa Bahrain

Sifa maalumu ya operesheni za makundi ya Muqawama dhidi ya Wazayuni, -mbali na kuwa na wigo mpana-, ni kutumia mbinu mbalimbali za kijeshi na silaha mpya, huku Jeshi la Kizayuni likionyesha kuwa ni dhaifu na lisilo na uwezo wa kujibu mashambulizi hayo, kiasi kwamba makundi ya Muqawama yameweza kutoa vipigo visivyoweza kufidika kwa utawala huo.

Katika siku za karibuni, makundi ya Muqawama nchini Bahrain yamefungua kambi mpya dhidi ya utawala wa Kizayuni; na hilo litakuwa onyo kwa viongozi watenda jinai wa utawala huo. Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ilidhihirisha udhaifu unaozidi kuongezeka kila uchao katika uwezo wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni; na makundi ya Muqawama yamethibitisha kuwa licha ya uungaji mkono wa pande zote wa Ikulu ya Marekani White House kwa Tel Aviv, Wazayuni wamelazimika kukubali kuwa wameshindwa kukabiliana na operesheni zenye wigo mpana za makundi hayo ya Muqawama.

Hata wataalamu wa Kizayuni pia wametoa indhari kuhusu uwezo duni wa kijeshi na kijasusi wa jeshi la Kizayuni katika kukabiliana na Muqawama wa Palestina na makundi mengine ya Muqawama katika eneo. Liraz Margalit, mtafiti katika Taasisi ya Kistratejia ya Kituo cha Herzliya, ameandika makala katika gazeti la Kizayuni la Ma'ariv akisema, 'tumeshtukizwa kwa vita ambavyo hatukuwa tumejiandaa navyo hata kidogo'.

Kutokana na kuendelea vita huko Ghaza na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Palestina, umoja na mshikamano wa makundi ya Muqawama katika eneo umeongezeka; na makundi hayo yanaendelea na operesheni zao katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu licha ya vitisho na propaganda zinazofanywa na vyombo vya habari vya Magharibi. Mashambulizi hayo yameufanya utawala wa Kizayuni upoteze sehemu kubwa ya vituo vyake vya kijeshi na kiuchumi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuwafanya Wazayuni wakabiliwe na hali mbaya.

Kuanza operesheni za makundi ya Muqawama nchini Bahrain kumedhihirisha ukweli kwamba, njia athirifu zaidi ya kukabiliana na uzushaji mvutano ulioanzishwa na utawala wa Kizayuni ni kusimama imara na kuendeleza operesheni za kuwahami wananchi wa Palestina. Kwa kuielewa hali halisi ya eneo na kutumia fursa na uwezo yalionao, makundi ya Muqawama yamewafanya Wazayuni walazimike kurudi nyuma. Matukio ya leo katika eneo hili yameathiriwa na hatua na operesheni za makundi ya Muqawama ambayo hayaitakidi kama utawala bandia wa Kizayuni una uhalali wowote wa kisheria.../