Iran, nchi ya tatu kuidhaminia Iraq mahitaji yake ya msingi
https://parstoday.ir/sw/radio/iran-i28422-iran_nchi_ya_tatu_kuidhaminia_iraq_mahitaji_yake_ya_msingi
Licha ya kuwepo historia chungu ya vita vya kulazimishwa baina yao, lakini nchi mbili jirani za Iran na Iraq hivi sasa zimefungua ukurasa mpya wa mashirikiano.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Apr 29, 2017 20:50 UTC
  • Iran, nchi ya tatu kuidhaminia Iraq mahitaji yake ya msingi

Licha ya kuwepo historia chungu ya vita vya kulazimishwa baina yao, lakini nchi mbili jirani za Iran na Iraq hivi sasa zimefungua ukurasa mpya wa mashirikiano.

Katika miaka ya hivi karibuni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha kwamba haina nia yoyote ya kuingilia wala kuichokoza nchi yoyote jirani na imekuwa ikifanya juhudi kadiri ya uwezo wake ili kukidhi mahitaji ya nchi hizo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inauchukulia usalama na uthabiti wa nchi jirani kuwa usalama na uthabiti wake yenyewe na mtazamo huo hauhusiana na Iraq tu bali unahusiana na majirani zake wengine wote ikiwemo Afghanistan. Iran inayatambua vyema matatizo ya Iraq na majirani zake wengine na hivyo kufanya juhudi kubwa za kutatua matatizo hayo yakiwemo ya umeme, madawa, chakula na kushiriki vilivyo katika ukarabati wa nchi hiyo. Mwenendo wa kiuchumi na kibiashara wa Iran na Iraq umeimarika sana katika kipindi cha miaka 13 iliyopita, yaani tokea wakati wa kung'olewa madarakani utawala dhalimu wa Saddam Hussein. Mwaka uliopita Iran ilikuwa nchi ya tatu kuuza bidhaa zake nchini Iraq na bila shaka mkondo huo umeimarika tokea wakati huo. Kati ya bidhaa za thamani ya dola bilioni 13 zilizouzwa mwaka uliopita nchini Iraq dola bilioni 6.2 kati ya hizo zilizotokana na uuzaji wa bidhaa za Iran zisizo za mafuta.

Maonyesho ya baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa nchini Iran

Kuwepo vivuko rasmi na visivyo rasmi 18 katika mpaka wa pamoja ulio na urefu wa kilomita 1400 kati ya nchi mbili kumeifanya Iran kuwa moja ya nchi muhimu zinazouza bidhaa zao nchini Iraq. Kuhusiana na suala hilo maonyesho mahususi ya tatu ya bidhaa za Iran yalifanyika katika uwanja wa kimataifa wa maonyesho ya bidhaa mjini Baghdad mwezi Februari mwaka huu. Katika mazungumzo aliyofanya na Salman Ali Al-Jumaili, Waziri wa Mipango ambaye pia anasimamia Wizara ya Biashara ya Iraq katika ufunguzi wa maonyesho hayo, Muhammad Ridha Ne'matzadeh, Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran alisisitiza kuwa Iran iko tayari kuendelea kushirikiana na nchi jirani ya Iraq katika ukarabati wa miji, miundombinu na pia kudhamini bidhaa za msingi zinazohitajika na wananchi wa nchi hiyo. Ushirikiano huo hivi sasa umeenea hadi kwenye sekta muhimu ya afya na tiba.

Hassan Qadhizadeh Hashemi, Waziri wa Afya na Tiba wa Iran

Mwaka 2015 Mawaziri wa Afya wa nchi mbili hizi walitiliana saini hati ya ushirikiano ambapo kudhaminiwa madawa ya Iraq na mashirika ya kutengeneza madawa ya Iran ni moja ya vipengee vya hati hiyo ya ushirikiano. Kwa msingi huo Hassan Qadhizadeh Hashimi, Waziri wa Afya na Tiba wa Iran alisafiri kwenda Iraq wiki iliyopita ambapo akiwa na waziri mwenzake wa nchi hiyo Adileh Hamoud, alisisitiza juu ya kuimarishwa ushirikiano wa seketa ya afya na tiba ya Iran nchini Iraq. Katika safari hiyo maonyesho mahususi ya bidhaa za afya na tiba za Iran yalifunguliwa mjini Baghdad. Katika mazungumzo hayo, Waziri Adileh Hamoud alishukuru mchango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuiunga mkono Iraq katika vita vyake dhidi ya ugaidi na kuongeza kuwa katu wananchi wa nchi hiyo hawatasahau mchango huo unaotolewa katika mazingira magumu sana.

Uharibifu mkubwa uliofanyika Iraq kutokana na mashambulio ya magaidi na uvamizi wa kigeni

Kupelekwa gesi na umeme nchini humo pia ni miongoni mwa nyanja za ushirikiano kati ya nchi mbili hizi. Miamala hiyo bila shaka inasisitiza wazi kwamba nchi mbili hizi za Kiislamu zimeazimia kunyanyua kiwango cha ushirikiano wao katika nyanja zote. Biashara, ushirikiano wa kitiba, vyuo vikuu, maendeleo na ustawi, mapambano dhidi ya uchafuzi wa hali ya hewa, ushirikiano wa kiulinzi kwa ajili ya kupambana na ugaidi na kulinda usalama ni miongoni mwa nyanja muhimu zaidi katika ushirikiano huo.