Aug 21, 2023 16:24 UTC
  • Mchango wa Maulamaa (76)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kwa pamoja kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 76 ya mfululizo huu kitamzungumzia Shekhe Muhammad Khiabani, mwanazuoni na mwanaharakati ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika Mapinduzi ya Katiba na matukio ya baada ya hapo katika mji wa Tabriz nchini Iran. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Shekhe Muhammad Khiabani alizaliwa mwaka 1297 Hijria mwafaka na 1880 katika mji wa Khameneh, moja ya miji ya mkoa wa Azarbaijan Mashariki nchini Iran. Baba yake alikuwa mfanyabiashara na alikuwa akifanya biashara katika mji mkuu wa Jamhuri ya Dagestan. Baada ya kumaliza elimu yake ya msingi, Muhammad alitumia muda fulani kwenye kituo cha biashara cha baba yake, akijifunza siri za biashara, lakini taratibu alitambua kwamba roho yake iliendana zaidi na kusoma elimu na maarifa, hivyo aliiacha biashara hiyo na kurudi Khameneh. Sheikh Mohammad Khiabani alianza kusoma masomo ya dini huko Tabriz na, tofauti na wanafunzi wengine, hakutosheka na kusoma na kujifunza fiqhi na usul tu, bali sambamba na masomo hayo alisoma hisabati, historia, fasihi, unajimu na falsafa. Tangu alipoanza kusoma masomo ya dini alikuwa na shauku kubwa ya kuandika kalenda na alikuwa na uwezo mkubwa wa kutatua matatizo masuala magumu zaidi ya elimu ya jiometri.

Sheikh Muhammad Khiabani

 

Kulingana na desturi za zamani za Hawza (Chuo cha Kidini), Muhammad Khiabani kila kitu alichojifunza alikifundisha kwa wanafunzi wanagenzi na vijana, lakini kati ya elimu zote, alipenda sana kufundisha elimu ya nujumu na hisabati miongoni mwa elimu ngumu zaidi. Ufasaha, mbinu na mtindo wake katika kufundisha elimu hizi, ufikishaji wake na usahihi wa hali ya juu wa kielimu sambamba na umakini wa hali ya juu aliokuwa nao katika kufundisha elimu hizi kuliwafanya sio tu wanafunzi wanagenzi, bali pia wasomi na Maulamaa kuvutiwa na masomo yake na kusifia ustadi wake wa kufundisha. Sheikh Muhammad aliishi katika kitongoji kimoja cha mji wa Tabriz kilichojulikana kwa jina la Khiaban. Alikuwa akiswalisha Sala ya Jamaa katika msikiti wa Karim Khan, ambao ulikuwa katika mtaa huo huo, na ni kutokana na sababu hiyo alijulikana kwa jina la Sheikh Mohammad Khiabani.

Kufunga kwake ndoa na binti wa mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Tabriz yaani Seyyid Hussein Khamenei, kulimfanya kuwa maarufu zaidi. Wakati fulani alikuwa akisalisha na kutoa hotuba katika Msikiti Mkuu wa Tabriz badala ya baba mkwe wake. Kwa muktadha huo, tangu ujana wake Sheikh Khiabani alikuwa akiwasiliana na umma kwa ujumla kupitia mimbari na kusalisha na alikuwa akiwaeleza na kuwabainishia masuala ya kidini, kielimu, kiutamaduni na kijamii.Wakati kujiri wa Mapinduzi ya Katiba, Sheikh Muhammad Khiabani alikuwa mmoja wa wanachama hai wa Jumuiya ya Mji wa Tabriz na alikuwa  nafasi na mchango usio na kifani katika kuendesha na kusimamia mambo ya mji huo. Kuwepo kwake pamoja na wapiganaji wengine, miongozo na hotuba zake za Kimapinduzi ni mambo ambayo yaliwatia moyo wapiganaji na Mujahidina na kuongeza muqawama na mapambano yao.

Nyumba ya Sheikh Khiabani katika kitongoji cha Khiaban katika mji wa Tabriz

 

Muhammad Ali Shah Qajar, mfalme wa wakati huo wa Iran ambaye alikuwa akipinga mapinduzi ya kikatiba, alituma jeshi la watu 40,000 kwenda kupigana na wapigania katiba wa Tabriz, lakini hakuweza kusambaratisha muqawama wa wananchi wa Tabriz, hivyo ili kukidhi mahitaji ya kifedha ya vita aliamua kuomba mkopo kutoka kwa madola ya kigeni. Wanachama wa Jumuiya ya Jimbo la Tabriz walipinga vikali uamuzi huu wa Shah, na kwa pendekezo la Sheikh Muhammad Khiabani, walituma telegrafu kwa Seneti na Baraza la Kitaifa la Ufaransa, ambapo walitangaza kwamba: "Katika kipindi hiki katika wakati Bunge la Taifa la Iran limefungwa na Shah, aina yoyote ya mkopo utakaochukuliwa kutoka kwa serikali za kigeni bila ya idhini ya Bunge, taifa la Iran haliko tayari kulipa mkopo huo!" Malalamiko haya yalipelekea Shah Qajar kushindwa tena na wapigania  katiba.

