Dec 01, 2023 09:53 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (37)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 37 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 37.

کُنْ سَمْحاً وَ لَا تَکُنْ مُبَذِّراً، وَ کُنْ مُقَدِّراً وَ لَا تَکُنْ مُقَتِّراً

Kuwa mkarimu wala usiwe mbadhirifu na kuwa mtu wa wastani wala usiwe bakhili.

Uislamu ni dini ya wastani na ni dini ya kati na kati. Qur'ani Tukufu na Sunnah za Mtume (SAW) na Ahlul-Bayt AS wote wanawahimiza watu kuwa na misimamo ya wastani katika kila kitu kwenye maisha yao. Wanachuoni wengi wa akhlaki ya Kiislamu wanapozungumzia umuhimu wa maadili mema, wanataja mipaka miwili kuwa ni kitu cha dharura yaaani kutopindukia mipaka iwe kwa sura chanya au kwa sura hasi yaani ifrat na tafrit. Kwa mfano, inasemwa kwamba ikiwa mtu hana woga hata chembe na ikawa kutoogopa kwake kumechupa mipaka, huyo tena huitwa mpuuzi haitwi tena shujaa. Ushujaa wa kuchupa mipaka unaokosa hikma na tahadhari, ni ujinga na upuuzi. Lakini vile vile kama mtu atakuwa kazi yake ni kufanya tahadhari kupindukia huyo huitwa mwoga na goigoi. Kila kitu kinataka kifanywe kwa kiasi chake. Na hivyo ndivyo inavyotufundisha dini tukufu ya Kiislamu. Kwa maana ya kwamba, mtu asiwe mwoga kupita kiasi, lakini pia asijifanye jasiri na shujaa kupindukia maana husababisha uharibifu. Ni hivyo hivyo, mtu anatakiwa awe mkarimu, lakini asiwe mbadhirifu na vile vile anatakiwa achukue tahadhari kwenye utoaji wake, lakini asijibane mpaka akawa bakhili. Ndio maana aya ya 67 ya Sura Furqan, Qur'ani Tukufu inatoa sifa za waja wema wa Mwenyezi Mungu ikisema: 

وَ الَّذِینَ إِذا أَنْفَقُوا لَمْ یُسْرِفُوا وَ لَمْ یَقْتُرُوا وَ کانَ بَیْنَ ذلِکَ قَواماً 

Na wale ambao wanapotumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.

Na wale ambao wanapotumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.

 

Ni vivyo hivyo, Imam Ali AS katika hikma hii ya 37 ya Nahjul Balagha ambayo kimsingi imetokana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu, anawausia watu wote kufanya mambo yao kwa wastani ikiwa ni pamoja na katika matumizi yao ya fedha. Anasema:

کُنْ سَمْحاً وَ لَا تَکُنْ مُبَذِّراً، وَ کُنْ مُقَدِّراً وَ لَا تَکُنْ مُقَتِّراً

Kuwa mkarimu wala usiwe mbadhirifu na kuwa mtu wa wastani wala usiwe bakhili.

Katika hekima hii, Imam ametumia maneno "Mubadhiran" na "Muqattiran" ambapo neno mubadhirra asili yake ni kupanda mbegu kutokana na neno tabdhir. Lakini kwa vile neno hilo limetumika kuzungumzia matumizi ya fedha na mali hapa, linawakusudia watu ambao wanatumia kwa ubadhirifu mali zao. Neno muqattira nalo linatokana na neno taqtir kwa maana ya kubana na wakati linapotumika kwa matumizi ya mali na fedha, huwa na maana ya ubakhili. 

Tab'an kuna baadhi ya mambo yanatoka kwenye kanuni hiyo nayo ni yale yanayohusina na mawalii wa Mwenyezi Mungu. Mtume mtukufu na Ahlul Bayt wake AS hawamo kwenye kanuni hii kwa maana ya kwamba, wao walikuwa wanatoa kila walicho nacho na kuanza upya kutafuta riziki. Kiwango hicho kikubwa na uzuhdi na kuitaliki dunia, wanakiweza tu mawalii wa Mwenyezi Mungu kutokana na hofu yao kubwa kupindukia kwa Muumba wao. Qur'ani Tukufu ina aya nyingi zinazozungumzia ukaribu wa kupindukia wa Ahlul Bayt AS. Mfano wa wazi kabisa ni kisa cha Bibi Fatimatuz Zahra SA na mumewe yaani Imam Ali na wanawe wawili yaani Hassan na Husain AS. Watukufu hao walisamehe chakula chote walichokuwa nacho kwa ajili ya kuwalisha maskini, yatima na mtumwa licha ya kwamba walifululiza siku tatu kwenye saumu bila ya kula chochote. Aya ya 8 ya Surat al Dahr inasema:

وَ یُطْعِمُونَ الطَّعامَ عَلى حُبِّهِ مِسْکِیناً وَ یَتِیماً وَ أَسِیراً

Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa.

Hayo lakini ni katika masuala yanayotoka nje ya mipaka ya kanuni jumla na wanaoyaweza ni mawalii wa Mwenyezi Mungu tu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags