Medvedev: Yumkini mataifa mengi zaidi yakaunda silaha za nyuklia
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Russia, Dmitry Medvedev amesema kuna uwezekano mataifa zaidi kuzalisha silaha za nyuklia kutokana na kuongezeka ukosefu wa utulivu duniani.
Katika mahojiano na Kommersant yaliyorushwa leo Jumatatu, Rais huyo wa zamani wa Russia ameonyesha kukata tamaa kuhusu kutoenea kwa silaha za nyuklia, akisema, "Mpasuko uliojitokeza katika nidhamu ya dunia unayasukuma mataifa kadhaa kutafuta njia bora zaidi za kujilinda."
Medvedev ameeleza bayana kuwa, "Baadhi (ya mataifa) yataamua kwamba chaguo bora zaidi ni kupata silaha za nyuklia."
Afisa huyo wa Russia amesema, "Mataifa mbalimbali yana uwezo wa kiufundi wa kuendesha mradi wa nyuklia wa kijeshi, na baadhi yanaendelea na utafiti katika eneo hili. Hilo linaweza kuwa kinyume na maslahi ya ubinadamu, lakini tuwe waaminifu, ubinadamu haujabuni njia nyingine ya kuhakikisha kujilinda na uhuru kwa uhakika."
Mara kadhaa, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Russia amenukuliwa akisema kuwa, Marekani inafanya makosa ikiwa inaamini kwamba Moscow haitatumia silaha za nyuklia iwapo uwepo wake utatishiwa.
Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia wa 1968 (NPT) unatambua wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama mataifa pekee yenye silaha za nyuklia. Tangu utiaji saini mkataba huo, India, Pakistan na Korea Kaskazini zimeunda silaha za nyuklia.
Kadhalika, utawala wa Kizayuni wa Israel unaaminika kumiliki kiwango kikubwa cha vichwa vya nyuklia. Afrika Kusini ya enzi ya ubaguzi wa rangi 'apartheid' ndiyo nchi pekee iliyosambaratisha kwa mafanikio mpango wake wa nyuklia wa kijeshi.