Jul 10, 2016 07:46 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (131)

Assalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu ya 131 ya kipindi hiki kinachozungumzia masuala mbalimbali ya itikadi ya Kiislamu.

Kama tulivyosema katika kipindi kilichopita kipindi cha juma hili kitaendelea kuashiria maandiko ambayo yanajibu swali ambalo tulilijadili katika kipindi hicho ambalo linasema: Je, aya ya kukamilishwa dini na kutimia neema ya Mwenyezi Mungu inazungumzia Uimamu wa Imam Ali (as) peke yake au inahusiana pia na Uimamu wa Maimamu wengine watoharifu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw)?

Tuliandaa mazingira ya kujibu swali hili katika kipindi kilichopita ambapo tuliashiria aya ya 67 ya Surat al-Maida ambapo tulifahamu kuwa aya hiyo inasema wazi kwamba Mweyezi Mungu Mtukufu anafahamu sehemu ya kuweka risala na ujumbe wake. Tuliona katika kipindi hicho kwamba Mwenyezi Mungu alimuamuru Mtume (saw) kutangaza katika Hija yake ya mwisho tangazo muhimu kutoka kwa Muumba wake ambapo kama hangefanya hivyo, basi hangekuwa amewafikishia watu asili ya ujumbe aliopewa kuwafikishia. Suala hili bila shaka lina maana kwamba jambo aliloamuru Mwenyezi Mungu litangazwe ni nguzo ya dini yake aliyowajaalia wanadamu, ambayo (nguzo) kama isingekuwepo basi dini isingekamilika. Ni kwa msingi huo ndipo aya ya kukamilika dini na kutimia neema ikateremka baada ya Mtume Mtukufu (saw) kutangaza kile alichoamrishwa kukitangaza katika tukio la Ghadir Khum. Aya hii iliteremka kubainisha kwamba kwa kutangazwa jambo hilo, Mwenyezi Mungu alikuwa amekamilisha dini yake ambayo aliwaridhia waja wake kuifuata na kuwahalalishia mambo mezuri. Je, ni jambo gani hilo alilolitangaza Mtume (saw)?

**********

Ndugu wasikilizaji wanazuoni na wafasiri wa Qur’ani Tukufu wa madhehebu zote mbili za Suni na Shia wamethibitisha katika utafiti wao wa kielimu kwamba jambo alilotangaza Mtume Mtukufu (saw) siku ya Ghadir lilitimia katika kujibu amri aliyopewa na Mwenyezi Mungu kupitia aya ya 67 ya Surat al-Maida ambayo inasema: Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako. Na kama hutafanya, basi hukufikisha ujumbe wake; na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.

Katika tukio hilo la Ghadir Mtume (saw) ambaye alikuwa akitoka katika Hija yake ya mwisho akiwa ameadamana na Mahujai wengiene, aliamuru Mahujaji wote wakusanyike katika eneo la Ghadir Khum ambalo ndilo lililokuwa eneo la mtawanyiko wa Mahujaji kuelekea katika nchi zao, ili idadi kubwa zaidi ya Mahujaji wapate kusikia yale aliyokuwa ameamrishwa na Mwenyezi Mungu kuwatangazia.

Katika kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, Mtume (saw) alimteua Imam Ali (as) kuwa khalifa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake kwa kusema: ‘Yule ambaye mimi ni Maula wake (kiongozi/msimamizi wa masuala yake) basi na huyu Ali ni Maula wake. Allahuma mpende anayempenda na mchukie anayemchukia, mnusuru anayemnusuru na mdhalilishe anayemdhalilisha.’ Kisha aliamuru Waislamu kumbai nao wakambai (kumpa mkono wa utiifu) na hilo lilitimia kwa ajili ya kutekeleza amri na kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu.

Hadithi ya Ghadiri imepokelewa kwa wingi katika vitabu vya madhehebu yote mawili ya Shia na Suni ambapo imepokewa kutoka kwa karibu masahaba 100. Kupokelewa kwingi kwa hadithi kama huku hakujawahi kunukuliwa kuhusiana na hadithi nyingine yoyote kati ya hadithi tukufu za Kiislamu.

Kufikia hapa tunafahamu kwamba aya hii ni dalili tosha na kamilifu ya Qur’ani Tukufu ambayo inathibitisha Uimamu wa Imam Ali (as), dalili ambayo hakuna mtu yoyote mwenye insafu na muadilifu anayeweza kuipinga licha ya kuwepo hujudi zote za kuficha ukweli huo, isipokuwa wale manazuoni vibaraka wa utawala wa Bani Umaiyya na Bani Abbas ambao walifanya jitihada kubwa za kubuni hadithi bandia au kupotosha maana ya hadithi tuliyotangulia kuisoma. Ili kuwaridhisha mabwana zao wanazuoni hao walipotosha kabisa maana ya maneno, ‘yule ambaye mimi ni Maula wake’ katika hadithi hiyo. Je, hotuba ya Mtume (saw) iliisha baada ya yeye kumtangaza Imam Ali al-Murtadha (as) kuwa Imam na khalifa wa Umma wa Kiislamu? Jibu la swali hili litakujieni hivi punde, hivyo endeleeni kuwa pamoja nasi.

