Feb 27, 2024 02:30 UTC
  • Jumanne, tarehe 27 Februari, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 17 Sha'ban 1445 Hijria sawa na Februari 27 mwaka 2024.

Leo tarehe 8 Esfand katika kalenda ya mwaka wa Kiirabu ni siku ya kumbukumbuka na kumuenzi mwanafalsafa mkubwa wa Kiislamu na Kiirani, Mulla Hadi Sabzevari. 

Mulla Sabzevari anatambuliwa kuwa mwanafalsafa mkubwa zaidi wa Kiislamu wa karne ya 13.

Mulla Hadi Sabzevari alizaliwa mwaka 1212 Hijria na alitumiwa umri wake ulijaa baraka katika zuhdi na uchamungu. Athari za Mulla Hadi Sabzevari zinaonyesha kwamba, alimu huyo mkubwa wa Kiislamu mbali na kwamba alikuwa mmoja wa wanafalsafa wakubwa, pia alitabahari katika uwanja wa elimu ya sheria za Kiislamu (fiq'hi), tafsiri ya Qur'ani, mantiki, hisabati, fasihi na elimu ya tiba.

Miongoni mwa athari za mwazuoni huyo ni pamoja na 'Mandhumah' katika uwanja wa elimu ya mantiki, 'Asraarul-Hikam' na 'al-Jabru Wal-Ikhtiyaar.'

Mulla Hadi Sabzevari

Katika siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, alizaliwa John Steinbeck mwandishi wa riwaya wa Kimarekani.

Katika kipindi cha ujana wake alijishughulisha na kazi mbalimbali kabla ya kuchagua kazi ya uandishi ambako alionesha kipawa kikubwa. Mashaka ya kimaisha yalimtayarishia John Steinbeck mazingira mazuri ya kueleza kwa ufasaha maisha ya watu dhaifu na maskini katika jamii ya Marekani.

Alikuwa hodari mno katika kueleza mandhari, matukio na hali mbalimbali. Steinbech ameandika vitabu vingi kama Of Mice and Men, Bombs Away na Cup of Gold.

John Steinbeck

Miaka 48 iliyopita katika siku kama hii ya leo Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara ilijitangazia uhuru. Jamhuri hiyo iko kaskazini magharibi mwa Afrika katika pwani ya Bahari ya Atlantic na ina ukubwa wa kilomita mraba laki mbili na 84 elfu na jamii ya watu karibu laki sita.

Jamii ya Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara inaundwa na watu wa kaumu mbalimbali za kiarabu, Barbar, Hassaniya na Tuareg. Mwaka 1975 wakoloni wa kihispania waliikabidhi ardhi ya Sahara kwa Morocco baada ya mapambano ya miaka mingi ya watu wa eneo hilo.

Baada ya kuondoka wakoloni wa Kihispania, harakati ya Polisario ilitangaza uhuru wa nchi hiyo kwa kuunda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu na kukataa utawala wa Morocco na Mauritania katika ardhi ya eneo hilo. Mwaka 1979 Mauritania pia ilitupia mbali madai ya kumiliki eneo hilo la Sahara lakini Morocco ingali inadai kuwa ni sehemu ya ardhi yake.

Lugha rasmi ya watu wa Sahara ni Kiarabu na asilimia 99 ya wakazi wake ni Waislamu.   

Katika siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, alifariki dunia Waziri Mkuu wa zamani wa Uturuki Najmuddin Erbakan akiwa na umri wa miaka 84.

Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Istanbul, Erbakan alijiunga na Chuo Kikuu cha Aachen nchini Ujerumani ambako alipata shahada ya uzamivu. Mwaka 1969 Najmuddin Erbakan aliingia katika uwanja wa siasa na kuchaguliwa kuwa Mbunge.

Mwaka 1987 aliongoza chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Refah ambacho kilipata viti vingi vya bunge na kumteuwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1996. Tukio hilo liliwakasirisha mno wanasiasa wa kilaiki wa Uturuki, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Serikali ya Erbakan ilipigwa vita na jeshi la Uturuki na miezi 10 baadaye chama cha Refah kilivunjwa na wanajeshi, na mwanasiasa huyo akapigwa marufuku kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa kipindi cha miaka 5. Profesa Najmuddin Erbakan anatambuliwa kuwa baba wa harakati ya Kiislamu ya Uturuki.   

Najmuddin Erbakan

Katika siku kama hii ya leo miaka 8 iliyopita aliaga dunia mtengezaji filamu mashuhuri wa Iran, Farajullah Salahshur. Alizaliwa mwaka 1331 Hijria Shamsia katika mji wa Qazvin.

Farajullah Salahshur, ametengeneza filamu nyingi maarufu kama ile ya kisa cha Maisha ya Nabii Yusuf (as), kisa cha As’habul Kahf na maisha ya Nabii Ayyub (as). Filamu hizo hasa ile ya kisa cha maisha ya Nabii Yusuf (as) zimewavutia watazamaji wengi duniani.

Kabla ya kufariki dunia, Salahshur alikuwa ameshaandika kisa cha filamu ya maisha ya Nabii Musa AS. Uchukuaji filamu ya kisa hicho ulipangwa kuanza miezi michache kabla ya kifo chake, lakini hilo halikuwezekana kutokana na ugonjwa wa saratani ya mapafu ulioishia kwenye kifo chake. 

Farajullah Salahshur

 

Tags