Feb 28, 2024 05:26 UTC
  • Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu 5

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili , Sauti ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Kipindi cha juma hili kinajadili suala la Waislamu kukombola ardhi ya Palestina na mji wa Beitul Muqaddas, karibuni.

Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba ardhi ya Palestina ina umuhimu mkubwa na maalumu kwa Umma wa Kiislamu kutokana na ukweli kwamba ndicho Kibla cha kwanza cha Waislamu na mahali alipotokea Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad (saw) kupaa kwenda mbinguni. Suala jingine linaloimarisha uhusiano wa kiroho, kihisia na kiimani wa Waislamu na Palestina, Quds na Msikiti wa al-Aqsa, ni kwamba Aya nyingi za Qur'ani Tukufu zilizoteremshwa kwa Mtume mpendwa wa Uislamu (saw) na hadithi pamoja na visa vingi vinavyozungumzia Mitume, wakiwemo Manabii Ibrahim, Yaaqub, Lut, Zakaria, Yahya, Dawoud, Suleiman na Isa (as), vyote vilitimia katika ardhi ya Palestina na suala hilo mbali na matukio ya Qibla, Miraaji na Aya za Qur'ani zinazozungumzia utukufu na umuhimu wa ardhi ya Palestina,  linatilia nguvu uhusiano wa kiroho, kihisia na kiimani wa Waislamu na maeneo hayo matakatifu ya Palestina, Quds na Aqsa. Kwa hivyo lilikuwa jambo la kawaida kabisa kwamba sambamba na kuenea dini ya Uislamu, Waislamu walivutiwa haraka na ardhi ya Sham na Palestina na kuwashawishi watu wa ardhi hiyo waitikie Uislamu na kupinga uvamizi wa Warumi.

Kuhusiana na suala hilo hata kama vita vya Mu'tah (The Battle of Mu'tah) ambavyo vilipiganwa mwaka wa nane Hijiria (629 AD) kwa ajili ya kutekwa maeneo ya Shamaat na Palestina havikuwa na matokeo yoyote maalum kwa Waislamu, lakini katika mwaka wa 9 Hijiria (630 AD), na katika Vita vya Tabuk ((The Expedition of Tabuk) waliweza kuteka eneo la Tabuk lililokuwa karibu na ardhi ya Sham na katika kuimarisha zaidi nafasi yao, wakateka maeneo mengine kama vile eneo la Dumat al-Jandal, ambapo watu wa maeneo hayo walikubaliana na Waislamu kuwalipa jizya mkabala wa kudhaminiwa usalama wao.

Eneo la Vita vya Tabuk

 

Katika muendelezo huo na baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw) mwaka 11 Hijiria 632 Miladia Jeshi la Kiislamu likiongozwa na Usama bin Zaid lilifanikiwa kuimarisha utukufu na nguvu ya Uislamu katika mipaka ya pamoja na Sham. Katika miezi na miaka iliyofuata, jeshi hilo lilifanikiwa kushinda vita vingi katika eneo hilo ambapo liliteka miji kwa mslahi ya Waislamu. Hali hiyo iliendelea hadi pale Waislamu walipofanya mashambulizi ya kuteka Sham na Palestina ambapo waliwashambulia Warumi waliokuwa wakidhibiti eneo hilo kutokea pande kadhaa. Wakiwa Palestina, Waislamu walifanikiwa kuwashinda Warumi katika eneo la kusini mwa Ramleh. Lakini vita vikali na muhimu zaidi vilivyopiganwa kati ya pande mbili kwa ajili ya kuliteka eneo la Shamaat (lililojumuisha Palestin, Jordan, Lebanon na Syria) kutoka katika udhibiti wa Warumi ni vile vya Yarmuk (The Battle of the Yarmuk). Vita hivyo vilipiganwa kando ya mto wenye jina hilo (Yarmuk) mnamo mwaka 636 Miladia. Hivyo ndivyo vilikuwa vita vikubwa zaidi kwa lengo la kudhibiti eneo hilo. Vita hivyo viliashiria kushindwa kwa pili kukubwa kwa ufalme wa Roma kutoka kwa Waislamu katika ardhi ya Syria, jambo ambalo lilikata mikono yake katika ardhi za Shamaat na kwa ujumla katika eneo zima la Asia na hivyo kuwawezesha Waislamu kuizingira Beitul Muqaddas.

