Feb 28, 2024 06:22 UTC
  • Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu 6

Assalaam Alaykum wpenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Katika kipindi cha leo tutajadili kwa kifupi historia ya ardhi ya Palestina tokea karne za kati hadi wakati wa kuasisiwa harakati ya Mayahudi katika karne ya 19 Miladia, karibuni.

 

Vita vya Msalaba vilipoanza mwaka 1095 Miladia, na wapiganaji wa msalaba wakahujumu maeneo ya Palestina na Mashariki waliweza kuteka na kukalia kwa mabavu miji kadhaa ya Palestina ukiwemo mji wa Ramla. Mji wa Quds nao ulizingirwa na washambuliaji hao kwa muda wa mwezi mmoja na baada ya mapigano yaliyodumu kwa muda mrefu, hatimaye Julai 15, 1099 Milaadia vikosi vya Fatimiyyun vilivyokuwa katika mji huo vikajisalimisha kwa wapiganaji wa Vita vya Msalaba ambao waliuteka mji huo na kuwaua kwa umati wakazi wa mji huo mtakatifu. Wapigani wa Msalaba ambao walitoka katika makabila na mataifa tofauti ya Ulaya wakati wa kuuteka mji wa Quds walisahau kabisa hoja na dalili za kidini walizodai kuzifuatilia katika mashambulio yao dhidi ya mji huo mtakatifu. Walipoteka na kuikalia kwa mabavu miji tofauti waliua kikatili wakazi wa miji hiyo ambapo inasemekana waliua kinyama Waislamu wapatao elfu 70 katika hujuma hiyo. Jambo la kushangaza ni kuwa wapiganaji hao walijivunia mauaji hayo ya umati walipoyazungumzia katika vitabu na nyaraka zao za kihistoria. Katika kipindi hicho, mji wa Beitul Muqaddas ulitangazwa rasmi kuwa mji wa Wakristo ambapo watu wasiokuwa Wakristo na hasa Waislamu hawakuruhusiwa kuishi huko. Kufuatia hatua hiyo misikiti ilibadilishwa kuwa makanisa au majengo yasiyokuwa ya shughuli za kidini. Wapiganaji wa msalaba waliondoa nembo ya hilali iliyokuwa imetundikwa juu ya Msikiti wa Qubbatu Swakhra na kuweka mahala pake msalaba na hivyo kuuvunjia msikiti huo heshima uliyokuwa nayo. Walipora kila kitu kilichokuwa humo na kuzuia kusomwa adhana katika msikiti huo kwa karibu karne moja.

Katika nyaraka na vitabu vya karne za kati, wapiganaji wa Msalaba wanajivunia mauaji ya umati yaliyofanywa dhidi ya wakazi wa mji wa Quds wakati wa kutekwa mji huo

 

Wapiganaji wa Msalaba walitekeleza jinai kubwa katika mji wa Quds. Kasisi kwa jina Raymond of Aguilers ambaye mwenyewe alishuhudia mauaji hayo ya umati anaandika hivi: "Mambo ya kushangaza yanaweza kuonekana kutoka kila upande. Kundi la Waislamu lilikatwa vichwa... kundi jingine liliuawa kwa mishale au kulazimishwa kujirusha chini kutoka kwenye minara. Wengine waliteswa kwa siku kadhaa na kisha kuchomwa moto. Kulikuwa na rundo la vichwa, mikono na miguu ya wafu mitaani." Godfrey wa Bouillon, kamanda wa wapiganaji wa msalaba ambaye baadaye alikuwa mfalme wa Palestina, aliandika katika ripoti yake kwa Papa kuwa: "Ikiwa unataka kujua nini kiliwapata maadui walioanguka mikononi mwetu huko Jerusalem, fahamu tu kwamba watu katika Hekalu la Suleiman walikuwa wakikimbia kwenye bahari ya damu ya Waislamu, na damu ilifika kwenye magoti ya farasi." Waandishi wengine pia wameandika kwa kina kuhusu tukio hilo na kueleza jinsi wanawake walivyokuwa wakidungwa visu hadi kufa, watoto wachanga waliokuwa wakinyonyeshwa wakivutwa kwa miguu kutoka vifuani mwa mama zao na kutupwa kwenye kuta, au wakivunjwa shingo zao kwa kutupwa kwenye nguzo. Mayahudi waliookoka walikusanywa katika sinagogi na kuchomwa moto wakiwa hai, na wakawaua Waislamu sabini elfu waliobakia mjini humo."

