Hikma za Nahjul Balagha (41)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 41 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 40 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 37.
وَ قَدْ لَقِیَهُ عِنْدَ مَسِیرِهِ إِلَى الشَّامِ دَهَاقِینُ الْأَنْبَارِ فَتَرَجَّلُوا لَهُ وَ اشْتَدُّوا بَیْنَ یَدَیْهِ، فَقَالَ (علیه السلام): مَا هَذَا الَّذِی صَنَعْتُمُوهُ؟ فَقَالُوا خُلُقٌ مِنَّا نُعَظِّمُ بِهِ أُمَرَاءَنَا. فَقَالَ وَ اللَّهِ مَا یَنْتَفِعُ بِهَذَا أُمَرَاؤُکُمْ، وَ إِنَّکُمْ لَتَشُقُّونَ عَلَى أَنْفُسِکُمْ فِی دُنْیَاکُمْ وَ تَشْقَوْنَ بِهِ فِی [أُخْرَاکُمْ] آخِرَتِکُمْ؛ وَ مَا أَخْسَرَ الْمَشَقَّةَ وَرَاءَهَا الْعِقَابُ، وَ أَرْبَحَ الدَّعَةَ مَعَهَا الْأَمَانُ مِنَ النَّار.
Wakati Imam Ali (AS) alipokuwa safarini kuelekea Sham, wakulima na wanavijiji wa mji wa Anbar walikuja kumtembelea. Walishuka kwenye vipando vyao na kukimbilia kwake. Imam aliwauliza, ni kitu gani hiki mnachofanya? Wakasema hiyo ni desturi yetu katika kuwaenzi watawala wetu. Imam AS aliwaambia: Haya ni mambo ambayo maamiri wenu hawakufaidika nayo na nyinyi wenyewe mnajitia bure kwenye dhiki hapa duniani na mtakutwa na masaibu huko Akhera. Ni hasara kubwa iliyoje kujiingiza kwenye mashaka ambayo mwisho wake ni adhabu na ni manufaa na faida kubwa illiyoje kuwa na utulivu wa moyo ambao utamsalimisha mja na adhabu ya Allah!
Huko nyuma, ilikuwa ni kawaida kwa watu wa nchi au jiji kuwasujudia wakuu na masultani na ilikuwa ni ishara ya kujidhalilisha kabisa mbele ya maamiri, mabwana wafalme na masultani. Sasa wakati Imam Ali AS alipokuwa safariki kuelekea Sham na jeshi lake, watu wa miji ya njiani walikuwa wanatoka nje kulipokea jeshi la Kiislamu. Walitoka kumkaribisha kwa heshima zote Amirul Muminin na askari wake. Watu wa al Anbar (kaskazini mwa Iraq ya leo) nao pia walijumuika na watu wengine kujitokeza kulikaribisha jeshi la Kiislamu na Amirul Muuminina Ali AS. Wakati Imam na jeshi lake walipoingia kwenye mji wa al Anbar, watu wa mji huo walishuka kwenye vyenye vipando vyao na wakaanza kukimbia kwa miguu mbele ya msafara wa Imam na jeshi lake. Kitendo hicho kwa hakika kilikuwa kibaya na kilikumbusha ule ule unyonge, udhalili na unyanyasaji uliokuwa unafanywa na watawala wa kiimla dhidi ya wananchi. Imam Ali AS alipoona madhari hiyo ambayo ilikuwa mbali na hadhi na heshima ya mwanadamu, aliwauliza watu hao akisema: Ni nini hiki mnachofanya? Baadhi yao walijitetea kwa kusema: Tunawaheshimu mno watawala wetu na namna hivi ndivyo tunavyofanya muda wote kuonesha hisia zetu kwao. Imam ambaye suala la kujipendekeza na kujidhalilisha kwake halikuwa na nafasi yoyote na na serikali yake haikuwa ya watu wanaojitweza na kuwatwaza wengine aliikemea vikali tabia na mila hiyo ya kijahilia na kutoa sababu tatu za ubaya wa tabia na mila hiyo akisema:
Kwanza, watawala wanapofanyiwa kitu kama hicho hawapati manufaa yoyote, bali hupelekea wapande kiburi na hatimaye wapoteze utu na hisia zao za kibinadamu.
Pili ni kwamba mashaka na mzigo mkubwa huwaangukia watu wengi na wakati mwingine watu dhaifu wanaweza kudharauliwa na yakaachwa kufanywa mambo ya maana, zikatumika fedha na mali nyingi za taifa kwa ajili ya kujipendekeza kwa watawala.
Tatu, tabia hiyo ovu inahesabiwa kuwa ni chanzo cha kupata matatizo katika maisha ya baada ya kifo, kwa sababu inakuwa ni aina fulani ya ushirikina na kumpandisha kiongozi daraja ya Mungu.
Lakini iwapo watu na wananchi watatosheka na heshima za kawaida na zinazoruhusiwa mbele ya viongozi wao, watawala na viongozi wote hawataathiriwa na kiburi na majivuno, na watu hawatoingia kwenye udhalili wa kujiona duni na wanyonge au watu wa daraja za chini mbele ya watu wengine na badala yake watamuweka kila mtu katika daraja yake na watapata fursa ya kuelewa kwamba anayepasa mtu kujidhalilisha mbele yake, ni Allah Muumba tu.
Kumepokewa hadithi nyingine ambayo inasema: Siku moja Amirul-Muuminina Ali bin Abi Talib AS aliwajia maswahaba zake akiwa juu ya kipando. Kikundi cha watu kilianza kutembea kwa miguu kumfuata nyuma yake. Imam aliwatazama na kuwaambia: Je, kuna kazi yoyote mnahitaji nikufanyieni? Wakasema: Hapana, Yaa aAmiral-Muminin, lakini tungependa kutembea pamoja nawe. Imam aliwaambia: “Rudini, kwa sababu kutembea kwa miguu karibu na mtu aliyeko juu ya kipando kunasababisha ufisadi (yaani kupanda kiburi na kujitukuza) aliyeko juu ya kipando na unyonge na udhalili kwa anayetembea kwa miguu.
Tab’an inabidi ifahamike hapa kwamba, hii haina maana watu wasiwaheshimu wazee na viongozi wao, bali maana yake ni kwamba heshima wanayowaonesha wafalme na viongozi wao isiwe sababu yao wao kujidhalilisha na kuingia kwenye tabu na matatizo. Heshima yao isiwe chanzo cha kupanda kiburi watu wakubwa na kudunishwa watu wadogo. Ni wajibu wa kila mtu kulinda heshima, utu na hadhi ya mwanadamu mwingine, katika hali yoyote ile.