Hadithi ya Uongofu (45)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia suala la Swilat Rahm yaani kuunga udugu na tulielezea umuhimu wa jambo hili kijamii na kidini na pia athari zake kimaada na kimaanawi.
Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 45 ya mfululizo huu kitazungumzia Udugu wa Kiislamu. Kuweni namI hadi mwisho wa kipindi hiki kusikiliza niliyokuandalieni kwa wiki hii.
Dini Tukufu ya Kiislamu inawahutubu Waislamu wote kwa anuani ya watu wa familia moja yenye umoja na kwamba, wao ni kaka na dada. Imekuja katika hadithi kwamba, Waislamu ni mithili ya jengo moja imara ambapo kila sehemu moja ya jengo hilio inamtegemea mwenzake. Mafundisho haya ya Kiislamu yaliyotambulishwa na Qur'ani ni moja ya njia bora na athirifu kabisa za kulinda na kuimarisha jamii ya kidini. Hii ni kutokana na kuwa, chini ya kivuli cha udugu wa kidini masuala kama huba, umoja na ushirikiano huongezeka na kwa muktadha huo jamii hupata kinga na kuepukana na mambo mengi kama upotofu wa kiroho, kijamii na kidini.
Kwa hakika Uislamu ni dini ya huba, upendo na rehma ambayo kupitia nara ya "Al-Muuminuun Ikhwah" Waumini ni Ndugu" umetoa adia na zawadi kwa Umma wa Kiislamu. Hivyo basi, kadiri imani ya watu itakavyokuwa kubwa na imara, ndivyo ambayo, mshikamano na urafiki baina ya wanadini hao unavyokuwa imara na madhubuti zaidi baina yao.
Imam Ja'afar Swadiq AS amenukuliwa akisema kuwa: Uhakika wa imani ya mja hautakamilika mpaka pale atakapompenda ndugu yake. Aidha amesema katika hadithi nyingine kwamba: Miongoni mwa ishara za kushikamana na dini mtu ni kumpenda ndugu yake katika dini.
Kuweko mapenzi, huba na upendo baina ya ndugu katika dini hupelekea kuchipua amani na utulivu katika jamii ya Kiislamu. Kwa hakika mfungano wa kimoyo wa wanadamu unarejea katika njia ya usalama na ustawi wa kila mtu.
Imam Ja'afar Swadiq AS amesema kuwa, kila kitu kina wenzo na suhula ambayo kupitia kwayo raha na utulivu hupatikana; na muumini hupata utulivu kwa kuweko (karibu yake) ndugu yake katika imani. Cha kuvutia zaidi ni pale Imam Ali bin Abi Twalib AS anapowataka Waislamu washindane katika kufanya huba na upendo. Anasema, ndugu asiwe imara zaidi kushinda wewe katika urafiki.
Kimsingi ni kuwa, ndugu katika imani ni mithili ya ngome na husuni au msaidizi ambaye mbali na vita au suluhu humkinga mtu na kuwa kizuizi chake katika nyuga mbalimbali.
Mmoja wa wapokezi wa hadithi kutoka kwa Imam Ja'afar Swadiq AS yaani bin Bakhtari anasimulia kwamba:
Nilikuwa kwa Imam Swadiq AS mara akaingia bwana mmoja. Imam akaniuliza: unapanda Bwana huyu? Nikwambia, ndio. Akasema, na kwa nini usimpenda hali ya kuwa ni ndugu yako na mshirika wako katika dini na vilevile msaidizi wako dhidi ya adui yako….?
Kwa hakika udugu wa kidini ni moja ya njia bora na mwafaka kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano baina ya watu katika jamii. Ni kwa msingi huo ndio maana Bwana Mtume SAW alitekeleza mpango wa kuunga udugu katika mji wa Madina. Kigezo kilichotumiwa na Mtume SAW za kumuainishia ndugu yake kila Mwislamu kilikuwa ni mlinganano wa sifa na ukaribu wa daraja ya Imani yao. Mtu SAW alikuwa akiwachagua watu wanaolingana na wanaokamilishana na kuwaunganisha udugu baina yao. Mwandishi Ibn Sa'ad anaeleza katika kitabu chake cha Tabaqal al-Kubra kwamba, katika zoezi la kuunga udugu baina ya Waislamu Mtume SAW alimuunganisha udugu Abubakar na Omar, Twalha na Zubeir, Othman bin Affan na Abdul-Rahman bin Awf, Abu Dhar al-Ghifaari na Miqdad na kisha yeye Mtume SAW akaunga udugu na Ali bin Abi Twalib AS.
Dini ya Kiislamu ikiwa na nara na kauli mbiu ya "Waumini ni Ndugu" imepandisha kiwango cha mahusiano ya Waislamu na kukifikisha katika daraja ya urafiki ambacho ni huba baina ya ndugu wawili.
Ni kwa msingi huo muhimu wa Kiislamu basi, ndio maana Waislamu kwa kaumu yoyote watakayokuwa nayo, kabila lolote watakalokuwa nalo, lugha yoyote watakayokuwa wakiizungumza na umri wowote watakaokuwa nao, wao ni ndugu na ni sawa na kiwiliwili kimoja.
Imam Swadiq AS anasema, Muumini ni ndugu yake ni Muumini. Wao ni sawa na kiwiliwili kimoja, kiungo kimoja kikiumia basi viungo vingine navyo huhisi maumivu...
Kwa hakika Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, ushirikiano huyabadilisha maslahi tofauti na yanayokinzana kuwa ya pamoja na hali hiyo huunganisha pamoja nyoyo za watu.
Katika jamii ya Kiislamu, watu ni sawa na viungo vya mwili mmoja, ambapo kiungo kimoja kikipata maumivu, basi viungo vingine navyo huwa pamoja na kiungo hicho katika maumivu.
Miongoni mwa matunda na natija ya udugu wa kiimani katika jamii ya Kiislamu ni Mwislamu kumueleza ndugu yake Mwislamu mapungufu na aibu alizonazo na kila mmoja kumkumbusha mwenzake. Ukumbusho huu huandaa mazingira ya ukamilifu wa mwanadamu. Imepokewa hadithi katika kitabu cha Nahaj al-Fasah kutoka kwa Bwana Mtume SAW ya kwamba amesema: Muumini ni kioo cha ndugu yake Muumini.
Katika maisha ya kawaida mtu anapojitazama katika kioo lengo huwa ni kuangalia kama amekaa vizuri na hujaribu kuondoa kasoro zilizopo kabla ya kutoka nje au mbele za watu. Kwa muktadha huo basi, Muumini ni kioo cha ndugu yake Muumini yaani hana budi kumueleza ndugu yake mapungufu alionayo na kumnasihi kwa njia bora na nzuri ili ajirekebishe. Kufanya hivi ndiko kutimia kwa udugu wa Kiislamu. Ndio maana inaelezwa kuwa, ndugu yako bora kabisa ni yule ambaye anakueleza kuhusiana na aibu na mapungufu ulionayo. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Imam Ja’afar Swadiq AS anasema kuwa: Ndugu yangu ninayempenda zaidi ni yule ambaye ananizawadia aibu zangu.
Jukumu la Mwislamu kwa ndugu yake Mwislamu yaani kwa mtu ambaye wanashirikiana katika imani, ni jambo ambalo limebainishwa katika hadithi mbalimbali. Mtume SAW anasema, Mwislamu ni ndugu wa Mwislamu mwenziwe; hamdhulumu katu, haachi kumsaidia na wala hamsalimishi kwa adui yake.
Aidha Imam Swadiq AS amenukuliwa akisema kuwa, Mwislamu ni ndugu wa Mwislamu, na ni sawa na jicho, kioo na muongozo kwake, katu hamsaliti, hamhadai, hamdhulumu, hamwambii uongo na wala hamsengenyi. Katika kueneza utamaduni wa udugu wa Kiislamu na kila mmoja kusitiri aibu za mwenzake, Mtume SAW alikuwa akilihesabu jambo hili kuwa ni jukumu la kidini.
Mtukufu huyo amenukuliwa akisema:
Kila ambaye ataficha na kufunika aibu ya ndugu yake Mwislamu na kutomuumbua, basi Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama atazisitiri aibu zake.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Tutakutana tena wiki ijayo panapo majaaliwa yake Mola Muweza.
Ninakuageni nikimuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa wanaochunguza na kulifanyia kazi suala la udugu wa Kiislamu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…