Vita vya Msalaba vilidumu kwa takriban karne mbili ambapo Wakristo walitawala Palestina kwa miaka 90. Wakati fulani, Salah al-Din Ayubi katika mwaka wa 583 Hijiria/1187 Milaadia, na kupitia vita vya siku kadhaa, aliweza kuuteka mji wa Hattin ulioko kaskazini mwa Palestina, baada ya kukusanya jeshi kubwa la Waislamu na kuwashinda wapiganaji wa Msalaba. Baada ya muda fulani Waislamu walifanikiwa kuteka miji mingine kadhaa na kuizingira Quds kwa muda mrefu, na hatimaye kuuteka kikamilifu mji huo baada ya kuuzingira kwa miezi kadhaa. Lakini baada ya kifo cha Sultan Salahuddin mwaka 589 Hijiria/1193 Milaadia na kuzikwa karibu na Msikiti wa Bani Umayya, watoto wake walihitilafiana, ambapo Wapiganaji wa Msalaba walitumia fursa hiyo kuishambulia tena Palestina. Waliteka na kukalia kwa mabavu baadhi ya maeneo yake na mwishowe kuuteka kikamilifu mji wa Quds. Baada ya hapo, Salah Ayoub, mfalme wa wakati huo wa Misri alifanikiwa kukomboa Quds na Gaza baada ya kupita miaka kumi na tano. Lakini kufukuzwa kabisa wapiganaji hao wa msalaba kutoka katika nchi ya Palestina kulifanyika takriban karne mbili baada ya vita vya kwanza vya msalaba.

Wakati wa kujisalimisha Guy Lusignian (Mfalme wa Jerusalem-Quds) kwa Salahdin baada ya kumalizika Vita vya Hattin

Katika kipindi cha kufukuzwa wapiganaji wa msalaba kutoka ardhi ya Palestina, wakazi na watu wa magharibi mwa Palestina walishirikiana kwa karibu na askari wa jeshi la Kiislamu ambapo walikuwa wakiwaelekeza na kuwaongozwa kwenye njia na maficho ya wapiganaji hao. William wa Tyre askofu na mwandishi wa historia wa karne za kati anasema kuhusu suala hilo: "Wao waliwafundisha na kuwaambia maadui wetu, kwa ibara nyingine Waislamu, namna ya kutumaliza kwa sababu walikuwa na taarifa za kutosha kutuhusu."

Wapenzi wasikilizaji ni muhimu mtambue kwamba baada ya vita vya saba vya msalaba na baada ya kuuawa mfalme wa mwisho wa ukoo wa Ayyubi, Mamaleek ambao ni silsila ya Kiislamu ya makamanda wa Kituruki waliingia madarakani nchini Misri. Waliwashinda wapiganaji wa msalaba na kutawala kwa karibu karne tatu katika miji mingi ya Palestina ukiwemo mji wa Beitul Muqaddas. Hicho kikawa kipindi kingine cha kunawiri Quds na Palestina kwa ujumla. Wafalme wa Mamaleek walizingatia sana Quds na Palestina, ambapo walipunguza malipo ya kodi  na kutoa zawadi ya nakala tofauti za Qur'ani zenye thamani kwa misikiti tofauti ya Quds. Walijenga pia misikiti mipya, shule, vituo, njia za chini kwa chini na vituo vya kupumzikia misafara kwa ajili ya watu masikini. Mamaleek walipigana vita na kulishinda jeshi la Wamongoli ambao walikuwa wameanzisha hujuma ya kutaka kuuteka mji wa Beitul Muqaddas na wakati huo huo kuyamaliza kabisa mabaki ya wapiganaji wa msalaba ambao walikuwa wamejificha katika mji wa Akka.