************

Ndugu wasikilizaji, tunapochunguza hadithi zinazozungumzia hotuba ya Mtukufu Mtume (saw) katika eneo la Ghadir Khum tunapata kwamba aliandaa vyema uwanja wa kumtangaza Imam Ali (as) kuwa Imam na khalifa wa Waislamu kwa kuwataka Waislamu washikamane na kufungamana vilivyo na Vizito Viwili ambavyo ni Kitabu Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu yaani Qur’ani Tukufu na Ahlul Bait wake watoharifu (as). Katika riwaya inayohusiana na hotuba hii ambayo imenukuliwa na faqihi wa Kishafi’ Sheikh al-Islam al-Juweini ambaye ni mmoja wa wanazuoni mashuhuri walioishi katika karne ya saba Hijiria, katika kitabu chake cha Faraid as-Simtwein anasema baada ya kunukuu sehemu ndefu ya hotuba hiyo: ‘Kisha Mtume alisema: ‘Enyi watu! Mimi ninakutangulieni na nyinyi mtanijia kwenye Hodhi…. Nami nitakuulizeni kuhusiana na Vizito Viwili, basi tazameni jinsi mtakavyoniwakilisha kwenye vitu hivyo……Hapo mtu mmoja akapaza sauti kwa kuuliza: Je, ni Vizito Viwili vipi ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?  Mtume akajibu kwa kusema: Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Upande mmoja wa kitabu hicho uko mkononi mwa Mwenyezi Mungu na upande mwingine uko mikononi mwenu, basi shikamaneni nacho na wala msipotee wala kukibadili. Cha pili ni kizazi, Ahlul Beit wangu. Hakika Mwenyezi Mungu mwenye huruma na mjuzi wa mambo yote amenijulisha kwamba viwili hivi havitaachana hadi vitakaponifikia kwenye Hodhi…… Basi msivitangulie mkaja mkahiliki wala kuchwa nyuma navyo mkaja mkahiliki na msivifundishe kwa sababu vina ujuzi kukulikoni nyinyi.’ Kisha akasema: Je, hamjui kwamba mimi ni mbora wa kusimamia masuala ya waumini kuliko nafsi zao?....... Je, si mnashuhudia kwamba mimi ni mbora wa kila muumini kuliko alivyo yeye mwenyewe kwa nafsi yake?

Wakasema: ‘Ndio ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!’ Hapo Mtume akaushika mkono wa Ali na kusema: ‘Enyi watu! Mwenyezi Mungu ni Maula wangu na mimi ni Maula wenu. Hivyo, yule ambaye mimi ni Maula wake basi na huyu Ali ni Maula wake. Allahuma mpende anayempenda na mfanyie uadui anayemfanyia uadui, mnusuru anayemnusuru na mdhalilidhe anayemdhalilisha na mpende anayempenda na mchukie anayemchukia.’ Kisha Mtume alisema: ‘Eeh Mwenyezi Mungu shuhudia!’…….Basi hawakuwachana – Mtume na Ali -  hadi aya hii ilipoteremka: Leo nimekukamilishieni dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo dini….

Mtume akasema: 'Mwenyezi Mungu ni mkubwa kwa kukamilisha dini na kutimiza neema na kuridhia kwake ujumbe wangu na wilaya (uongozi) ni ya Ali baada yangu.’

*********

Kwa maelezo hayo wapenzi wasikilizaji tunafikia natija hii kwamba kile alichokitangaza Mtume Mtukufu (saw) siku ya Ghadir Khum kwa amri yake Mwenyezi Mungu kilijumuisha kutangazwa kwa Uimamu wa Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) kupitai Hadithi ya Thaqalain. Hii ni pamoja na kuwa siku hiyo pia Mtume (saw) alimtangaza wazi Imam Ali (as) kuwa Imam na khalifa wa kwanza wa Umma wa Kiislamu. Kwa msingi huo aya tuliyotangulia kusoma inakuwa ni dalili na hoja ya wazi ya Qur’ani Tukufu kuthibitisha Uimamu wa Maimamu wote watoharifu wa Nyumba ya Mtume (saw). Hii ni kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika vya wanazuoni wa Kisuni lakini kwa mtazamo wa madhehebu ya Watu wa Nyuma ya Mtume (saw) yaani Ahlul Beit (as) ambao ni Mashia, jambo hili limewekwa wazi kabisa na Inshallah tutakutajieni mifano ya jambo hili katika kipindi chetu kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain.

Basi hadi wakati huo hatuna budi kukuageni kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka Tehran kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.