Baada ya kuundwa Bunge la Pili la Taifa, Sheikh Muhammad Khiabani aliingia kwenye Bunge hilo akiwa mwakilishi wa wananchi wa Tabriz. Wakati huo Mmarekani Morgan Shushter alikuwa amekuja nchini Iran akiwa mwakilishi wa nchi isiyoegemea upande wowote baada ya hilo kupasishwa na Bunge ili aweze kushughulikia na kuboresha matatizo ya kifedha yaliyotokana na uwepo wa Uingereza na Russia nchini Iran. Uwepo wake nchini Iran haukuwa ukiafikiana na  kwa vyovyote vile na sera za kikoloni za Urusi na Uingereza, kwa hivyo Urusi ilitaka afukuzwe kutoka Iran. Wawakilishi wa Bunge walikuwa wakipinga vikali takwa hilo la Urusi kwani lilikuwa likienda kinyume na mamlaka ya kujitawala nchi. Hatimaye na licha ya upinzani wa wawakilishi wa Bunge, serikali ya muda ya wakati huo ilichukua uamuzi wa kumfukuza Iran Mmarekani Morgan Shuster. Serikali ikalifunga Bunge na kuwatia mbaroni wawakilishi wa mrengo wa upinzani.

Vosugh od-Dowleh

 

Sheikh Muhammad Khiabani ambaye alikuwa mmoja wa wapinzani wakubwa wa Russia, akiwa na lengo la kusalimika alilazimika kuelekea Caucasia. Baada ya muda alirejea Tabriz. Kurejea kwake Iran kulisadifiana na kukaliwa kwa mabavu mji wa Tabriz na Warusi kulikoambatana na ukandamizaji wa kisiasa kiasi kwamba, Sheikh Khiabani aliona bora alijihusishe na masuala ya biashara kwa muda fulani.

Baada ya Mapinduzi ya Russia mwaka 1917 na kurejea nyuma kwa Warusi kutoka mikoa tofauti ya Iran, kukajitokeza anga na mazingira ya harakati za kisiasa za wapigania uhuru. Shekhe Khiabani alitumia neema ya uhuru na kuwakusanya marafiki zake wapigania uhuru na kupigana na kuunda jumuiya. Asasi hiyo ilijulikana kwa jina la Kamati ya Mrengo wa Demokrasia. Mbali na kufanya hima ya kuinua kiwango cha ufahamu wa wananchi, Sheikh Khiabani alijitahidi pia kushughulikia matatizo yao. Kwa msingi huo, mbali na harakati za kisiasa na kiutamaduni kama kusambaza gazeti lililokuwa na jina la Tajaddod, alikuwa na mchango mkuybwa pia katika kudhamini ustawi na utulivu wa wananchi.

Nyumba ya makumbusho ya Sheikh Muhammad Khiabani

 

Mwaka 1919 kukaanza kufanyika uchaguzi wa Bunge la nne. Katika kipindi hiki, Waziri Mkuu Vosugh od-Dowleh alikuwa akitaka kusaini mkataba wa kikoloni na Uingereza. Kwa mujibu wa mkataba huo ambao ni maarufu kama mkataba 1919, mamlaka kamili ya masuala ya kifedha, forodha na kijeshi ya Iran yangekabidhiwa kwa washauri wa Kiingereza na kivitendo Iran ingekuwa koloni la Uingereza. Baada ya kusambazwa hati ya mkataba huo, kukaibuka wimbi la malalamiko ya wananchi nchini Iran na Shekhe Muhammad Khiabani aliandika katika gazeti la Tajaddod: Madhali mkataba haujapasishwa na Bunge, basi hilo ni karatasi tu lisilo na itibari yoyote.

Hatua na harakati za Shekhe Khiabani zilimfanya Vosugh od-Dowleh kutafuta njia. Kwa kubadilisha wafanyakazi na maafisa wa idara na kuvuruga uchaguzi wa Tabriz, alihoji uhalali wa uchaguzi wa Azerbaijan, na Sheikh Mohammad Khayabani, licha ya kuwa alipata kura nyingi, hakuweza kuingia bungeni. Khiabani alifunga safari na kuelekea Tehran na akafanya juhudi za kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kwa mazungumzo. Hata hivyo baadaye alifahamu kwamba, hii ni njama ambayo haiwezi kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo, hivyo akarejea Tabriz na kuunda Bunge la kieneo huko Tabriz ili wananchi waweze kutoa maoni yao kwa njia ya kujitegemea kuhusiana na masuala ya kisiasa na kijamii. Baadhi wakamtuhumu kwamba, anapigania kujitenga lakini lengo lake lilikuwa ni kuendesha harakati ya malengo ya mapinduzi ya katiba. Hatimaye nyumba ya Shekhe Khiabani ilivamiwa na mwanaharakati huyo akauawa shahidi.

Kaburi la Shekhe Khiabani

 

Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu cha leo umefikia tamati ambapo tulitupia jicho kwa mukhtasari maisha na harakati za Shekhe Muhammad Khiabani, mmoja wa wanazuoni na wahakari wa Kiislamu aliyekuwa na mchango mkubwa katika matukio ya Kiislamu nchini Iran. Hadi tutakapokutana tena wiki ijayo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalaamu Aalaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh