Feb 28, 2024 06:34 UTC
  • Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu 7

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tukiwa bado tunaendelea kujadili kwa kifupi historia ya Palestina, leo tutazungumzia nafasi ya Uingereza katika kubuniwa utawala haramu wa Israel katika ardhi za Wapalestina kupitia Azimio la Balfour, karibuni.

Katika vipindi vilivyopita tulizungumzia historia ya Palestina tangu mwanzo hadi wakati wa kudhibitiwa ardhi hiyo na ufalme wa Othmaniyya. Tulisema kwamba wakati ambao Uingereza ilikuwa inatekeleza njama mbalimbali za kutenga maeneo na ardhi zilizokuwa chini ya utawala wa Dola la Othmaniyya na kuziondoa kwenye udhibiti wa utawala huo, Mayahudi nao walikuwa wakijishughulisha na fikra ya kubuni dola lao, fikra ambayo ilishajiishwa na kuungwa mkono mara moja na serikali ya kikoloni ya Uingereza. Kwa msingi huo Harakati ya Kaumu ya Mayahudi ikaasisiwa mwaka 1880 katika Ulaya ya Kati.

Harakati hiyo ya Kaumu ya Mayahudi ilibuniwa kwa msaada wa nchi kama Uingereza kwa lengo la kuunda dola la Kiyahudi. Katika miaka ya 1882 hadi 1897, harakati hiyo ilifanya juhudi za kuwahamisha Mayahudi kutoka pembe zote za dunia na kuwahamishia Palestina, lakini haikufanikiwa sana katika uwanja huo. Ni katika kipindi hicho ndipo mwandishi mmoja wa habari aliyeitwa Theodor Herzl (1860-1904) ambaye wengi wanasema hakujua lugha ya Kiibrania wala kufahamu lolote kuhusu historia ya Mayahudi, akachapisha kitabu huko Ufaransa mwaka 1895 kwa jina la "Nchi ya Mayahudi" akiwaomba Mayahudi kufanya juhudi za kubuni "dola la Mayahudi". Herzl alikuwa ripota wa gazeti la "New Free" lililochapishwa huko Budapest Hungary, na akisafiri mara nyingi kati ya mji huo na Paris nchini Ufaransa. Mnamo 1897, alichapisha gazeti la "The World", ambacho kilikuwa chombo rasmi cha kueneza fikra za Kizayuni. Mwaka huo huo, na akiwa na viongozi wengine wa Kizayuni, walikusanyika katika mji wa Basel Uswizi na kuunda "Umoja wa Kizayuni Ulimwenguni", ambao mamlaka yake kuu lilikuwa "Kongamano la Uzayuni." Herzl aliandika hivi kuhusu matokeo ya mkutano huo: "Ikiwa tunataka kufupisha matokeo ya Kongamano la Basel katika sentensi moja, ambalo sitawahi kufichua maamuzi yake, lazima niseme kwamba nilianzisha taifa la Kiyahudi katika Kongamano la Basel."

Theodor Herzl

Tangu mwanzo wa kuasisiwa kwake, Kongamano la Uzayuni lilianza kutekeleza siasa za hadaa na udanganyifu wa makusudi ambapo wakati wa kufanyika kikao cha kwanza cha Wazayuni wa Kiyahudi, lilijiepusha kwa makusudi kutumia neno "nchi", bali lilitumia neno "kituo" kwa ajili ya kuwahamishia Mayahudi wote wa dunia katika nchi ya Palestina. Hii ni kwa sababu kama neno "dola au nchi" lingetumika kwa ajili ya Mayahudi, bila shaka suala hilo lingekabiliwa na malalamiko na upinzani mkubwa wa wananchi wa Palestina na mataifa mengine. Pamoja na hayo ni wazi kuwa makusudio ya kongamano hilo la Wazayuni na waungaji mkono wao kuhusiana na neno "kituo" tangu mwanzo ilikuwa ardhi ya Palestina jambo ambalo lilithibitishwa kivitendo na matukio yaliyofuata.

