Rafsanjani, Mwanasiasa wa Aina Yake-2
https://parstoday.ir/sw/radio/iran-i23812-rafsanjani_mwanasiasa_wa_aina_yake_2
Makala yetu leo itazungumzia mchango wa Rafsanjani katika kutatua migogoro ya muongo wa kwanza baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 18, 2017 04:53 UTC
  • Rafsanjani, Mwanasiasa wa Aina Yake-2

Makala yetu leo itazungumzia mchango wa Rafsanjani katika kutatua migogoro ya muongo wa kwanza baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Hashemi Rafsanjani

Jumapili iliyopita wananchi wa Iran na wapenzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ujumla walimpoteza mmoja kati ya shakhsia waliokuwa na taathira kubwa katika harakati za Mapinduzi na katika kuimarisha misingi ya Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Kifo cha ghafla cha Ayatullah Rafsanjani kimeleta huzuni na simanzi kubwa. Rafsanjani ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa karibu sana kwa mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu katika harakati za kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliendelea kuwa mwaminifu na msaidizi wa karibu wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi dakika za mwisho za uhai wa Imam Ruhullah Khomeini. Tangu kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini, Ali Akbar Hashemi Rafsanjani alijulikana kwa kuwa mwanamapambano shupavu, mtu mwenye tadbiri, mwenye uoni wa mbali, hodari na mchapakazi. Sifa hizi zilimfanya Rafsanjani kuwa shakhsia makhsusi na ya aina yake.

Katika ujumbe wake uliotolewa kwa mnasaba wa tukio la kufariki dunia Ayatullah Hashemi Rafsanjani, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema: "Uhodari wake mkubwa na upendo nadra kuonekana katika miaka hiyo ulikuwa egemeo la kutegemewa kwa wale wote walioshirikiana naye hususan mimi mwenyewe..". Rafsanjani alianza kuunda jumuiya na taasisi mbalimbali za baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kipindi cha kilele cha harakati za mapambano dhidi ya utawala wa Shah hadi utawala huo ulipoondolewa madarakani. Miongoni mwa taasisi zilizoanzishwa na Rafsanjani akishirikiana na wanafunzi na wasaidizi wengine wa Imam Ruhullah Khomeini ni pamoja na kuunda Jumuiya ya Wanazuoni Wanamapambano, kuasisi Baraza la Mapinduzi, Idara ya Kusimamia Migomo na Maandamano, kamati ya kushughulikia tatizo la nishati na kuunda tume ya mapokezi na kulinda usalama wa Imam Khomeini wakati wa kurejea kwake nchini akitokea uhamishoni nje ya nchi. Miongoni mwa kazi nyingine kubwa za Hashemi Rafsanjani kwa ajili ya kuimarisha misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu baada ya ushindi wa Mapinduzi ni kuanzisha Chama cha Jamhuri ya Kiislamu kwa idhini ya hayati Imam Ruhullah Khomeini akiwa pamoja na watu wengine mashuhuri kama Ayatullah Muhammad Beheshti na Ayatullah Ali Khamenei.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni mapinduzi yaliyofanyika kwa msingi wa kuhuisha thamani na maadili ya kibinadamu na kidini chini ya uongozi wa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu. Kwa sababu hiyo mapinduzi hayo yalipigwa vita na kukabiliwa na uhasama mkubwa wa madola makubwa mawili ya Mashariki na Magharibi na vibaraka wao wa ndani tangu siku za mwanzoni mwa ushindi wake. Ili kuyavunja na kuyaua Mapinduzi ya Kiislamu yakiwa bado machanga, mabeberu hao na vibaraka wao walianza kufanya mauaji ya kigaidi dhidi ya viongozi wake. Mhanga kwanza wa njama hiyo chafu alikuwa Ayatullah Murtadha Mutahhari ambaye alikuwa mnadharia mkubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu na mwanafunzi hodari sana wa Imam Ruhullah Khomeini. Ayatullah Mutahhari aliuua shahidi kwa kupigwa risasi na wanachama wa kundi moja lililokuwa likipinga Mapinduzi ya Kiislamu miezi miwili na nusu tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Mlengwa wa pili wa njama hiyo alikuwa Ayatullah Rafsanjani.   

Ayatullah Rafsanjani akiwa pamoja na Ayatullah Khamenei na marehemu Ahmad Khomeini

Ilikuwa haijapita miezi minne kamili wakati Ayatullah Rafsanjani aliposhambuliwa na kunusurika kifo. Rafsanjani alijeruhiwa katika shambulizi hilo. Miongoni mwa sababu zilizopelekea kufeli jaribio hilo la mauaji ya kigaidi lililokuwa limepangwa kwa uhodari mkubwa, ni hatua iliyochukuliwa wakati mwafaka na mke wa Ayatullah Rafsanjani, Bibi Iffat Mar'ashi. Wakati huo Imam Khomeini alitoa ujumbe wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na kuokoka kifo Hashemi Rafsanjani, suala ambalo lilionesha mapenzi makubwa ya Imam kwa mwanamapinduzi huyo shupavu. Katika ujumbe huo, Imam Ruhullah Khomeini alisema: Janabi Hujjatul Islam, mwana jihadi, mwenye kushikamana na dini, Hashemi mpenzi! Wakati marehemu Mudarres aliponusurika jaribio la mauaji lililofanyika kwa amri ya mfalme Reza Khan alituma ujumbe akiwa hospitalini na kusema: Mwambieni Shah kwamba mimi ningali hai. Hivi sasa pia Mudarres huko hai. Watu adhimu katika historia hubakia hai siku zote. Watu wabaya wanapaswa kuelewa kwamba, Hashemi ataendelea kuwa hai maadamu harakati iko hai", mwisho wa kunukuu.

Ayatullah Mudarres anayezungumziwa hapa katika ujumbe huo wa Imam Khomeini alikuwa miongoni mwa wanamapambano wakubwa dhidi ya utawala wa kifalme nchini Iran na aliokoka jaribio la kutaka kumuua, akapelekwa uhamishoni na hatimaye aliuuawa shahidi kwa amri ya mtawala Reza Khan.

Lengo kuu la vinara wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kipindi hicho ambapo uhasama na uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ulikuwa umepamba moto, lilikuwa kuimarisha misingi na nguzo za mfumo mchanga ya Kiislamu. Mwanzoni kabisa mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Rafsanjani alipewa jukumu la kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani. Akiwa katika nafasi hiyo, Rafsanjani alitekeleza jukumu muhimu sana ambalo lilikuwa kusimamia uchaguzi wa kwanza wa rais nchini Iran baada ya kuondolewa madarakani utawala wa kifalme uliotawala Iran kwa kipindi cha miaka elfu mbili na mia tano (2500). Baada ya hapo Rafsanjani alijiuzulu cheo cha Waziri wa Mambo ya Ndani kwa shabaha ya kugombea ubunge katika duru ya kwanza ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na akachaguliwa kuwa Spika wa Bunge hilo. Misimamo ya Rafsanjani kama Spika wa Bunge na ushawishi wake katika kupinga au kupasisha maazimio na sheria mbalimbali vilikuwa na taathira kubwa kiasi kwamba, wakati huo alitajwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa kiongozi nambari mbili wa Iran baada ya Imam Ruhullah Khomeini.

