Feb 28, 2024 06:49 UTC
  • Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu 8

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya makala hii ya Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu. Katika kipindi cha leo tutazungumzia matukio ya ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu tangu wakati wa himaya ya Uingereza katika ardhi hiyo hadi wakati wa kutokea Intifadha ya taifa la Palestina dhidi ya wavamizi wa utawala wa Kizayuni.

Bila shaka mngali mnakumbuka ni kwa nini tunazungumzia vipindi hivi vinavyojadili ardhi ya Palestina na umuhimu wake kwa ulimwengu wa Kiislamu. Ni kutokana na umuhimu huo ndipo katika vipindi vilivyopita tukajadili kwa kina historia ya ardhi hii na wakazi wake wa mwanzo, pamoja na kuingia na kutoka makabila mbalimbali katika ardhi hiyo. Katika kipindi kilichopita, tulijadili namna Azimio la Balfour lilivyotangazwa na watu waliohusika katika kuliandaa, azimio ambalo kwa namna fulani liliweka msingi wa zaidi ya karne moja ya migogoro na mizozo katika ardhi ya Palestina. Azimio hilo liliwaahidi Mayahudi kwamba Uingereza ingewaunga mkono katika jitihada zao za kujipatia makao ya kitaifa. Pia tulisema kwamba mnamo Aprili 25, 1920, Baraza Kuu la Washirika (lililojumuisha wakuu wa nchi na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tano kuu za Washirika, Uingereza, Ufaransa, Marekani Italia, na Japan) kwenye Mkutano wa San Remo huko Italia, lilikabidhi usimamizi wa ardhi ya Palestina kwa serikali ya Uingereza ambapo tarehe 22 Julai 1922, suala hilo liliwasilishwa kwa serikali ya Uingereza na Baraza la Jumuiya ya Mataifa kupitia hati yenye vifungu 28.

Kwa kukabidhiwa usimamizi na uendeshaji mambo wa Palestina kwa serikali ya Uingereza, serikali hiyo ilimteua mtu aliyeitwa Herbert Louis Samuel, ambaye alitoka katika familia maarufu ya Mayahudi wa Uingereza, kuwa Kamishna Mkuu wa kwanza wa Palestina. Kufuatia uteuzi huo, uhamiaji wa Mayahudi kwenda Palestina uliwezeshwa ambapo walihimizwa na kushawishiwa kununua ardhi za Waarabu wa Palestina. Kabla ya hapo, Lloyd George, Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo, alisema baada ya kutangazwa rasmi Azimio la Balfour kwamba Mayahudi walitakiwa kufika kwa wingi huko Palestina ili kuunda jumuiya ya manufaa ya pamoja. Kwa hivyo, uhamiaji wa kila aina wa Mayahudi kuelekea ardhi za Palestina ulihimizwa na kuungwa mkono kwa kila namna na serikali ya Uingereza. Jambo hilo liliendelea hata katika miaka yote ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Kwa kadiri kwamba hata kama idadi ya Mayahudi waliokuwa Palestina kati ya mwaka 1905 hadi 1914 ilikuwa elfu chache tu, lakini wakati wa kuanza vita hadi mwisho wake, Mayahudi wapatao elfu 20 walikuwa wamepewa makazi huko Palestina. Baada ya Herbert Samuel kuteuliwa na Uingereza kuwa Kamishna Mkuu huko Palestina, kufikia mwaka 1923, idadi ya Mayahudi ilikuwa imeongezeka hadi kufikia watu 35,000.

Herbert Louis Samuel

Kuhimizwa Mayahudi kuhamia Palestina na kutekelezwa masharti ya Azimio la Balfour kulipingwa mara moja na Waarabu, na ghasia zikawa zimeanza tangu kutangazwa Azimio la Balfour. Kuhusiana na hilo, kongamano la kwanza la wanaharakati wa Palestina na makundi ya mapambano lilifanyika Beitul Muqaddas (Jerusalem) kuanzia Januari 29 hadi Februari 10, 1919, ambapo azimio la mwisho la kongamano hilo lilijumuisha maombi ya kuzuia uhamiaji, kuvunjwa ahadi za Balfour, kukomeshwa serikali ya usimamizi (himaya) na kuunganishwa Palestina na Syria, ikizingatiwa kuwa Palestina pia ilikuwa sehemu ya Syria inayoitwa "Syria ya Kusini". Kufuatia malalamiko hayo, Februari 1920, kulifanyika maandamano makubwa huko Quds, ambapo zaidi ya raia 40,000 wa Kiarabu wa Palestina walishiriki, na baada ya hapo ujumbe wa waandamanaji hao ulikutana na Kansela wa Quds na Gavana wa Uingereza na kuwasilisha malalamiko yao kuhusu uhamiaji wa Mayahudi, Azimio la Balfour na Uzayuni, malalamiko ambayo hayakupewa umuhimu wowote na Kamishna Mkuu wa Palestina wala serikali ya Uingereza.

Kwa hivyo, mnamo Machi 8, 1920, maandamano mengine yalifanyika Quds ambapo waandamanaji walipiga nara dhidi ya Uzayuni, uhamiaji wa Mayahudi na kuunga mkono kujitawala, uhuru na umoja wa Waarabu. Lakini moja ya maandamano makubwa zaidi ya Waarabu wanaoishi Palestina yalifanyika tarehe 4 hadi 8 Aprili 1920 katika mji wa Quds (Jerusalem), sehemu ambako sherehe za Nabii Musa (as) zilikuwa zinafanyika. Maandamano hayo, yaligeuka na kuwa machafuko na malalamiko ya kitaifa ya Wapalestina dhidi ya Uzayuni na ukoloni wa Uingereza, ambapo watu kadhaa waliuawa na kujeruhiwa. Mnamo 1921, kulitokea ghasia dhidi ya Mayahudi ambapo Waarabu wa nchi nyingine walitangaza wazi upinzani wao dhidi ya mpango wa Kizayuni uliolenga kuigeuza Palestina kuwa makazi ya Mayahudi wa Kizayuni.

Maandamano ya kupinga Uzayuni kwenye lango la Damascus, Machi 8, 1920

Kutokea maandamano na upinzani huo, ambao sasa ulienea hadi nje ya mipaka ya ardhi ya Palestina, uliilazimu serikali ya Uingereza kuchukua hatua, ambapo ilijaribu kidhahiri kuwadhibiti Mayahudi na kuwafanya wakubalike mbele ya Waarabu. Hii ni kwa sababu kama isingefanya hivyo, Wazayuni kamwe wasingeweza kukubalika kuishi Palestina, na wangeendelea kutengwa milele na Waarabu wa Palestina, na kutazamwa kama wageni. Kwa kuzingatia hilo, serikali ya Uingereza, kupitia waraka wa Churchill uliochapishwa tarehe 3 Juni, 1922, ilitangaza sera zake mpya kuhusu Palestina.

Waraka huo ulidai kwamba lengo halikuwa kuijaza Palestina na Mayahudi, kama vile Uingereza ilivyo kwa Waingereza, bali nia ilikuwa ni kuunda jumuiya ya Kiyahudi ambayo ingejivuniwa na Mayahudi wa rangi na mahdhebu zote kutokana na ustawi wake. Pia ilidaiwa kuwa idadi ya Mayahudi waliokuwa wanahamia Palestina, ingedhibitiwa na kupunguzwa kutokana na kuwa ardhi hiyo haikuwa na uwezo wa kutosha wa kiuchumi wa kukidhi mahitaji ya wahamiaji wapya. Pia ilielezwa kuwa nia haikuwa "kuwang'oa Waarabu, lugha na utamaduni wao huko Palestina ili kuwaweka chini ya mamlaka ya watu wengine."

Hata kama kwa tamko hilo, serikali ya Uingereza ilijaribu kuzima hasira za Waarabu wa Palestina, lakini pia iliitaka jumuiya ya Kizayuni kuelewa kwamba kama ilitaka kutambua rasmi usimamizi wa Waingereza juu ya Palestina, ilitakuwa kukubali na kupitisha tafsiri hiyo kuhusu Azimio la Balfour. Kwa mujibu wa tamko la Churchill, makazi ya kitaifa ya Mayahudi na tamko la Balfour hayakuwa na maana ya Kuyahudishwa kikamilifu Palestina, na wala Uingereza haikuwa na nia kama hiyo. Pia, lugha, utamaduni na jamii ya Waarabu haikutakiwa kuwa chini ya udhibiti wa Mayahudi.

Picha kuhusu mapambano ya Buraq

Ingawa tamko la Churchill, lilionekana kidhahiri kuwa ni kulegeza msimamo na makali ya Azimio la Balfour na matakwa ya Wazayuni, lakini kivitendo halikuwa na tofauti yoyote na Azimio la Balfour wala matakwa ya serikali ya Uingereza kwa niaba ya Wazayuni. Kila mwaka idadi ya Wazayuni na Mayahudi waliokuwa wakihamia katika ardhi ya Palestina ilongezeka. Matakwa ya Wazayuni yalikuwa yakiongezeka kila siku, hivi kwamba mwishoni mwa Machi 1929, walianza kudai ''haki'' zao waziwazi! Walianza kupiga nara za eti kutetea haki zao katika Haram ya Quds na Ukuta wa Buraq, na kusisitiza ulazima wa kujengwa upya Hekalu la Nabii Suleiman badala ya msikiti wa Al-Aqsa.

Hata kuhani mmoja wa Romania alisema katika barua aliyomwandikia Haj Amin al-Husseini, Mufti Mkuu wa Palestina, kwamba alipasa kukabidhi Msikiti wa Al-Aqsa kwa Mayahudi ili waweze kufanyia humo sherehe zao za kidini! Hali hiyo iliwakasirisha tena Waarabu na kuchochea maandamano dhidi ya Wazayuni ambayo yalianza tena mwaka 1928, na katika majira ya joto ya 1929, mgogoro wa umwagaji damu, ambao baadaye ulijulikana kwa jina la "Mapambano ya Buraq", ulizuka kati ya Waarabu wa Palestina na Wazayuni. Kutokana na ufyatuaji risasi mkali uliofanywa na Wazayuni na wanajeshi wa Uingereza, Wapalestina walipata hasara kubwa katika machafuko hayo wakiwemo mashahidi 351, majeruhi 150 na mamia ya wafungwa. Ni baada ya machafuko hayo ndipo mapambano na maandamano ya wananchi wa Palestina yalipoanza kupangwa kiutaratibu zaidi na ni kwa mapambano ya watu kama Sheikh Ezzeddin Qassam, ndipo ukaanzishwa muhimili wa muqawama na harakati za mapambano za taifa la Palestina dhidi ya ukoloni na Uzayunim na huo ukawa mwanzo wa awamu ndefu ya harakati ya kitaifa ya watu wa Palestina ya kuendesha muqawama dhidi ya uvamizi na ukaliaji mabavu wa Israel katika ardhi za Wapalestina.