Jun 04, 2023 11:25 UTC
  • Mexico yaupandishia hadhi ubalozi wa Palestina nchini humo

Mexico imechukua hatua ya kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Palestina, na sasa ofisi ya mahusiano ya Palestina katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini imepandishwa ngazi na kuwa ubalozi kamili.

Ujumbe wa ukurasa wa Palestina katika mtandao wa kijamii wa Twitter ulioandikwa kwa lugha ya Kihispania unasema: Ofisi ya Palestina jijini Mexico City sasa imepandishwa hadhi na kuwa ubalozi kamili, baada ya Mexico kulitambua kikamilifu dola la Palestina. 

Ujumbe huo unasema, hatua hiyo imechukuliwa katika moyo wa ushirikiano na urafiki baina ya mataifa mawili, hiyo ikiwa ni ithibati tosha kuwa uhusiano wa nchi mbili hizo unazidi kuimarika tangu kuasisiwa kwake mwaka 1975.

Ikumbukwe kuwa, Novemba mwaka uliopita, Seneti ya Mexico ilipasiaha azimio la kuitambua kikamilifu Palestina kama taifa huru, wakati Palestina ilipokuwa ikiadhimisha kumbukumbu ya siku ilipojitangazia uhuru wake mnamo Novemba 15, 1985. 

Kwa muda mrefu sasa, aghalabu ya nchi za Amerikali ya Latini zimekuwa zikitangaza wazi wazi uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina, sambamba na kupinga sera kandamizi na jinai za Israel mkabala wa Wapalestina. 

Rais Andrés Manuel López Obrador wa Mexico amekuwa akiwatetea wazi Wapalestina

Februari mwaka huu, kundi la nchi za Amerika ya Latini ikiwemo Mexico ililaani na kukosoa vikali uamuzi wa serikali yenye misimamo ya kufurutu ada ya Benjamin Netanyahu wa kuidhinisha ujenzi wa vitongoji vipya tisa katika ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Aidha mwaka 2020, Wabunge wa baadhi ya nchi za Amerika ya Latini walitaka kutungwe sheria za kuususia na kuuwekea vikwazo utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kupora ardhi za Wapalestina.

Tags