Eneo ambalo vita vya Yarmuk vilipiganwa, kaskazini mwa Jordan, na hivyo kuwa chanzo kikuu cha Waislamu kukomboa Beitul Muqaddas na miji mingine ya Sham

 

Waislamu waliteka mji mmoja baada ya mwingine hatua kwa hatua hadi walipofika Quds (Beitul Muqaddas) mwaka wa 16 Hijiria (637 Milaadia). Kwa kuzingatia kuzingirwa Beitul Muqaddas na Jeshi la Kiislamu, wakazi wa mji huo walimwandikia barua kamanda wa jeshi hilo wakimwambia kwamba walikuwa tayari kusalimu amri na kukabidhi funguo za mji huo kwa sharti kwamba funguo hizo zikabidhiwe khalifa wa Waislamu, yaani Omar bin al-Khattab. Omar ambaye alikuwa katika eneo hilo kwa ajili ya kufuatilia masuala ya makamanda na viongozi wa jeshi hilo, alikubali sharti hilo na mkataba wa amani ukatiwa saini hapo hapo. Katika mkataba huo wa amani, Omar aliwadhaminia amani na usalama wakazi wa mji huo ikiwa ni pamoja na mali na maneo yao ya ibada na kwa mujibu wa matakwa ya wakazi hao, hakuna Yahudi yeyote aliyeruhusiwa kubakia Beitul Muqaddas na katika upande wa pili Wakristo waliokuwa wakiishi Quds wakakubali kulipa jizya kwa Waislamu. Kwa utaratibu huo, mwaka 17 Hijiria (mwishoni mwa mwaka 637) mji wa Beitul Muqaddas ukakabidhiwa kwa Waislamu kwa amani na bila umwagaji damu ambapo dola la Kiislamu lilitawala mji huo kwa miaka 400 mfululizo hadi wakati wa vita vya kwanza vya Msalaba mwaka 1099. Katika kipindi hicho chote Wakristo na wakazi wengine wa Beitul Muqaddas waliishi kwa amani na utulivu kamili chini ya utawala wa ukhalifa wa Kiislamu.

Kutekwa Beitul Muqaddas na Waislamu mwaka 16 Hijiria

William Fitzgerald, Mwandishi wa Uingereza anasema kuhusu kutekwa mji huo na Waislamu kwamba: "Katika historia yote ya vita vya utekaji ardhi, hadi kabla ya kutekwa Quds, hakukuwahi kushuhudiwa watu walioshindwa kwenye vita wakihisi utulivu, ukarimu na amani kutoka kwa watu walioshinda vita kama ilivyofanyika kutoka kwa Waislamu walioteka Quds. Waislamu waliita Quds kwa majina ya "Bait al-Haram" na "Bait al-Maqdis." Waliswali katika Msikiti wa al-Aqsa, ambapo Bilal bin Riyah (Bilal wa Abyssinia (Ethiopia)) aliadhini kwa mara ya kwanza huko Quds baada ya kifo cha Mtume (saw) na Waislamu wakaanza kujenga msikiti mdogo na wa kawaida kabisa mahala hapo.

Katika muendelezo wa utawala wa Kiislamu juu ya Palestina, Bani Umayya (41-132 AH/661-750 AD) walizingatia sana suala la Palestina na Quds, kiasi kwamba Abd al-Malik bin Marwan, Khalifa wa tano wa Bani Umayya, alijenga msikiti mkubwa karibu na Msikiti wa Al-Aqsa, ambao ulijulikana kama Masjidu al-Swakhra. Msikiti huo ulijengwa juu ya jabali ambalo Mtume alisimama juu yake muda mfupi kabla ya kupaa mbinguni. Mwanawe, Waleed bin Abdul Malik, alijenga upya Msikiti wa Al-Aqsa, na kuanzia wakati huo na kuendelea, eneo lililo karibu na msikiti huo likajulikana kwa jina la "Haram Sharif." Hisham Abdul Malik pia alilipa kipaumbele maalum eneo la Jericho ambapo alijenga huko msikiti wa kifahari. Pia, Suleiman bin Abdul Malik, Khalifa wa saba wa Bani Umayya, aliasisi mji wa Ramlah huko Palestina na akaufanya kuwa makao makuu yake, ambapo alizingatia sana Quds na Msikiti wa al-Aqswa. Wakati alipojitenga Abdullah bin Zubair huko Makka na Madina wakati wa utawala wa Abd al-Malik bin Marwan na kushindwa Waislamu wa Syria kwenda kutekeleza ibada ya Hija huko Makka, alifanya ibada ya Quds na swala katika Msikiti wa Al-Aqsa kuwa mbadala wa Hija.

Msikiti wa Kubbatu Swakhra (Mwamba)

Katika kipindi cha utawala wa makhalifa wa Bani Abbas (750-1258 AD), licha ya kuhamishiwa kituo cha ukhalifa katika ulimwengu wa Kiislamu mjini Baghdad, lakini Bani Abbas walitilia maanani na kulipa umuhimu mkubwa suala la Palestina na Quds, ambapo Abu Jafar Mansour anayejulikana kama Mansour Dawaniqi, Khalifa wa pili wa Bani Abbas, (utawala: 136 - 158 Hijiria), alitembelea Quds mara mbili na akaamuru kujengwa upya majengo yaliyokuwa yamebomolewa kufuatia uharibifu uliosababishwa na tetemeko kubwa la ardhi lililokumba eneo hilo. Al-Mahdi, Khalifa wa tatu wa Bani Abbas, pia aliutembelea mji huo (Quds). Pia, al-Ma’mun, Khalifa wa saba wa Bani Abbas, alifanya ukarabati na marekebisho makubwa katika Kuba la Msikiti wa Mwamba, ambapo baada ya hapo, wanazuoni wengi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu pia waliishi katika mji wa Quds, miongoni mwao, akiwemo Abu Hamid Ghazali anayejulikana kama Imam Muhammad, ambaye alikuwa mmoja wa wanafalsafa wakubwa wa karne ya 5 Hijria. Baada ya hapo watawala wa ukoo wa Fatimiyyun (909 hadi 1171 Milaadia) waliziondoa Misri na Palestina katika utawala wa Bani Abbas, lakini uadui kati yao na masultani wa Seljuk (1037 hadi 1210 Miladia) uliongezeka na hilo likaibua utengano na kudhoofika majeshi ya Waislamu. Hivyo, Vita vya Msalaba vilipoanza mwaka 1095 Miladia, na Wapiganaji wa Msalaba wakahujumu maeneo ya Palestina na Mashariki, waliweza kuteka na kukalia kwa mabavu miji kadhaa ya Palestina ukiwemo mji wa Ramla. Mji wa Quds nao ilizingirwa na washambuliaji hao kwa muda wa mwezi mmoja na baada ya mapigano yaliyodumu kwa muda mrefu, hatimaye Julai 15, 1099 Milaadia vikosi vya Fatimiyyun vilivyokuwa katika mji huo vikajisalimisha kwa wapiganaji wa Vita vya Msalaba ambao waliuteka mji huo na kuwaua kwa umati watu wa mji huo mtakatifu. Kwa mujibu wa marejeo ya kihistoria, Waislamu wapatao sabini elfu waliuawa na wamavizi hao bila huruma.