Maswali yetu na Majibu ya Thaqalain (128)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.
Kabla ya kuzungumzia aya zinazothibitisha Uimamu wa Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw), tutajibu na kujadili swali ambalo linaulizwa na wengi ambalo linasema, je, ni kwa nini Qur’ani Tukufu haijataja majina ya Maimamu hao kama ilivyotaja bayana jina la Bwana wao Nabii Muhammad al-Mustafa (saw)? Na ni kwa nini ilimuachia Mtume Mtukufu (saw) jukumu la kuwaarifisha Maimu hao kwa Waislamu? Umewadia wakati wa kutafuta kwa pamoja jibu la swali hili muhimu kwenye maandiko matikatifu, karibuni.
***********
Ndugu wasikilizaji tunaporejea hadithi tukufu tunaona kwamba swali hili liliulizwa tokea karne ya pili Hijiria na kujibiwa na Maimamu wenyewe (as), kwa ufasaha na uwazi mkubwa na kwa kutegemea Qur’ani Tukufu. Thiqatul Islam al-Kuleini (MA) amemnukuu katika kitabu chake cha al-Kafi Abu Basir (MA) akisema: Nilimuuliza Aba Abdillah (yaani Imam Swadiq (as)) maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema; Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi.
Akasema (as): iliteremka kumuhusu Ali bin Abi Talib, al-Hassan na al-Hussein (as). Nikamuuliza: Basi ni kwa nini Ali na Ahlul Beit wake hawakutajwa kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu?
Akasema (as): Waambieni: Hakika Mtume aliteremshiwa swala (yaani aya zinazoamrisha swala) na wala Mwenyezi Mungu hakuwatajia tatu wala nne (yaani hakuwaambia ni swala gani iliyo na rakaa tatu na ni gani iliyo na rakaa nne), hadi Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alipowabainishia hilo.
Kisha (as) akasema: Na zilimteremkia Mtume mtukufu (saw) (aya) zinazoamrisha Zaka lakini hazikuzungumzia kiwango kinachapasa kutolewa bali ni Mtume (saw) ndiye alikuwa akiwabainishia viwango hivyo na aliteremsha Hija lakini (Mwenyezi Mungu) hakuwaambia: Fanyeni tawafu mara saba bali ni Mtume (saw) ndiye aliyewafasiria hilo.
*********
Ndugu wasikilizaji na baada ya Imam Swadiq (as) kuwatolea mifano hiyo katika nguzo muhimu zaidi za dini ya Kiislamu ambapo Qur’ani Tukufu ilizifaradhisha kwa Waislamu bila ya kuwafafanulia kiwango na jinsi ya kuzitekeleza bali ilimwachia Mtume (saw) kutekeleza jukumu hilo, baada ya hapo Imam (as) alibainisha mkondo na sunna hiyo ya Qur’ani kuhusiana na Maimamu walio na mamlaka miongoni mwa Waislamu na kusema: Na ikateremka aya ya Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi, ikiwakusudia Ali, al-Hassan na al-Hussein na hapo Mtume (saw) akasema kuhusiana na Ali: Yule ambaye mimi ni Maula (msimamizi wa mambo/Bwana) wake basi na huyu Ali ni Maula wake, na akasema: Ninakuusieni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul Beit Wangu. Ama Kwa hakika nimemuomba Mwenyezi Mungu asivitenganishe vitu viwili hivi hadi atakapovifikisha mbele yangu kwenye Hodhi, na akanikubalia hilo. Na Akasema (saw): Msiwafundishe kwa sababu wao ni wajuzi zaidi kukulikoni nyinyi, na akasema: Hakika wao hawatakutoeni kwenye mlango wa wongofu wala kukuingizeni kwenye mlango wa upotovu.
Kwa hivyo ndugu wasikilizaji, Mtume Mtukufu (saw) alibainisha kwa ufasaha na uwazi mkubwa maana halisi ya aya ya watu walio na mamlaka miongoni mwa Waislamu ili kuwatimizia hoja na hivyo kuwalazimu kuwafuata watukufu hao na wakati huohuo kufupisha njia ya watu ambao wangejitokeza baadaye na kudai kuwa wao ndio waliokusudiwa kwenye aya hiyo. Mtukufu Mtume alilibainisha hilo kwa uwazi mkubwa katika hadithi nyingi ambazo zimepokewa na madhehebu yote ya Waislamu.
Hilo ni mosi, la pilli ni kuwa Qur’ani yenyewe imezithibitisha hadithi hizo za Mtume (saw) katika aya nyingine. Imam Swadiq (as) anasema mwishoni mwa hadithi yake: ‘Kama Mtume (saw) angenyamaza na kutobainisha ni nani waliokusudiwa kwenye Ahlul Beit wake (saw) ukoo wa fulani na fulani ungelidai jambo hili. Lakini Mwenyezi Mungu aliteremsha katika kitabu chake aya inayothibitisha aliyoyasema Mtume (saw) kwa kusema: Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukutakaseni kabisa kabisa. Ali, al-Hassan, al-Hussein na Fatuma (as) walikuwa hapo na Mtume (saw) akawaingiza kwenye shuka, wakiwa kwenye nyumba ya Ummu Salama. Akasema (Mtume): Allahumma hakika kila Mtume ana ahli na uzito na hawa ni ahli na uzito wangu. Ummu Salama akasema: Je, si mimi ni katika ahli zako? Akasema: Wewe uko kwenye kheri lakini hawa ndio Ahlu Beiti na uzito wangu.
***********
Na hivi wapenzi wasikilizaji tunaona kwamba Qur’ani Tukufu imewataja Maimamu wa wongofu kwa njia ya ufasaha na uwazi mkubwa kuliko kuwataja kwa majina, na hilo linatokana na kutaja sifa zao na kusema kuwa ni watukufu ambao Mwenyezi Mungu amewapa isma na kuwaondolea uchafu pamoja na kuwatakasa kabisa kabisa.
Katika hili kuna ishara ya kuvutia kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayoashiria hakika hii kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliamuru watukufu hawa watiiwe na kufuatwa sio kutokana na kuwa ni kizazi cha mpendwa wake al-Mustafa (saw) bali kutokana na kuwa ni watu waliopewa isma yaani kinga ya kutofanya dhambi, waliotakaswa na walio na daraja ya juu ya kumwamini Mwenyezi Mungu.
Al-Imam as-Swadiq (as) anasema mwishoni mwa hadithi hii katika kubainisha aya ya kutakaswa Maimamu kutokana na uchafu kwa kusema: Rijsi (uchafu) ni shaka; Wallahi hatumshuku Mola wetu abadani. Imam (as) anaendeleza hadithi yake hii kwa kuashiria utimilifu wa hoja kupitia ujumbe huu wa Qur’ani na maneno haya ya Mtume yanayokamilisha utambulisho wa makhalifa wa Mtume Mtukufu (saw) kwa kusema: Mtume alipoaga dunia Ali alikuwa mbora zaidi wa watu ambaye Mtume alimuarifisha kwa watu kwa kumsimamisha na kumshika mkono mbele yao. Alipoaga dunia Ali, hakupasa (ali) - na wala hangeweza kufanya hivyo – kumuingiza (mwanawe) Muhammad bin Ali wala Abbas bin Ali wala yeyote katika watoto wake wengine. Hi ni kwa sababu al-Hassan na al-Hussein wangesema: Mwenyezi Mungu aliteremsha Wahyi kutuhusu sisi kama alivyouteremsha kukuhusu wewe, ambapo aliamuru tutiiwe kama alivyoamuru utiiwe wewe, na Mtume (saw) akafikisha ujumbe kutuhusu kama alivyofikisha ujumbe kukuhusu wewe na Mwenyezi Mungu akatuondolea uchafu kama alivyokuondolea wewe……. Basi alipoaga dunia Ali (as), al-Hassan ndiye aliyestahiki kuwa Imam…….’
***********
Na muhtasari wa mambo tuliyoyasoma kwenye kipidi cha leo ni kwamba moja ya sababu za kutotajwa majina ya Maimamu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) katika Qur’ani Tukufu ni kuwas hilo ni jambo ambalo limezoeleka katika kitabu hicho kitakatifu ambapo huwa kinamwachia Mtume Mtukufu (saw) ubainishaji wa kina wa mambo yanayokusudiwa kwa ujumla na Qur’ani Tukufu, kama tunavyoshuhudia wazi jambo hilo kuhusiana na swala, zakaa, hija na ibada nyinginezo. Sababu ya pili ni kwamba takwa la Qur’ani ni kutaka kutanabaisha na kuwafahamisha watu kwamba kusudio la amri ya Mwenyezi Mungu ni kuwataka wafuate na kuwatii Ahlul Beit (as) – wakiwa ni watu waliopewa isma na Mwenyezi Mungu na ambao wanafaa zaidi miongoni mwa watu kuwa Maimamu na makhalifa wa Mtume (saw).
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kwa juma hili, kipindi ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhiri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema: Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.