Kufuatia Vita vya Kwanza vya Dunia na uungaji mkono wa ufalme wa Othmaniyya kwa Ujerumani ambapo upande huo na washirika wake walishindwa kwenye vita hivyo, mwaka 1916 mkataba unaojulikana kama "Sykes-Picot Agreement" ulitiwa saini kati ya serikali ya Uingereza na Ufaransa kwa ajili ya kugawana ardhi zilizokuwa chini ya utawala wa Othamaniyya barani Asia. Makubaliano hayo yalitiwa saini kati ya Sir Mark Sykes aliyewakilisha Uingereza na Georges Picot aliyewakilisha serikali ya Ufaransa.

Wakati huo huo, serikali ya Uingereza ilikubaliana na Sharif Hussein, ambaye alikuwa mtawala wa Hijaz kwa niaba ya serikali ya Othmaniyya, kwamba aasi ufalme huo na kuwa Uingereza ingemuunga mkono (yaani Sharif Hussein) na kuwasaidia Waarabu katika uasi wao dhidi ya utawala wa Othmaniyya. Pia, Mkataba wa Sykes Picot uliarifishwa kwa serikali ya Russia ya Kitatsari ambayo iliukubali baada ya kupata fursa na maslahi kadhaa kutoka upande huo. Mnamo Aprili 16, 1916, makubaliano yalitiwa saini kati ya serikali tatu za Uingereza, Ufaransa, na Russia, kwa jina "Mkataba wa Sazonov" ambao ulikamilisha Mkataba wa Sykes-Picot, na mwishowe, ardhi ya serikali ya Othmaniyya ikagawanywa kati ya serikali hizo tatu. Sehemu ya ardhi ya serikali ya Uingereza katika mkataba huo ilikuwa mikoa ya kusini mwa Iraq, mji wa Baghdad na bandari ya Haifa na Akka huko Palestina.

Inafaa kufahamu kwamba moja ya matatizo na changamoto zilizojitokeza katika kugawanywa ardhi zilizochukuliwa kutoka Dola la Othmaniyya ni ardhi ya Palestina. Wote Sykes na Picot walitaka kuichukua ardhi hiyo kwa ajili ya nchi zao. Baada ya majadiliano ya kina, hatimaye iliamuliwa kwamba Uingereza ichukue bandari za Akka (Acre) na Haifa huko Palestina na kuwa maeneo mengine ya ardhi ya Palestina yasimamiwe kimataifa kwa namna fulani. Bila ya pande zote kuwa na taswira maalum kuhusu mchakato wa usimamizi wa kimataifa akilini, ziliamua kuzungumzia suala hilo baada ya kumalizika vita.

Katika Makubaliano ya Sykes-Picot, walipokuwa wakichukua maamuzi kuhusu Palestina, kimsingi hawakuwa wakizungumzia Mayahudi kupewa makazi huko Palestina. Hii ni katika hali ambayo kwa muda mrefu na katika kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia mazungumzo ya kisiasa ya kina yalikuwa yakifanyika kati ya viongozi wa Kiyahudi na wa Uingereza, yakisisitiza juu ya uungaji mkono wa serikali ya Uingereza kwa malengo ya Mayahudi duniani yakiwemo ya kuanzishwa dola la Mayahudi katika ardhi ya Wapalestina. Kufuatia mabadiliko yaliyotokea katika serikali ya Uingereza, ambapo Lloyd George aliingia madarakani, hamu na tamaa ya Uingereza katika ardhi ya Palestina iliongezeka. Katika upande wa pili, kuingia madarakani Clemenceau huko Ufaransa mnamo 1917, ambaye alipinga vikali sera za ukoloni wa Ufaransa, kuliifanya nchi hiyo kutokuwa na hamu tena ya kujilimbikizia ardhi za kikoloni katika Mashariki ya Kati, hivyo Ufaransa ikawa imepoteza hamu yake ya awali kuhusiana na ardhi ya Palestina.

