Russia yatangaza, imeharibu kambi 2 za magaidi nchini Syria
Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa imeharibu kambi mbili za magaidi wanaosaidiwa na Marekani huko magharibi mwa Syria.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kwamba, jeshi la anga la nchi hiyo limeangamiza kambi mbili za magaidi walioondoka eneo la Al-Tanf kwenye mpaka wa Syria, Iraq na Jordan na kujificha katika eneo la milimani, mashariki mwa mkoa wa Homs magharibi mwa Syria, na katika eneo la Al-Amur katika mkoa huo.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Russia imeongeza kuwa, katika eneo la al-Tanf, kunarikodiwa kesi 9 za ukiukaji wa anga unaofanywa kila siku na ndege za kijasusi za F-15, Typhoon, Thunderbolt na MC-12W, ambazo zote ni za muungano wa Marekani eti dhidi ya ISIS.
Jeshi la kigaidi la Marekani liliteka baadhi ya maeneo ya Jazeera na al-Tanf nchini Syria na kuanzisha vituo vya kijeshi huko kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la ISIS, lakini ukweli wa mambo na taarifa za kijasusi zimethibitisha baadaye kuwa kambi hizo zilitumika kama vituo vya kuyasaidia makundi ya kigaidi katika eneo hilo.