Tahadhari ya WHO kuhusu Zika kwa waendao Olympiki Brazil
(last modified Wed, 22 Jun 2016 07:05:04 GMT )
Jun 22, 2016 07:05 UTC
  • Tahadhari ya WHO kuhusu Zika kwa waendao Olympiki Brazil

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa tahadhari ya afya kwa wote wanaokwenda kwenye mashindano ya Olimpiki nchini Brazili kufuatia mlipuko wa homa ya Zika.

WHO imesema wasafiri wote pamoja na wachezaji wa mashindano ya Olimpiki na Olimpiki ya walemavu lazima wafahamishwe kuhusu hatari za kiafya kwenye maeneo watakayozuru nchini Brazil na pia njia za kujikinga ili kupunguza hatari ya kupata virusi hivyo.

WHO imebaini kuwa, kila nchi sasa ina ushauri wa kitaifa kuhusu mlipuko wa Zika na wasafiri ni muhimu kupata ushauri kutoka kwa mamlaka za afya katika nchi zao. Aidha WHO imesema miongoni mwa mambo ya kuzingatia ni watu kujizuia kushika ujauzito kwa kipindi chote watakachokuwa Brazil.

Na kwa upande wa mwenyeji wa mashindano Brazil, wizara yake ya afya imejiandaa na inatoa ushauri kwa wageni wote wanaowasili nchini humo ikiwa ni pamoja na kuanzisha tovuti maalumu inayoelezea athari za Zika na jinsi ya kujikinga. Michuano ya Olimpiki inaanza Agosti 5 hadi 21 mwaka huu.

Kirusi cha Zika kuligunduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika mwaka 1947 na hakikuhesabiwa kuwa hatari hadi kilipoibuka upya mwaka jana Brazil na kusababisha wanawake walioambukizwa kuzaa watoto wenye ubongo mdogo. Kwa msingi huo wataalamu wanasema kirusi cha Zika kilichoibuka Brazil ni hatari zaidi ya kirusi cha zika kilichogunduliwa Afrika miaka iliyopita.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan amesema tafiti zinazoendelea zimebaini kuwa kirusi hicho sasa sio tu kinasambazwa kupitia mbu bali pia kwa njia ya ngono.