Marehemu Bazargan, Imam Khomeini na Ayatullah Rafsanjani

Ayatullah Rafsanjani aliendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha misingi na nguzo za mfumo mchanga wa Kiislamu nchini Iran mbele ya tufani na migogoro ya aina mbalimbali. Miongoni mwa migogoro na changamoto kubwa zilizojitokeza katika kipindi hicho ni kufichuka kwa usaliti wa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bani Sadr katika kipindi kigumu cha vita na mashambulizi ya Saddam Hussein dhidi ya Iran. Mwanzoni mwa mwaka 1981 nchi ilikuwa katika kipindi kigumu na nyeti mno. Baada ya kushika hatamu za urais, Bani Sadr alizusha hitilafu nyingi na kubwa kati ya mirengo mbalimbali ndani ya mfumo na utawala na kupuuza maslahi ya Jamhuri changa ya Kiislamu. Alijikurubisha zaidi kwa kundi la kigaidi la MKO katika jutihada za kuimarisha nafasi yake na kuwafutilia mbali wafuasi na wasaidizi wa karibu wa Imam Khomeini. Makundi ya wanamgambo wa MKO waliyojumuisha wanamgambo wasichana na wavulana yaliwekwa chini ya mamlaka ya Bani Sadr. Hapa ndipo yalipobainika malengo ya Bani Sadr na kuondoka kwake katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika hatua ya kwanza na kukabiliana na harakati hiyo iliyokuwa dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu, hayati Imam Khomeini alimuuzulu Bani Sadr kutoka kwenye cheo cha Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Iran, kisha Bunge lililokuwa likiongozwa na Spika Hashemi Rafsanjani likapiga kura ya kutokuwa na imani na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kiislamu. Baada ya kuuzuliwa Bani Sadr, kundi la MKO liliingia katika awamu nyingine kwa kuanzisha mashambulizi ya silaha kama njia ya kupinga Mapinduzi ya Kiislamu. Mauji ya kigaidi na milipuko ya mabomu ilishamiri kote nchini. Jaribio la kutaka kumuua Ayatullah Ali Khamenei ambaye wakati huo alikuwa Imam wa Swala ya Ijumaa ya Tehran, mlipuko mkubwa uliolenga Ofisi ya Kuu ya Chama cha Jamhuri ya Kiislamu na kuuliwa shahidi Ayatullah Muhammad Beheshti aliyekuwa Mkuu wa Vyombo vya Mahakama akiwa pamoja na viongozi wengine 72 wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu katika shambulizi hilo, shambulizi na bomu lililolenga Ofisi ya Waziri Mkuu na kuwaua shahidi Rais wa nchi, Muhammad Rajai na Waziri wake Mkuu Dakta Muhammad Bahonar ni mifano ya wazi ya jinai na uhalifu uliofanywa na kundi hilo katika kipindi hicho. Wakati huo Rafsanjani na wanamapinduzi wenzake walikuwa na nafasi kubwa na muhimu sana katika kuiondoa nchi kwenye kipindi hicho kilichojaa migogoro na changamoto nyingi.  

Imam Khomeini, Ayatullah Khamenei na Ayatullah Rafsanjani

Katika kipindi hicho suala muhimu zaidi lilikuwa kukabiliana na mashambulizi ya utawala wa kibaath wa Saddam Hussein dhidi ya Iran. Kutokana na hitilafu zilizokuwa zimesababishwa na Bani Sadr ndani ya jeshi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu wakati huo Ayatullah Ali Khamenei alimwandikia barua Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran, Imam Ruhullah Khomeini akipendekeza kwamba masuala yote yanayohusiana na jeshi yakabidhiwe kwa mtu mmoja ili kuepusha migongano na hitilafu katika medani za vita. Ayatullah Khamenei alisema katika barua hiyo kwamba mtu mwenye uwezo zaidi wa kushika nafasi hiyo ni Bwana Hashemi Rafsanjani. Imam Khomeini alikubaliana na pendekezo hilo la kumteua Rafsanjani kuwa Kamanda Mkuu wa Majeshi yote ya Iran. Rafsanjani ambaye kipindi hicho alikuwa pia Spika wa Bunge alikuwa na majukumu mazito katika medani ya siasa na handaki za mapambano dhidi ya utawala vamizi wa Iraq.

Katika makala ijayo ambayo tutatupia jicho jinsi vita hivyo vilivyomalizika, kipindi cha tukio chungu la kuaga dunia Imam Ruhullah Khomeini na jinsi Ayatullah Ali Khamenei alivyochaguliwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na hayati Imam, na nafasi mpya ya Rafsanjani baada ya vita vya kulazimishwa na kuanza kipindi cha harakati ya ujenzi wa nchi.