Feb 28, 2024 07:27 UTC
  • Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu 9

Assalaama Aeykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu. Kufuatia mapambano ya Izzuddin Qassam, mapambano ya Kiislamu ya Palestina yalipata msukumo, uhai na azma mpya kwa akili ya kupambana na uchokozi na uvamizi wa Wazayuni.

Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba mapambano ya "Buraq" ambayo yalianzishwa na watu wa Palestina mwishoni mwa Machi 1929 kwa lengo la kupinga uvamizi wa Waingereza na hatua za mtawala wa kijeshi wa Uingereza katika kuharakisha mwenendo wa kuhamia Mayahudi katika ardhi ya Palestina yalikuwa na nafasi muhimu katika mwamko na mapambano ya taifa la Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni. Mapambano hayo  yalifanyika kwa ajili ya kukabiliana na madai ya Wazayuni kuhusu Msikiti wa Al-Aqswa na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) pamoja na Qur'ani Tukufu, na yalianzia katika mji wa Quds na kuenea haraka katika ardhi yote ya Palestina. Lau isingekuwa ujasiri na mwamko huo wa watu wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni, labda leo Msikiti wa Al-Aqsa ungekuwa umeharibiwa na sehemu yake kujengwa hekalu bandia la Mayahudi katika ardhi hiyo ambayo ni Kibla cha kwanza cha Waislamu.

Kwa upande mwingine, kama isingekuwa ni usaliti wa watala wa Kiarabu kama vile Sharif Hussein na ukoo wa Al Saud, pengine leo hii kusingekuwepo athari yoyote ya Uzayuni katika ardhi hiyo. Tutajadili katika kipindi hiki matukio ya muongo wa 1930 ya ardhi ya Palestina hadi mwanzo wa Vita vya Pili vya Dunia ili kujifunza zaidi kuhusu historia ya ardhi ya Palestina katika muongo wa nne wa karne ya 20.

Baada ya "Mapambano ya Buraq", taifa la Palestina lilizidi kudhamiria kupambana na uvamizi wa Wazayuni, na ni katika kipindi hicho ndipo mtu kwa jina "Izzuddin Qassam" akafungua njia mpya katika mapambano ya wananchi wa Palestina, jambo lililomfanya atambuliwe kuwa mwasisi wa Harakati ya Kiislamu ya Palestina. Qassam ambaye alizaliwa mwaka 1882 katika kijiji cha milimani karibu na mji wa Latakia nchini Syria, alihitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar nchini Misri katika taaluma ya masomo ya kidini. Akiwa huko huko Misri, alipata kuujua vizuri ukoloni wa Waingereza na udhibiti wake juu ya taifa na rasilimali za kitaifa za nchi hiyo, ambapo aliwaza sana kuhusu suala la kupambana na vikosi vya wakoloni na hatimaye kujiunga na harakati ya kitaifa ya upinzani dhidi ya Waingereza.

Wakati wanajeshi wa Ufaransa walipoingia Syria mwaka 1920, Qassam alianzisha mapambano dhidi ya wavamizi hao kwenye pwani ya kaskazini mwa Syria. Wafaransa walijaribu kumzuia Qassam asiendelee na pambano kwa kumpa mapendekezo ya hadaa na udanganyifu kama vile kumpendekezea vyeo na nafasi za juu nchini, lakini hilo halikumhadaa bali aliyatupilia mbali mapendekezo hayo yote. Sisitizo la Qassam la kuendelea na mapambano hatimaye liliipelekea mahakama ya kijeshi ya Ufaransa huko Latakia kutoa hukumu ya kifo dhidi yake na baadhi ya washirika wake. Ili kukwepa mateso na adhabu hiyo ya Wafaransa Qassam alikimbilia Damascus na kisha kwenda Palestina.

Qassam alianza kufundisha katika shule ya Kiislamu ya Haifa na kuwafahamisha wanafunzi wake kuhusu mustakabali wa ardhi yao katika mazingira ya kukaliwa kwa mabavu na maadui. Alikuwa akifanya mihadhara misikitini baina ya swala tano na kutumia fursa hiyo kuwatayarisha Waislamu kwa ajili ya vita. Vitisho vya mashambulizi ya vikosi vya Uingereza vilipoongezeka, Qassam alianzisha "Jumuiya ya Vijana wa Kiislamu."

