Ijumaa, tarehe 09 Mei, 2025
(last modified Sat, 10 May 2025 06:41:18 GMT )
May 10, 2025 06:41 UTC
  • Ijumaa, tarehe 09 Mei, 2025

Leo ni Ijumaa tarehe 11 Dhulqaada 1446 Hijria sawa na Mei 09 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 1298 iliyopita, yaani tarehe 11 Dhilqaada mwaka 148 Hijiria, alizaliwa Imam Ali bin Musa al-Ridha (as), mmoja wa Ahlul Bait watukufu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Madina.

Imam Ridha (as) alianza kuongoza Umma wa Kiislamu mwaka 183 Hijria baada ya kuuawa shahidi baba yake mtukufu, yaani Imam Musa al-Kaadhim (as). Katika uhai wake alifahamika kama shakhsia wa pekee katika Ulimwengu wa Kiislamu kutokana na elimu yake kubwa na uchaji-Mungu. Ni kutokana na hali hiyo na katika kujaribu kudhibiti hali ya mambo na kuzuia taathira chanya za mtukufu huyo katika ulimwengu wa Kiislamu, ndipo khalifa wa utawala wa Bani Abbasi yaani Ma'amun, akamlazimisha kuwa mrithi wake wa kiti cha ufalme lengo kuu likiwa ni kumdhibiti Imam Ridha (as).

Hatua hiyo ililazimu mtukufu huyo kupelekwa mjini Mar'wu, kaskazini mashariki mwa Iran ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Bani Abbasi enzi hizo. Hata hivyo njama chafu hizo za mtawala Ma'amun ziligonga mwamba baada ya watu wengi kuvutiwa sana na Imam Ridha kutokana na elimu ya hali ya juu na mawaidha yake aliyokuwa akiyatoa kwa Waislamu suala ambalo lilipelekea mtawala huyo kupanga njama za kumuua. Hatimaye mwaka 203 Hijiria, Imam Ridha aliuawa shahidi baada ya kulishwa sumu ndani ya chakula. 

Siku kama ya leo miaka 1109 iliyopita, alizaliwa mjini Baghdad, Iraq, Muhammad Bin Muhammad, maarufu kwa lakabu ya 'Sheikh Mufid', msomi na faqihi mkubwa wa Kiislamu.

Sheikh Mufid alikulia katika familia ya watu wenye elimu na imani, na lipata elimu ya msingi katika familia yake na kisha kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Baada ya hapo Muhammad, alitokea kuwa alimu mkubwa katika uga wa teolojia na sheria za Kiislamu wa zama hizo.

Miongoni mwa harakati za kifikra na kitamaduni za Sheikh Mufid ni pamoja na midahalo yake ya kielimu na wasomi wa sheria za Kiislamu na maulama wa madhehebu tofauti za Kiislamu, suala ambalo lilimfanya kuwa mwanazuoni hodari katika uga wa teolojia na fiqhi.

Sheikh Mufid ameacha athari nyingi za vitabu ambavyo vinafikia juzuu 200 baadhi yavyo ikiwa ni vitabu vya 'Al-Irshaad' 'Al-Arkaan' na 'Usulul-Fiqhi.' 

Siku kama ya leo miaka 371 iliyopita, kazi ya ujenzi wa jengo la Taj Mahal linalohesabiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kuvutia zaidi duniani na moja kati ya mifano bora zaidi ya usanifu majengo wa Kiislamu huko India ilimalizika baada ya miaka 22.

Ujenzi wa jengo la Taj Mahal ulianza baada ya kufariki dunia mke wa Shah Jahan, mfalme wa India huko katika jimbo la Agra. Jengo hilo lilijengwa kwa kutegemea ramani iliyochorwa na msanifu majengo mashuhuri wa Iran, Isa Isfahani.

Kwa upande wa nje, jengo la Taj Mahal limenakshiwa kwa ustadi kwa rangi mbalimbali huku kuta zake zikiwa zimeandikwa maandishi ya Kiarabu yenye aya za Qur'ani Tukufu.

Ndani ya jengo hilo kuna makaburi mawili ya mfalme Shah Jahan na mkewe, Nur Jahan. 

Tarehe 9 Mei miaka 220 iliyopita aliaga dunia mwandishi, malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kijerumani kwa jina la Johann Christoph Friedrich von Schiller akiwa na umri wa miaka 46.

Von Schiller alipenda sana masuala ya uandishi tangu utotoni mwake. Friedrich Von Schiller alikuwa hodari katika fasihi ya Kijerumani na anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waandishi mahiri wa Kijerumani katika uga wa fasihi.     

Miaka 109 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Mei, mkataba wa kihistoria wa Sykes-Picot ulitiwa saini na wawakilishi wa Uingereza, Ufaransa na Urusi ya zamani. Hata hivyo Umoja wa Kisovieti baadaye ulijitoa kwenye makubaliano hayo baada ya mapinduzi ya Bolshevik.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, tawala za Uingereza na Ufaransa ziligawana nchi za Kiarabu zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Kiothmania. Kwa msingi huo Iraq na Jordan zikawa chini ya udhibiti wa Uingereza huku Syria na Lebanon zikitawaliwa na Ufaransa. ****

Miaka 98 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 19 Ordibehesht mwaka 1306 Hijria Shamsia, sheria ya "Capitulation' ilifutwa na Bunge la Kitaifa la Iran.

Kimsingi sheria hii ilikuwa na lengo la kuwapa kinga ya kutoshtakiwa raia wa kigeni waliopatikana na hatia ya kufanya uhalifu nchini Iran. Haki ya  'Capitulation' ilitumika mara ya kwanza nchini Iran baada ya mapatano ya Torkmanche ya mwaka 1206 wakati wa utawala wa Fath-Ali Shah ambapo Warusi walipata kinga hiyo na baada ya hapo serikali zingine za kigeni nazo ziliweza kupata haki hiyo ya raia wao kutoshtakiwa nchini Iran.

Hata hivyo sheria hiyo ilipitishwa tena na bunge la kitaifa la Iran mwaka 1343 kwa lengo la kuwapa kinga Wamarekani. Imam Khomeini MA alipinga vikali sheria hiyo na utawala wa Shah ulikasirishwa sana na malalamiko hayo na ukachukua uamuzi wa kumbaidisha Imam nchini Uturuki.

Hatimaye, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, sheria ya 'Capitulation' ilifutwa daima nchini Iran.