Imam Khomeini (ra), Mhuishaji wa dini katika ulimwengu wa sasa
Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji. Tuko katika siku za kukumbuka kufariki dunia Imam Khomeini (MA) ambaye ni muanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Huyu ni shakhsia na mwanazuoni ambaye kuaga kwake dunia mnamo tarehe 3 Juni mwaka 1989 kuliuacha Ulimwengu wa Kiislamu ukiomboleza na kulifanya taifa la Iran kuikumbuka siku hii kuwa mojawapo ya siku za majonzi makubwa katika historia yake. Imam Khomeini akiwa mhuishaji mkubwa wa misingi na mafundisho ya Kiislamu, alianzisha na kuendesha moja ya harakati kubwa zaidi za wananchi za kupigania uadilifu katika karne hii na kuuarifisha Uislamu kuwa dini inayomtatulia mwanadamu matatizo yake yote pamoja na kumuongoza kuelekea wokovu wa milele. Tunakumbuka na kumuenzi mwanazuoni huyu mkubwa wa Kiislamu ambaye kutokana na uono wake wa kina na imara kuhusiana na masuala ya kiitikadi na imani ya Mwenyezi Mungu, aliweza kuziteka nyoyo za watu na kuwavutia kwa kiwango kikubwa. Bila shaka kuenziwa na kukumbukwa mwanazuoni huyo kunafungamana kikamilifu na kufahamu vyema fikra na itikadi zake katika kuhuisha thamani za kidini. Endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa mnasaba huo.
*****
Dini na thamani zake zinatajwa kuwa msingi wa maisha ya mwanadamu kutokana na kuwa humletea kiumbe huyo saada na uokovu hapa duniani na huko Akhera. Yaani sifa ya uhai na uhuishaji inafungamana moja kwa moja na dini. Kuhusiana na jambo hili Qur'ani Tukufu inasema kama ifuatavyo katika aya ya 24 ya Surat al-Anfaal: Enyi mlioamini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapokuitieni jambo litakalokupeni uhai.
Ni wazi kuwa wito wa Mwenyezi Mungu hapa unahusiana na dini, thamani zake za juu na uhai wa kimaanawi. Jambo tunalopasa kulifahamu vyema ni kwamba hata kama dini ni msingi wa maisha ya mwanadamu lakini ni wazi kuwa inaweza kupotoshwa na kutiwa ndani yake bidaa yaani mambo ya uzushi ambayo hayana asili katika dini. Hapa ndipo umuhimu wa uhuishaji kwenye dini unapohitajika. Pamoja na kuwa ni vigumu kufuta misingi na nguzo za dini wala kuondolewa miongoni mwa watu, lakini ni wazi kuwa baadhi ya wakati watu hushindwa kufahamu vyema na kwa njia sahihi masuala ya kidini. Ni baada ya kupotoshwa baadhi ya mambo ndipo watu hukosea na kuwa na mtazamo potevu na finyu kuhusiana na dini na thamani zake. Maneno ya Imam Khomeini katika wasia wake wa kisiasa na kidini kuhusiana na uhuishaji wa Qur'ani Tukufu yanabainisha wazi suala hili. Hii ni kwa sababu kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA), hakika ya Qur'ani, ambacho ni kitabu cha mbinguni cha Waislamu, ni hai na ya kudumu milele lakini huenda baadhi ya watu wakawa na uelewa finyu na usio na uhai kuhusiana na thamani za kitabu hiki kitakatifu.
Kuhusiana na suala hili, mwanazuoni huyu mashuhuri wa Kiislamu anasema: "Sisi na taifa letu tukufu ambalo linaamini kwa dhati Uislamu na Qur'ani tunajivunia kuwa wafuasi wa madhehebu ambayo inataka kuondoa Qur'ani Tukufu makaburini, madhehebu ambayo inahubiri umoja kati ya Waislamu bali wanadamu wote, na kuifanya kuwa mwokozi mkubwa wa jamii ya mwanadamu. Madhehebu hii inataka kukata na kuondoa vizuizi vyote vilivyowekwa kwenye miguu, mikono, nyoyo na akili za wanadamu na kuwaelekeza kwenye maangamizi na utumwa kwa ajili ya mataghuti." Kwa msingi wa maneno hayo, Imam Khomeini aliichukulia Qur'ani Tukufu na dini kuwa hakika iliyo thabiti na imara, iliyo hai na ya kudumu milele na isiyokabiliwa na aina yoyote ya ombwe, upoozaji wala upotevu. Akiamini kuwa jambo linaloonekana kidhahiri humo kuwa ni upotevu na mgando, linatokana na mitazamo na fikra zetu dhaifu na zilizojaa makosa kuhusiana na Qur'ani na thamani za kidini.