Sambamba na kipindi hicho katika karne ya 13 Hijiria, silsila ya masultani wa Kiothmania walianzisha mapigano makubwa ya kuteka ardhi (Osman Ghazi) katika maeneo ya karibu na Uturuki ya leo. Baada ya kifo cha Othman na warithi kadhaa wa kiti chake, ufalme ukaangukia mikononi mwa Sultan Muhammad. Mwaka 1453 Miladia, sawa na 875 Hijiria, Sultan Muhammad, aliuteka mji wa Constantinople, ambacho kilikuwa kituo kikuu cha nguvu ya wapiganaji wa msalaba na mji mkuu wa Roma ya Mashariki. Kwa hatua hiyo aliweza kuwafukuza wapiganaji wa msalaba hadi kwenye malango ya Ulaya. Baada ya tukio na ushindi huo alipewa jina la Muhammad Faatih, yaani mshindi.

Kuwasili Sultan Muhammad Fatih mjini Constantinople

Kutekwa mji wa Constantinople ilikuwa hatua muhimu ya mabadiliko katika historia ya Ulaya, ambapo maarifa na ustaarabu wa Kiislamu uliingia barani Ulaya baada ya kushindwa wapiganaji wa Vita vya Msalaba, na hilo likaashiria mwisho wa Zama (karne) za Kati na mwanzo wa mabadiliko makubwa ya Renaissance (enzi za mwamko). Baada ya hapo Constantinople ukawa mji mkuu wa Ufalme wa Othmaniyya. Waottoman waliteka nchi nyingi za Ulaya ya Mashariki kama vile Bulgaria, Yugoslavia, Romania na sehemu za Ugiriki. Utawala wao ulienea katika ulimwengu wa Kiarabu, ambapo nchi kama vile Iraq, Sham, Hijaz, Misri, Sudan na sehemu kubwa ya Magharibi ya Kiarabu zilikuwa chini ya Ufalme wa Ottoman. Hatimaye wakaikomoa Plaestina mnamo Agosti 1516 Miladia.

Masultani wa Othmaniyya walitawala ardhi yote ya Palestina, pamoja na Quds Sharif, kwa zaidi ya karne nne. Kuenea kwa mamlaka ya serikali hiyo na kupanuka utawala wa Uthmaniyya katika maeneo ya Asia, Afrika na sehemu za Ulaya kulizitia wasiwasi mkubwa nchi za Ulaya kama vile Uingereza, Ufaransa, Russia ya Kitatsari na Italia, ambapo zilikuwa na hofu kubwa ya kutawaliwa na utawala wa Othmaniyya. Walitaka kuzuia kwa kila njia kupanuka kwa mamlaka hiyo na kutafuta njia za kuiangamiza. Serikali ambayo ilifanya juhudi kubwa zaidi za kutaka kuingamiza serikali ya Othmaniyya ilikuwa serikali ya Uingereza. Kwa upande mwingine, mfalme na viongozi wa serikali ya Othmaniyya katika maeneo waliyotawala walikuwa wakali na wasio na huruma, na hiyo ikawa sababu ya kuwafanya waasi. Kuhusiana na hilo, mwishoni mwa karne ya 19, uasi mwingi ulitokea Palestina, hasa mjini Quds, ambapo serikali ya Uingereza, ambayo siasa zake hadi wakati huo zilijengeka katika msingi wa kulinda ardhi zote za Ufalme wa Othmaniyya barani Asia, iligeuza ghafla siasa hizo na kuanza kukabiliana na serikali ya Othmaniyya.

Serikali ya Uingereza ilifanya njama nyingi kwa ajili ya kudumisha udhibiti wake katika Mfereji wa Suez, kuimarisha ushawishi wake nchini India, kusambaratisha serikali ya Othmaniyya na kuwahadaa Waarabu kuwa ingewasaidia, kwa kuwachochea waasi serikali ya Othmaniyya. Ikiwa ni katika njama hizo ilimchochea Hussein, Amir wa Makka, ambaye alikuwa mwakilishi wa Uthmaniyyah huko Hijaz na aliyekuwa na uchu mkubwa wa madaraka, kujitenga na utawala wa Uthmaniyya. Katika mazingira hayo, baadhi ya Mayahudi walitoa fikra ya kuundwa taifa la Mayahudi, ambayo ilichangamkiwa na kuungwa mkono haraka na serikali ya Uingereza. Hivyo, harakati za dola la Mayahudi zikaibuka Ulaya ya Kati mnamo 1880.