Jun 16, 2023 02:28 UTC
  • Kupanuka zaidi mpasuko wa kidini nchini India

Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni wa Kituo cha Utafiti wa Jamii Zinazoendelea (CSDS) huko New Delhi unaonyesha kuwa, sera za Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, zimezidisha mgawanyiko wa kidini nchini humo.

Mgawanyiko huu wa kidini unaonekana zaidi kati ya Wahindu na Waislamu nchini India.

Ukweli ni kwamba Chama cha Bharatiya Janata kilichukua mamlaka kwa kaulimbiu za Uhindu na kupanda juu zaidi nara za utaifa za Chama cha Congress. Chama hicho kimefanya jitihada za kunyakua kura za wananachi kupitia njia ya kuchochea vikundi vya Wahindu wenye misimamo mikali kama RSS (shirika la kijeshi la kujitolea la Wahindu la mrengo wa kulia la India) na Shiv Sena, ambavyo vina ushawishi mkubwa sana katika maeneo ya vijijini na mijini midogo.

Kutokana na kushindwa kwa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, katika kuboresha hali ya kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo, chama cha BJP kinaendelea kusisitiza kaulimbiu zake za Uhindu, ambazo zimekuwa na taathira hasi kwa hali ya kidini ya India katika miaka ya hivi karibuni. Ali Alaei, mtaalamu nguli wa masuala ya India, anasema: "India ni nchi yenye dini, mbari na makabila mengi, na kaulimbiu pekee inayoweza kusaidia kuimarisha umoja wa kitaifa katika nchi hiyo ni ile inayohamasisha utaifa, ambayo imekuwa ikifuatwa na vyama vingine, haswa chama cha Congress. Tafauti na vyama hivi, chama cha Bharatiya Janata kiliingiza kaulimbiu ya Uhindu katika uwanja wa siasa za India katika kipindi cha uongozi wa Atal Bihari Vajpayee."

Msisitizo wa kaulimbiu kama hiyo hata wakati wa utawala wa Narendra Modi katika jimbo la Gujarat, ulisababisha uharibifu mkubwa wa kijamii na kidini katika jamii ya India, kwa kadiri kwamba Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mipaka wamekuwa wakiwashambulia Waislamu waziwazi katika sehemu tofauti za India, ambapo mamia miongoni mwao wameuawa na nyumba zao zimeteketezwa kwa moto. Maafa ya Msikiti wa Babri katika jimbo la Uttar Pradesh pia yalitokea kwenye muongo wa 80 wakati serikali ya eneo hilo ilipokuwa kwenye mikono ya chama BJP. Kumar Singh Yadav, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema: "Ingawa chama cha BJP kimeparamia mawimbi ya fikra za Uhindu na bado kinashikilia madakaka kimabavu nchini India, lakini kushindwa kwake kutatua matatizo ya kiuchumi na kijamii kunazidisha uwezekano kwamba tarehe na muda wa matumizi ya itikadi kali kama hizo unakaribia mwisho, na jambo hili linazidisha nguvu fikra kwamba watu wa India watarejea tena kwenye kaulimbiu za utaifa katika siku zijazo."

Kushindwa kwa chama cha BJP katika chaguzi za hivi karibuni za mitaa na majimbo kunaonyesha hofu inayoongezeka ya watu wa India kuhusu matokeo mabaya ya kaulimbiu za itikadi kali za Uhindu. Hasa ikitiliwa maanani kwamba, chama hicho kimeshindwa kutatua matatizo ya wananchi, hasa katika majimbo yenye hali duni, na mapengo ya kiuchumi pia yanaongezeka siku baada ya nyingine.

Uchunguzi wa maoni wa taasisi ya utafiti unaonyesha kuwa kiwango cha kuridhika Wahindu na utendaji wa chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP) kimefikia chini ya 60%; wakati huo huo, kiwango cha kutoridhika kwa Waislamu kimefikia karibu 60%, hii ni licha ya kwamba, jamii ya Waislamu wa India ina uzito mkubwa katika chaguzi za nchi hiyo.

Waislamu wa India

Pamoja na hayo, Waislamu wa India, ambao wana nafasi isiyopingika katika ustawi na maendeleo ya nchi hiyo, kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa, hawajawahi kamwe kuanzisha chama. Kwa hiyo, wanatarajia kuona vyama tawala nchini India vikitunga sera kwa maslahi ya umma kwa lengo la kuimarisha misingi ya usalama wa jamii, na sio kuwakumbuka Waislamu wakati wa uchaguzi tu.

Tags