&&&&&
Katika kipindi kirefu cha historia, fikra za kidini zimepoteza thamani yake halisi na kubadilika kutokana na masuala tofauti. Tunaweza kusema kuwa fikra hizi zimekuwa zikikabiliwa na hatari kutokana na masuala mawili muhimu. Moja ni watu walio na mitazamo finyu na ya kimgando ambao daima hujaribu kutoa fikra pungufu, potevu na duni kuhusiana na dini na thamani zake badala ya kutoa fikra sahihi, halisi na za thamani ya juu kuhusiana na dini ya Kiislamu. Wao huibana dini ya Mwenyezi Mungu na thamani zake katika mitazamo yao finyu na isiyo na upeo wa mbali. Mitazamo hii inaonekana wazi hii leo katika makundi ya Kiwahabi na kitakfiri. Katika upande mwingine upotofu katika dini husababishwa na maadui waovu wanaoabudu dunia ambao huhujumu misingi na thamani za kidini kwa kutumia kila mbinu. Maadui hao huhujumu thamani na misingi maalumu ya kidini kama kupigania uadilifu na kupambana na dhulma kwa kuiona inakinzana na matakwa yao ya matamanio ya nafsi, uhuru wa kufanya watakavyo na mielekeo yao ya kimabavu na kibeberu. Ni kutokana na ukweli huo ndipo waovu hao wakafanya juhudi kubwa za kuitenga dini katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Ili kufikia lengo hilo, wakati mwingine maadui hujaribu kutoa picha na taswira iliyopotoshwa kuhusiana na mafundisho ya Kiislamu ili yaendane na matamanio na matakwa yao ya kishetani.
Katika upande wa pili, kuna watu wema ambao wamesimama na kutumia nguvu zao zote katika kutetea Uislamu halisi na thamani zake za juu. Wamekuwa wakifanya hivyo kwa lengo la kurekebisha jamii na hata kuwa tayari kutoa muhanga roho zao kwa madhumuni ya kufikia lengo hilo tukufu. Imam Khomeini (MA) pia alikuwa mujahid mwaminifu na mwanazuoni mwenye mwamko ambaye aliendesha mapambano makubwa ya kifikra na kivitendo kwa lengo la kuhuisha dini na thamani zake. Alikuwa kiongozi ambaye kwa kutumia mafundisho ya kidini, hatimaye alifanikiwa kuuangusha utawala jabari wa kitaghuti na kusafisha kutu na vumbi lote la bidaa na fikra mgando katika Uislamu. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni mfano bora na wa wazi zaidi wa harakati ya kivitendo ya Imam Khomeini (MA) kwa madhumuni ya kuhuisha Uislamu na thamani zake katika ulimwengu wa leo. Jambo lililompa Imam moyo wa kuanzisha mapambano ya kubadilisha hali iliyokuwepo nchini ni kutozingatia jamii ya wakati huo ya Iran mafundisho ya dini. Kwa kadiri kwamba jambo hilo lilileta madhara makubwa ya kiitikadi na kidini kwenye jamii. Uislamu ulikuwa ukifasiriwa na kueleweka kimakosa kwamba haukupasa kujishughulisha na masuala ya kisiasa, kijamii wala kiutamaduni, bali ilipasa tu kushughulikia baadhi ya masuala ya kiibada na ya mtu binafsi. Fikra hii ndiyo iliyoenezwa nchini na watawala dhalimu na wa kidikteta wa wakati huo pamoja na mabwana zao wa Magharibi. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA), jamii ya Kiislamu ilikumbwa na balaa na upotevu huu wa kifikra baada ya kuondoka duniani Mtume Mtukufu (saw), upotevu ambao ulifikia kilele katika uhai wa Imam mwenyewe. Kuhusu jambo hili Imam Khomeini anasema: “Hii imekuwa ni njama ya kishetani ambayo ilianza kutekelezwa katika zama za watawala wa Bani Umayya na Bani Abbas na kuendelea. Kila utawala ulioingia madarakani ulifuata mkondo huohuo na hivi karibuni baada ya madola ya Magharibi na Mashariki kuingia katika nchi za Kislamu, njama hii ilifikia kilele chake ambapo ilidaiwa kuwa Uislamu ni suala la mtu binafsi na Mungu wake na kwamba unapasa kutenganishwa na siasa. Waislamu walitakiwa kujiepusha na siasa na wala wanazuoni wa Kiislamu hawakuruhusiwa kujishughuisha na masuala ya kisiasa.” Mwisho wa kunukuu.
********
Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Khomeini alitumia uwezo wake wote kukabiliana na pote hili la kueneza fikra potevu na finyu katika Uislamu na hasa fikra ya kutenganisha dini na siasa iliyokuwa ikienezwa nchini na vibaraka wa madola ya kibeberu ya Magharibi. Alisisitiza kwamba siasa hii mbovu ililenga kuwafanya Waislamu wapooze na hivyo kutofuatilia masuala yenye umuhimu mkubwa maishani mwao. Katika kufikia lengo lake hilo tukufu Imam Khomeini (MA) aliiga na kufuata kikamilifu sira ya Mtume Mtukufu (saw) na Ahlul Beit wake watoharifu (as). Kwa kufuata sunna hiyo ya Mtume alifanikiwa pakubwa katika juhudi zake za kuhuisha dini na hivyo kuleta uhai mpya katika maisha ya kila siku ya kisiasa na kijamii ya wananchi wa Iran. Alikuwa akisisitiza sana juu ya umuhimu wa kuasisiwa dola la Kiislamu na kuongeza kuwa ni kwa kuanzisha dola la Kiislamu tu ndipo Mtume alifanikiwa kutekeleza uadilifu katika jamii. Alisema Mtume alitumia umri wake wote katika kuasisi dola la Kiislamu.
Imam Khomeini (MA) alikuwa akiamini kwamba serikali ya Kiislamu ni chombo cha kufikiwa malengo matukufu kama vile kupambana na dhulma na kuwanusuru wanyonge.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tumefikia mwisho wa kipindi hiki maalumu. Natumai tumenufaika sote vya kutosha. Basi hadi wakati mwingine nakuageni kwa kusema, kwaherini.