Alikuwa akiwasiliana na viongozi wa miji mbali mbali ya Palestina, na kwa njia hiyo, aliweza kuwakomboa na kuwavutia vijana wengi kwenye jumuiya yake ya Jihadi, vijana ambao walikuwa wameachiliwa huru kutokana na minyororo ya upotofu na kutojiamini kulikosababishwa na hali ngumu ya kiuchumi na kisiasa ya wakati huo.

Izzuddin Qassam

Kufuatia mapambano ya Buraq, mateso na ukatili wa jeshi la Waingereza dhidi ya Waarabu wa Palestina uliongezeka hivi kwamba mnamo 1930, Waingereza waliwanyonga Wapalestina watatu kwa majina Atta el Zeer, Mohammed Khalil Jamjoum na Fouad Hijazi katika jela ya Akka (Acre) kwa tuhuma za kuchochea ghasia dhidi ya Waingereza na Wazayuni. Kabla ya hapo, waliwahukumu kifungo cha jela takriban Waislamu 800 kwa tuhuma hizo hizo. Katika upande wa pili, katika miaka ya 1933 na 1934, mchakato wa Wazayuni kuhamia Israel, kuunda makundi ya kigaidi na vilevile kupora ardhi za Wapalestina uliongezeka kwa kasi kubwa. Wimbi kubwa la Mayahudi na Wazayuni kuhamia katika ardhi ya Palestina kulifanyika sambamba na makundi ya kigaidi ya Wazayuni kupewa silaha kwa ajili ya kufukuza Waislamu na Waarabu wa Palestina katika ardhi zao na kuwaua kigaidi wale waliokataa kuondoka. Lengo la Wazayuni lilikuwa kuwafanya Waarabu wa Palestina wakimbie na kuwacha mashamba na nyumba zao na kuwaachia Mayahudi wapya waliohamia Palestina. Jambo hilo lilimlazimu Izzuddin Qassam aanzishe operesheni za kijeshi dhidi ya makundi ya kigaidi ya Kizayuni ambayo yalilenga roho na mali za wananchi wa Palestina, hata kabla ya kupata suhula na wapiganaji wa kutosha.

Atta Al-Zeer, Mohammad Khalil Jamjom na Fouad Hijazi

Moyo wa Jihadi na mafundisho ya Kiislamu ya Sheikh Izzudin Qassam yaliwezesha mapambano ya Kiislamu kuenea katika maeneo yote ya Palestina. Hivyo miongozo na amri za Qassam, zilianzisha mlolongo wa operesheni za kijeshi dhidi ya magenge ya kigaidi ya Kizayuni na doria za kijeshi za Uingereza. Sheikh Izzuddin Qassam aliamini kuwa, utamaduni na ustaarabu wa nchi za Magharibi ulikuwa umevamia ulimwengu wa Kiislamu na kuwatenganisha wasomi na wanafikra wa Kiislamu wenye mielekeo ya Kimagharibi na maumbile asili na salama ya mwanadamu. Wanafikra na vibaraka ambao walikuwa wamezama kwenye utamaduni na ustaarabu wa Magharibi na hivyo kutokuwa tena na uwezo wa kukabiliana na hujuma ya kiutamaduni ya Magharibi na majeshi ya Magharibi. Watu hao walikuwa wameathiriwa pakubwa na masuala ya kimaada. Kwa msingi huo, wengi wa wanafunzi na wafuasi wa Qassam walikuwa watu wa kawaida kabisa na makundi ya wakulima, wafanyakazi wa kazi za mikono, wafanyakazi wa Shirika la Reli la Haifa na wafanyakazi wa migodi ya mawe.

Mapambano ya Izzuddin Qassam, yaliyoanza mwaka 1930, yaliendelea hadi 1935 ambapo aliuawa shahidi mnamo tarehe 20 Novemba mwaka huo huo. Moyo imara wa Qassam na hatua zake za kishujaa ziliwavutia Waislamu wengi wa Palestina na kuwafanya wapate ujasiri wa kupambana na uvamizi wa Wazayuni, kiasi kwamba wakati wa mazishi yake, idadi kubwa ya viongozi na wazee kutoka pembe zote za Palestina walifikwa kwa wingi Haifa kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho na kushiriki katika mazishi ya shujaa huyo wa Palestina. Mazishi hayo yalidumu kwa masaa mengi na yakageuka kuwa maandamano makubwa dhidi ya wavamizi wa Kizayuni na wakoloni wa Uingereza, maandamano ambayo yaliendelea kwa miezi na miaka mingi iliyofuata. Kwa njia hiyo, “Mapambano ya Izzuddin Qassam” yakawa mwanzo wa mapambano makubwa zaidi ambayo yalienea Palestina nzima kwa miezi kadhaa baada ya kuuawa kwake shahidi.

Kaburi la Sheikh Izzuddin Qassam karibu na Haifa

Nuru ya taa iliyowashwa na Qassam na marafiki zake ilienea na kuonekana katika pembe zote za Palestina katika nusu ya pili ya muongo wa 1930. Mawimbi ya mapinduzi ambayo yaliondoa kabisa fursa ya kufanyika mapatano ya aina yoyote kati ya viongozi vibaraka wa kisiasa wa Kipalestina na serikali kuu ya Uingereza. Baada ya kukabiliwa na hali hiyo serikali ya Uingereza ilijaribu kuwatumia wafalme na watawala vibaraka wa Kiarabu ili kukandamiza harakati za mapinduzi ya Wapalestina. Sambamba na hatua hiyo, mnamo Novemba 1936, Uingereza ilituma kundi lililojulikana kama Kamati ya Kifalme kutoka London kwenda Palestina ili kuchunguza sababu za maandamano na malalamiko ya Wapalestina. Kamati hiyo iliwasilisha maoni na mapendekezo yake kwa serikali ya Uingereza, ambapo ilidaiwa kuwa Wapalestina walikuwa wameamua kuigawa Palestina kuwa nchi mbili za Kiyahudi na Kiarabu.

Ripoti hiyo bandia na ya upendeleo ya Kamati ya Kifalme ya Uingereza ilichochea wimbi la malalamiko na upinzani katika maeneo kadhaa ya Palestina. Maandamano hayo, ambayo yalijulikana kama "Mapinduzi Makuu ya Palestina", yaliendelea bila kusita hadi mwishoni mwa mwaka 1939. Katika hali hiyo vikosi vamizi vya serikali ya Uingereza vilianza kusaka na kuwafuatilia viongozi wa mapinduzi ili eti kuzima moto wa mapambano ya wananchi wa Palestina.

Serikali ya Uingereza ilifanya juhudi za kuzima  mapambano hayo na wakati huo huo kutumia mbinu za ujanja kuwahadaa Wapalestina kwa sababu ilitambua kwamba kama isingemaliza mgogoro huo, ingeipoteza kabisa Palestina. Kwa hiyo, Mei 17, 1939, iliwasilisha mpango kupitia "Kitabu Cheupe", ambao ulionekana kidhahiri kuwa ushindi wa kisiasa kwa Wapalestina, lakini kwa hakika ulikuwa na madhara kwao. Serikali ya Uingereza ilidai katika mpango huo kwamba haikuwa na nia yoyote ya kuunda dola la Kiyahudi huko Palestina bali ilikuwa ikifuatilia kuundwa dola huru la Palestina lenye nguvu, la Waarabu na Mayahudi. Aidha, ilitangaza uamuzi wake wa kuunda taifa la Palestina ndani ya miaka kumi na kudai ingesimamisha mwenendo wa Mayahudi kuhamia Palestina isipokuwa kama Waarabu wenyewe wangetaka uendelee. Suala jingine ambalo Uingereza ililitilia mkazo kidhahiri katika kitabu hicho ni kupigwa marufuku Mayahudi kuuziwa ardhi katika katika baadhi ya maeneo ya Palestina, huku uuzaji huo ukiruhhusiwa katika maeneo mengine kwa masharti.

Mpango huo ulipingwa vikali na Wazayuni ambao walianza kujikurubishwa kwa Marekani ili kuendeleza malengo yao ya kichokozi dhidi ya Wapalestina. Viongozi wa Palestina pia walitilia shaka waraka huo wa Uingereza kwa sababu Uingereza haikutilia maanani utekelezaji wake. Kwa hiyo, wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipokaribia, mgogoro wa Palestina ulikuwa bado unaendelea.