Hadithi ya Uongofu (46)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni tena kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Juma lililopita tulizungumzia udugu wa Kiislamu na kubainisha umuhimu wa jambo hilo pamoja na athari zake katika jamii.
Moja ya sifa za kimaadili zenye thamani na umuhimu mkubwa ni utunzaji wa amana. Amana katika lugha ina maana ya ukweli na uaminifu na mkabala wake ni hiana na usaliti. Katika istilahi utunzaji amana maana yake ni mtu kukitunza kitu au mali aliyopatiwa na kumrejeshea mwenywe pindi anapohitajia. Katika kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 46 ya mfululizo huu tutazungumzia maudhui hii na kukunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na utunzaji wa amana. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki, kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo.
Katika maisha yetu ya kawaida, wakati linapozungumziwa suala la utunzaji wa amana akthari ya watu fikra ya akili yao huelekea katika suala la amana katika fedha na mali. Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa maana na fasili ya kilugha ya utunzaji wa amana pamoja na aya na hadithi zinazozungumzia suala hilo, utunzaji amana una maana pana na tofauti tofauti. Mambo aliyopatiwa mwanadamu na Mwenyezi Mungu kama maarifa, vipaji katika masuala mbalimbali na huba katika moyo wake ni moja ya vielelezo na mifano ya wazi ya amana.
Imam Ja’afar Swadiq AS amenukuliwa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir AS kwamba: Amana za Mwenyezi Mungu ni amri na makatazo yake, na amana za waja wa Mwenyezi Mungu ni amana za fedha na mali wanazopatiana. Kiuhakika kwa mtazamo wa Uislamu mbali na amana kujumuisha masuala ya fedha na mali, inajumuisha pia masuala ya kimaanawi kama vile: taklifu na majukumu ya kidini, kumtii Mwenyezi Mungu, kumuabudu, kuheshimu na kuchunga haki za watu na vitu vingine ambavyo viko katika fremu na majukumu ya Mwislamu.
Inanukuliwa katika hadithi kwamba, wakati wa Swala ulipokuwa ukiwadia, sura ya Imam Ali bin Abi Twalib AS ilikuwa ikibadilika rangi na kwamba, mtukufu huyu hali yake ilikuwa ikibadilika na kuwa isiyo ya kawaida na alikuwa akisema: Wakati wa Swala umewadia, wakati wa kutekeleza amana ya Mwenyezi Mungu. Tunapochunguza aya za Qur’ani Tukufu tunapata natija hii kwamba, amana kubwa kabisa ya Mwenyezi Mungu ni taklifu, majukumu na masuuliya ambayo Allah ameyakweka katika mamlaka na uwezo wa mwanadamu. Aya ya 72 ya Surat al-Ah’zab inasema kuwa:
Kwa hakika Sisi tulikadimisha amana kwa mbingu na ardhi na milima; na vyote hivyo vikakataa kuichukua na vikaogopa. Lakini mwanaadamu akaichukua.
Moja ya vielelezo vya amana ni imani. Kwani kila mtu ambaye anadai kushikamana na imani, kiuhakika amekubali kubeba mzigo wa amana na kuyafanyia kazi mafundisho ya Mwenyezi Mungu na hivyo anataka kufikisha amana hiyo kwa mwenyewe.
Umuhimu wa utunzaji amana ni mkubwa kiasi kwamba, inaelezwa katika hadithi kuwa, mtu ambaye si mtunza amani basi hana imani. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: Mtu ambaye hana sifa ya utunzaji amana basi hana imani. Imam Ja’afar Swadiq AS yeye anaona kuwa, utunzaji amana ni kigezo bora kabisa cha kupima shakhsia ya kimaanawi ya mtu.
Anasema: Kipimo cha kuwa Mwislamu na kipimo cha imani ya mtu ni ukweli na utunzaji amana wake na sio kuswali, kurukuu na kusujudu kwake, tazameni je ni mkweli na mtunza amana, na je anapokabidhiwa amana huirejesha kwa mwenyewe aua la?
Mtume SAW anaihesabu elimu na ujuzi aliopatiwa mwanadamu kuwa ni miongoni mwa amana za Mwenyezi Mungu. Mbora huyo wa viumbe anasema: Elimu ni amana ya Mwenyezi Mungu katika ardhi yake, na wanazuoni ni watunzaji wa amana hiyo; hivyo basi kila ambaye ataifanyia kazi elimu yake atakuwa ametekeleza haki ya amana na kila ambaye hataifanyia kazi elimu yake, jina lake litaandikwa katika daftari la wasaliti (wafanya hiana).
Miongoni mwa amana nyingine za Mwenyezi Mungu ni roho ya mwanadamu ambaye imepuliziwa na kuwekwa katika ujudi wake. Imam Ali AS anaoina roho kuwa ndio neema ya kwanza yenye thamani kubwa aliyopatiwa mwanadamu na Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo basi roho ya mwanadamu yaani uhai wake ni amana muhimu kabisa miongoni mwa amana za Mwenyezi Mungu ambayo inapaswa kutumiwa katika uwanja wa kumridhisha Mwenyezi Mungu. Endapo mwanadamu ataitumia neema hii yaani roho na uhai wake kwa ujumla katika maasi na mambo machafu, kimsingi mtu huyu atakuwa amefanya hiana katika amana ya Mwenyezi Mungu.
Moja ya mifano ya wazi kabisa ya amana baina ya watu ni vitu na fedha au mali. Wakati mtu anapomuamini mtu fulani na kumpatia fedha au mali yake amuhifadhie, mpokeaji kutokana na kukubali hilo anapaswa kuhifadhi amana hiyo na kumkabidhi mhusika mara tu atakapohitajia.
Tunakiendeleza kipindi chetu cha kile kwa kisa kifuatacho:
Baada ya Bwana Mtume SAW kuukomboa mji wa Makka yaani baada ya tukio la Fat’h Makka alimwita Othman bin Twalha aliyekuwa mtunzaji wa ufunguo wa al-Kaaba na kuchukua ufunguo kutoka kwake ili aweze kuisafisha nyumba ya Mwenyezi Mungu na uwepo wa masanamu. Baada ya kumaliza kazi hiyo, Abbas yaani ami yake Mtume SAW alimtaka Bwana Mtume SAW amkabidhi yeye ufunguo huo.
Katika zama hizo utunzaji wa ufunguo wa al-Kaaba ni jambo lililokuwa na daraja na hadhi ya juu miongoni mwa Waarabu. Hata hivyo Bwana Mtume SAW alimkatalia ombi lake na kuurejesha ufunguo kwa mtu aliyechukua kutoka kwake yaani Othman bin Twalha. Wakati Mtume SAW anaukabidhi ufunguo huo alisoma aya ya 58 katika Surat Nisaai inayosema:
Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe.
Kuhusiana na umuhimu wa utunzaji amana na kumrejeshea mwenyewe kwa wakati, Imam Ali bin Hussein Zainul Abidin AS anasema kuwa:
Hongereni kwa kuwa ni watunza amana, ninaapa kwa Mola ambaye alimteua na kumtuma kwa haki Mtume Muhammad SAW, kama muuaji wa baba yangu yaani Hussein bin Ali atanipatia upanga aliomuulia shahidi nao baba yangu ili nimtunzie kama amana, basi nitaitunza amana hiyo na kumpatia mara tu atakapoihitajia.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo sina budi kukomea hapa nikimuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa watunzaji wazuri wa amana za watu. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh..