Aug 19, 2023 13:55 UTC
  • Sura ya At-T’uur, aya ya 32-40 (Darsa ya 963)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 963 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 52 ya At-T’uur. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 32 hadi 34 ambazo zinasema:

أَمْ تَأْمُرُهُمْ أَحْلَامُهُم بِهَٰذَا ۚ أَمْ هُمْ قَوْمٌ طَاغُونَ

Au akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao ni watu waasi tu?

أَمْ يَقُولُونَ تَقَوَّلَهُ ۚ بَل لَّا يُؤْمِنُونَ

Au wanasema: Ameitunga hii! Bali hawaamini tu! 

فَلْيَأْتُوا بِحَدِيثٍ مِّثْلِهِ إِن كَانُوا صَادِقِينَ

Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoakisi maneno ya uzushi waliyokuwa wakiyasema wapinzani wa Bwana Mtume SAW dhidi ya mtukufu huyo. Aya hizi tulizosoma zinawauliza watu hao: hizo akili zenu timamu ndizo zinazokutumeni mropoke hayo mnayoropoka ya kumuita kuhani, mshairi na mwendawazimu Mtume wa Mwenyezi Mungu anayesema nanyi kwa hoja na mantiki kamili? Hakuna sababu nyingine ya kukufanyeni mseme maneno hayo isipokuwa hisia za kujikweza na kuonyesha uasi na jeuri mbele ya haki. Kwa kuwa hamtaki kumwamini Mtume, mumeamua kumzushia tuhuma kwamba ameyanasibisha na Mwenyezi Mungu mambo aliyowaza na kujibunia yeye mwenyewe. Kama ni kweli, na nyinyi pia fanyeni hivyo kwa kuleta maneno yanayofanana na hayo aliyokuja nayo yeye. Onyesheni kwamba anayodai yeye si ya kweli, kwa sababu watu wengine pia wanao uwezo wa kuleta maneno, kama anayoyasema yeye. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, chimbuko hasa la ukafiri na ukanushaji ni uasi na jeuri mbele ya haki, si kutafakari na kutumia mtu akili yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wapinzani wa Mitume walikuwa wakiibua kila aina ya tuhuma na uzushi dhidi yao ili kutetea na kuhalalisha ukafiri na ukanushaji wao na kuwafanya watu wasiwaamini na kuwafuata wajumbe hao wa Allah. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Qur'ani ni muujiza wa wazi kabisa wa Bwana Mtume SAW wa kuthibitisha ukweli wa Utume wake. Kwa hivyo kama wanaompinga wanao uwezo, na walete kitabu kilicho mfano wa Qur'ani.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 35 na 36 ambazo zinasema:

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ

Au wao wameumbwa pasipo kutokana na chochote, au wao ndio waumbaji (wa nafsi zao)?

أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ

Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawaitafuti yakini. 

Aya hizi zinaashiria moja ya burhani na hoja za kumjua Mwenyezi Mungu inayojulikana kama burhani ya kisababishi. Burhani hiyo inasema hivi: hakuna kisababishwaji chochote kinachoweza kuwepo bila ya kupatikana sababu au kisababishi chake; na hakuna kisababishwaji chochote kinachoweza kuwa kisababishi cha nafsi yake chenyewe; kwa hivyo kinahitaji kitu kingine kuwa sababu au kisababishi cha kuwepo kwake. Kwa kuzingatia kuwa vitu vyote vya mbinguni na ardhini viko namna hivi, kwa hiyo mwisho wa yote italazimu kufikia kwenye sababu au kisababishi ambacho chenyewe hakina sababu au msababishaji, vyenginevyo tutaishia kwenye mzunguko usio na mwisho, jambo ambalo halikubaliki katika akili na mantiki. Kwa upande mwingine, hakuna mwanadamu yeyote anayedai kuwa yeye ameumbika vivi hivi tu pasi na sababu au kisababishi kilichopelekea yeye kuwepo. Halikadhalika, hakuna mtu anayeweza kudai kwamba yeye alijiumba mwenyewe. Kuthibiti kwa dhana mbili hizi ni jambo muhali na lisiloyumkinika kiakili. Na sababu yake ni kwamba mwanadamu ni kitu kilichopo; na kila kilichopo kinahitaji sababu ya kuwepo kwake. Isitoshe, itawezekanaje kwa kiumbe mwanadamu ambaye hakuwepo hapo kabla, awe sababu na kisababishi cha kuwepo yeye mwenyewe!? Kwa hivyo hitajio la kuwepo Muumba ni jambo la kifitra na kimaumbile na la mantiki na kiakili, ambalo hata washirikina wa Makka pia walilikubali na hawakuwa wakilikana. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur’ani Tukufu inaibua baadhi ya masuali ya kuwatafakarisha na kuwataamalisha wanadamu ili wajitambue; na kwa kuziamsha fikra na dhamiri zao waache ukaidi na upinzani wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama mwanadamu atakuwa na nia ya kutaka kuujua ukweli na kuukubali, basi akili yake itamuongoza na kumfikisha kwenye lengo hilo. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, mwanadamu si muumbaji wa nafsi yake, wala si muumba wa mbingu na ardhi. Vilevile aya hizi zinatuonyesha kuwa, ikiwa mwanadamu atatafakari juu ya uumbwaji wake yeye mwenyewe na wa ulimwengu, basi tafakuri hiyo itamfikisha kwa Mwenyezi Mungu SWT na kumpa hakikisho na yakini ya kumtambua Muumba wake.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 37 hadi ya 40 ya sura yetu ya At-T’uur ambazo zinasema:

أَمْ عِندَهُمْ خَزَائِنُ رَبِّكَ أَمْ هُمُ الْمُصَيْطِرُونَ

Au wanazo hazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye mamlaka (ya ulimwengu)?

 أَمْ لَهُمْ سُلَّمٌ يَسْتَمِعُونَ فِيهِ ۖ فَلْيَأْتِ مُسْتَمِعُهُم بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ

Au wanayo ngazi ya kusikilizia (siri za mbinguni)? Basi huyo msikiaji wao na alete hoja iliyo wazi! 

أَمْ لَهُ الْبَنَاتُ وَلَكُمُ الْبَنُونَ

Au Yeye (Mwenyezi Mungu) ana mabanati, na nyinyi ndio mna wavulana? 

أَمْ تَسْأَلُهُمْ أَجْرًا فَهُم مِّن مَّغْرَمٍ مُّثْقَلُونَ

Au (wewe) unawaomba ujira, kwa hivyo wanaelemewa na gharama? 

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizopita kwa kuwatupia masuali mengine wapinzani wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Kwa kuanzia zinawaambia: kama mnakubali kwamba nyinyi si waumbaji wa nafsi zenu wala wa ulimwengu, je, ni nyinyi ndio mliokabidhiwa mamlaka ya uendeshaji mambo ya ulimwengu na ya watu pamoja na ugawaji wa neema na riziki? Hivi nyinyi mnatarajia Mwenyezi Mungu amteue kuwa Mtume mtu mnayemtaka nyinyi au amkabidhi jukumu hili au majukumu ya masuala mengine ya kijamii mtu yeyote yule mumpendaye nyinyi? Je, wao wanayo njia ya kuwafikisha mbinguni itakayowawezesha kuelewa namna ya kuendesha masuala ya ulimwengu au kupata wahyi wa kuwaelekeza watu kwenye uongofu na kufanya mambo yao kwa kufuata wahyi huo wa Allah? Au wao wana hoja kuhusiana na khurafa na uzushi wao usio na msingi wanaomnasibisha nao Mwenyezi Mungu, kama kudai kwamba malaika ni mabanati wake Mola? Au kwa mfano, yeye Mtume amewaomba wao ujira na malipo kwa sababu ya kuwafikishia wito wake, na hilo likawawia vigumu kufanya na ndio maana hawako tayari kuukubali wito wake? Ni wazi kwamba jawabu za masuali yote hayo ni ‘hapana’; na wala wapinzani hawana hoja wala mantiki yoyote ya kutetea wanachokipinga. Wanachotafuta ni uchochoro wa kukimbilia kwa ajili ya kuikana na kuikataa haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ikiwa wapinzani wetu nao pia watakuwa na maneno ya mantiki, basi tuwe tayari kuyakubali, badala ya kuonyesha taasubi na ukereketwa usio na maana. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wale wanaofikia hadi ya kumnasibisha Allah na mambo yasiyofaa, kama kudai kwamba ati Yeye ana mabinti, hawajali kuwavurumishia Mitume pia tuhuma zozote zile wasizostahiki. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, katika tablighi ya dini, na kuwaongoza na kuwalingania watu haki, tufuate njia ya Mitume kwa kujiepusha na uombaji pesa au kutaka kwa watu vitu vya kimaada. Kufanya hivyo kutafifisha athari ya tablighi na vilevile kuwapa watu mbinyo na mashinikizo. Isipokuwa kama watu wataamua wenyewe kutoa msaada au kututunukia zawadi, hapo hakutakuwa na ubaya wa kuipokea. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 963 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, azijaze ikhlasi nyoyo zetu na atutakabalie amali zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags