May 05, 2024 12:08 UTC
  • Rais wa DRC: Russia, china zina muamala bora na Afrika kuliko Magharibi

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema Russia na China zina muamala bora katika uhusiano na nchi yake na hazina kiburi wala hamu ya "kutoa somo kwa nchi za Afrika." Ameongeza kuwa Russia na China zina muamala mzuri  kwa nchi yake kuliko Magharibi.

Tshisekedi amenukuliwa na Shirika la Habari la Sputnik akisema: "Nchini Ufaransa, Israel ililaaniwa kwa baadhi ya vitendo huko Gaza. Je, hii inazuia Ufaransa kudumisha uhusiano wake na Israel? Kwa nini wanataka kutushinikiza linapokuja suala la Waafrika? Mtu asituhukumu. Tuna haki ya kuchagua marafiki. Tunataka kuwa marafiki kwa wale wote wanaotaka kuwa marafiki zetu... Warussia wanataka urafiki na Afrika na DR Congo, kwa nini tukatae? Hakuna sababu ya kukataa.

Rais wa DRC ameongeza kuwa China na Russia ni "washirika wanaokuja kupitia mlango wa mbele."

Tshisekedi, ambaye nchi yake ina utajiri mkubwa wa madini, anatazamiwa kushiriki kongamano la Russia na nchi za Afrika litakalofanyika mwezi Juni.

Hayo yanaripotiwa siku chache baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kusema itachukua hatua ya kisheria dhidi ya kampuni ya Apple Inc ya Marekani kwa kushirikiana na waporaji wa madini ya nchi hiyo.