Wakati huo, yaani mwaka 1917, viongozi wa Uzayuni ambao waliishawishi Marekani kushiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia kwa manufaa ya mrengo uliokuwa dhidi ya Wajerumani, na kutokana na ahadi walizokuwa wamepewa na Waingereza, waliona hiyo kuwa fursa nzuri kwa ajili ya kushinikiza matakwa yao ya kuundwa dola la Kiyahudi katika ardhi zilizoporwa za Wapalestina. Kwa msingi huo waliomba uungaji mkono rasmi wa serikali ya Uingereza kupitia Arthur James Balfour (1848-1930) aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali hiyo. Balfour, alipendekeza Jumuiya ya Wazayuni iunde kamati iliyojumuisha waandishi na wanasiasa wa Kizayuni na ikapewa jukumu la kuandaa rasimu iliyopelekea kutangazwa Azimio la Balfour na kutangazwa uungaji mkono rasmi wa serikali ya Uingereza kwa ajili ya kuundwa dola la Kiyahudi. Mayahudi wa Marekani pia walihusishwa katika jambo hilo ambapo hatimaye mnamo Oktoba 1917, maandishi ya mwisho yalipitishwa na serikali ya Uingereza, na mnamo Novemba 2 mwaka huo huo, azimio hilo likatangazwa rasmi kwa Lionel Walter Rothschild, mmoja wa mabepari na viongozi wa Uzayuni.

Katika tangazo hilo ambayo ilikuwa hatua ya kwanza ya kivitendo ya kuundwa utawala wa Kizayuni huko Palestina, Uingereza ilitangaza uungaji mkono wake kwa suala la kuanzishwa serikali huru ya Kiyahudi huko Palestina, na kuwa ingefanya kila juhudi zilizohitajika ili kuanzishwa utawala wa Kiyahudi huko Palestina.

Balfour (kushoto) na Rothschild (kulia)

 

Waingereza wamefanya juhudi kubwa kupitia Azimio la Balfour kujaribu kuonyesha kuwa wamebuni dola haramu la Wazayuni katika ardhi za Palestina kutokana na huruma yao kwa Mayahudi na kujaribu kufidia kile kinachodaiwa kuwa dhulma ya kihistoria waliyofanyiwa, lakini ukweli wa mambo ni kwamba tangu wakati huo baadhi ya wanasiasa wa Uingereza waliona kuwa kubuniwa dola la Wazayuni huko Palestina karibu na Mfereji wa Suez, ambao ulikuwa mshipa muhimu wa kiuchumi kwa ufalme wa Uingereza, kungekuwa na faida za kistratijia kwa ufalme huo. Kwa hivyo, tunapasa kusema kwamba sababu kuu ya kupitishwa Azimio la Balfour na Uingereza ilikuwa ni kulinda masilahi ya Waingereza kupitia kuundwa dola la Kizayuni katikati mwa Mashariki ya Kati. Kwa hakika maslahi ya Uingereza na ulimwengu wa Magharibi kwa ujumla katika eneo la Mashariki ya Kati yalilazimu kuundwa serikali ya Wazayuni ili iwe mshirika wao wa kistratijia katika eneo hili muhimu.

Kwa msingi huo, London ilitangaza Azimio la Balfour la kuanzishwa dola la Kizayuni ambalo lingedhamini maslahi ya Uingereza na ulimwengu wa Magharibi katika Mashariki ya Kati. Hivyo Uingereza ilichangia pakubwa katika kubuniwa kwa dola hilo ili kudhamini maslahi yake ya kikoloni, hasa katika Mfereji wa Suez na katika njia kuu ya bahari kuelekea India.

Azimio la Balfour lilikamilishwa mnamo Agosti 11, 1919 katika Kongamano la Amani la Nchi Waitifaki huko Paris na kisha kutumwa katika Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza mnamo Septemba 19, ambapo ilisajiliwa kama hati rasmi katika kuainisha sera za kigeni za Uingereza. Azimio hilo Iillipitishwa na waitifaki na hatimaye na Jumuiya ya Mataifa mnamo Julai 24, 1922, ambayo ilikabidhi rasmi usimamizi wa Palestina kwa Uingereza. Kuasisiwa 'Kituo cha Kitaifa cha Kiyahudi' huko Palestina kulijumuishwa katika jukumu la usimamizi huo, ambapo Azimio la Balfour lilitajwa katika karibu kila neno la majukumu ya usimamizi huo. Pamoja na kwamba kutangazwa Azimio la Balfour hakukuwatatiza wengi, hasa katika kwa ulimwengu wa Kiislamu, ambao walidhani kwamba kungelisahaulika baada ya muda, lakini historia imethibitisha kinyume na hilo, ambapo sasa azimio hilo linachukuliwa kuwa moja ya nyaraka muhimu na zenye utata wa kimataifa, ambazo zimewasababisha wanadamu machungu makubwa, hasa katika ulimwengu wa Kiislamu.