May 06, 2024 02:34 UTC
  • Kuanza awamu ya nne ya operesheni ya jeshi la Yemen dhidi ya meli zinazokwenda Israel

Sambamba na maandamano ya wananchi wa Yemen katika miji tofauti ya nchi hiyo ya kuwaunga mkono watu wa Gaza, msemaji wa jeshi la Yemen ametangaza habari ya kuanza awamu ya nne ya operesheni za nchi hiyo kwa ajili ya kuwatetea wananchi wa Palestina na kusisitiza kuwa: Wigo wa mashambulizi ya Yemen yutapanuka kuanzia Bahari ya Mediterania hadi sehemu yoyote ambayo nchi hii inaweza kuzifikia meli zinazoelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).

Jeshi la Yemen limetangaza kuwa, katika awamu hii ya oparesheni zake, itazishambulia meli ambazo zitakuwa zikifanya safari kutokea Bahari Nyekundu zikielekea katika bandari ya utawala wa Israel, katika maeneo yote ambayo jeshi la Yemen litayafikia. Kufuatia operesheni za jeshi la Yemen, safari za meli za Marekani kupitia Bahari Nyekundu zimepungua kwa asilimia 80, na wakati huo huo, gharama ya bima kwa meli za Marekani zinazotaka kupita katika Bahari Nyekundu zimeongezeka hadi dola milioni 50. 

Katika miezi liyopita, jeshi la Yemen limezishambulia meli za Marekani, Uingereza na za utawala wa Kizayuni wa Israel, au zile zilizokuwa zikielekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yaani Israel zilizokuwa zikivuka Bahari Nyekundu na katika Mlango Bahari wa Babul -Mandab. 

Mashambulizi ya jeshi la Yemen dhidi ya meli zinazoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu

Vikosi vya jeshi la Yemen vimeahidi kuendelea kuzishambulia meli za utawala huo ghasibu au meli zinazoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina zinapitia Bahari Nyekundu hadi pale utawala huo utakapokomesha mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza. Yemen, ambayo ni moja ya mihimili na harakati muhimu zinazoiunga mkono na kuihami Gaza, imeendelea kuwatetea wananchi wa Palestina katika ngazi zote tangu baada ya oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa na imetekeleza operesheni za kijeshi zisizo na kifani dhidi ya adui Mzayuni na waungaji mkono wake.  

Baada ya harakati ya Hizbullah huko kusini mwa Lebanon, Yemen ilikuwa ya pili iliyoingia uwanjani kuwaunga mkono watu wa Gaza na kwa shabaha ya kuwashinikiza Wazayuni maghasibu wasitishe mashambulizi na mzingiro dhidi ya watuu wa Gaza. Yemen pia ilianzisha mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya maslahi ya Wazayuni. Hatua ya jeshi la Yemen ya kuzishambulia meli za Wazayuni na zile zinazoelekea katika bandari za Israel, wakati huu ambapo mzingiro na mashambulizi dhidi ya Gaza yanaendelea, ni mlingano ambao ulibuniwa na Wayemeni siku kadhaa baada ya kuanza vita dhidi ya Gaza. Mlingano huu umeutia kiwewe utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake na kuzifanya Marekani na Uingereza kuanzisha mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya Yemen ili kuihami Israel.   

Kuingia Yemen vitani kwa maslahi ya watu wanaouawa kinyama wa Gaza ni kielelezo halisi cha dhana ya umoja katika medani ya mapambano yaani katika kupambana na adui. Jeshi la Yemen lilitangaza kuwaunga mkono kikamilifu wananchi wa Palestina tangu ambapo liliioshambulia bandari ya Eilat huko kusini mwa Israel katika oparesheni zake za ndege zisizo na rubani na makombora. Yemen pia imezizuia meli za Israel na zile zinazotaka kuelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina kuvuka mlango Bahari wa Babul- Mandab. 

Mlango Bahari wa Babul -Mandab 

Makombora ya Ansarullah yanapaswa kukata masafa ya zaidi ya kilomita 1600 ili kufika katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yaani Israel. Ikiwa upo uwezekano wa kuitwanga bandari ya Eilat kusini mwa Israel ambayo inactambuliwa kuwa bandari muhimu zaidi ya Israel, basi kuiparaganisha bandari ya Haifa kunaweza kuzingatiwa kama chaguo linalofuata la harakati ya Ansarullah. 

Dunia nzima, hasa Marekani, inajua umuhimu wa Mlango Bahari wa Babul - Mandab na maji ya Bahari Nyekundu kwa biashara ya kimataifa, kwa sababu karibu mapipa milioni 6.2 ya mafuta yasiyosafishwa hupita katika njia hiyo ya maji kila siku. 

Katika hali ambayo Marekani imetangaza kuwa imeanzisha muungano wa baharini kwa kuzishirikisha nchi 10 ili kukabiliana na vitisho vya jeshi la Yemen katika Bahari Nyekundu, lakini muungano huo sasa unakaribia kusambaratika kikamilifu na hakuna mtu aliye tayari kugharamika kwa ajili ya serikali ya mrengo wa kulia ya kibeberu ya Netanyahu isipokuwa Marekani na Uingereza. Hasa ikizingatiwa ukweli kwamba, harakati wanafunzi wa vyui vikuu zinaendelea kushika kasi zikidhihirisha upinzani wao kwa nchi zinazouhami utawala wa Kizayuni.