May 05, 2024 07:35 UTC
  • Hamas: Hakuna mapatano bila kukomesha mauaji na jinai za vita za Israeli huko Gaza

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Wapalestina, Hamas, imesema kwamba, haitakubali mapatano ambayo hayatakomesha kabisa vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel vilivyoendelea kwa takriban miezi saba sasa dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

.Maoni hayo yalitolewa jana Jumamosi na afisa wa Hamas ambaye hakutaka jina lake litajwe

Takriban watu elfu 34,654 wameuawa shahidi huko Gaza tangu tarehe 7 Oktoba mwaka jana, wakati utawala haramu wa Israel ulipoanzisha vita dhidi ya watu wa Gaza.

Afisa huyo ameongeza kusema kuwa harakati hiyo haitakubaliana na mapatano ambayo hayatajumuisha usitishaji vita wa kudumu na kuondoka wanajeshi wa Israel huko Gaza.

Aliongeza kwa kusema utawala huo haramu wa Israel unajaribu kufikia makubaliano ambayo yatawezesha kuachiliwa huru mateka waliokamatwa wakati wa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa huko Palestina bila kuhusisha kukomesha uchokozi unaofanywa Ukanda wa Gaza.

Afisa huyo wa Hamas vilevile aliongeza kwa kusema kuwa, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anazuia kufukiwa makubaliano ya kusitishwa vita kutokana na maslahi yake binafsi

Maoni hayo yanafanana na yale yaliyotolewa na Hossam Badran, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Hamas huko Palestina siku moja kabla.

Afisa wa ngazi ya juu wa harakati ya Hamas, Bardan

Bardan alikuwa amemlaumuu Netanyahu kwa kukwamisha makubaliano na kusisitiza kuwa uamuzi wa waziri mkuu huyo wa Israel wa kufanya mashambulizi ya nchi kavu dhidi ya mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah ni kikwazo kikubwa katika mazungumzo yanayolenga kufikia makubaliano ya kusitisha vita.

Takriban Wapalestina milioni 1.5 wamekimbilia hifadhi katika mji huo kutokana na uharibifu uliofanyika katika maeneo yaliyoharibiwa na vita vya utawala haramu wa Israel.