Apr 28, 2024 04:25 UTC
  • Jumapili, 28 Aprili, 2024

Leo ni Jumapili 19 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria sawa na 28 Aprili 2024 Miiladia.

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, Benito Mussolini dikteta wa Kifashisti wa Italia aliuawa kwa kunyongwa na wazalendo wa nchi hiyo. Mussolini alizaliwa Julai 29 mwaka 1883 katika familia masikini huko kaskazini mwa Italia. Baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu alianza kufanya kazi ya uandishi katika magazeti. Machi 23 mwaka 1919 Mussolini alistafidi na uasi na hali ya vurugu iliyojitokeza  nchini italia na kuanzisha Chama cha Ufashisti na kuwa kiongozi wa chama hicho. Ushindi wa chama hicho katika uchaguzi wa 1922 ulimfanya Benito Mussolini kuwa Waziri Mkuu baada ya kumridhisha mfalme. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, Marekani ililazimika kuondoka kwa madhila huko Vietnam baada ya kupata kipigo cha kuaibisha. Majeshi ya Marekani yaliingia Vietnam kwa shabaha eti ya kukabiliana na kasi ya kuenea ukomonisti na kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji waliokuwa maarufu kwa jina la Viet Cong huko Vietnam ya kaskazini. Katika vita hivyo Marekani ilitumia silaha zote zilizopigwa marufuku isipokuwa silaha za nyuklia. Wapiganaji hao wa mwituni walifanikiwa kutoa kipigo kikali kwa majeshi ya Marekani na tarehe 28 Aprili mwaka 1975 Rais Richard Nixon wa Marekani aliwaamuru wanajeshi wa nchi hiyo kuondoka Vietnam. ***

Marekani na vita vya Vietnam

 

Miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo, makundi ya Mujahidina wa Afghanistan hatimaye yalipata ushindi baada ya mapambano ya miaka 13 dhidi ya jeshi la Urusi ya zamani na serikali ya kibaraka ya nchi hiyo. Baada ya majeshi ya Urusi ya zamani kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka 13, hatimaye mwezi Februari mwaka 1989 wanajeshi hao wa Urusi walilazimika kuondoka Afghanistan. Hata hivyo kutokana na makundi hayo ya Kiafghani kutokuwa na mikakati mizuri na pia kutopata misaada kutoka nje, vikosi vya serikali ya Afghanistan viliendelea kubakia madarakani chini ya uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Urusi ya zamani. Aprili 28 Mujahidina walifanikiwa kuuteka kikamilifu mji wa Kabul na kuiondoa madarakani serikali kibaraka ya Afghanistan. ***

Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sheikh Muhammad Ghazali mwanazuoni na mwanamageuzi mkubwa wa Misri. Alizaliwa mwaka 1917 huko nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 10 tu, tayari Muhammad Ghazali alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu yote. Muhammad Ghazali alihitimu Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 24. Fikra zake zilijengeka juu ya msingi wa mageuzi ya maarifa ya kidini, kukurubisha baina ya madhehebu za Kiislamu na kupinga fikra za kikaumu. Muhammad Ghazali aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 79 kwa mshtuko wa moyo na kuzikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina. ***

شیخ محمد غزالی

 

Katika siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, yaani tarehe 9 Ordibehesht mwaka 1378 Hijria Shamsia, wawakilishi wa duru ya kwanza ya Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji nchini Iran walianza kazi zao na siku hii inajulikana hapa nchini kwa jina la Siku ya Mabaraza. Kwa kuzingatia kwamba, katika Uislamu suala la mashauriano na kuwa na fikra moja lina umuhimu mno, katika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia, Mabaraza yana nafasi muhimu na ni dhihirisho la urada ya wananchi katika mfumo wa kidini nchini Iran wenye ridhaa ya wananchi. Katika sheria hiii Mabaraza mbalimbali huchaguliwa na wananchi kwa ajili ya kuongoza masuala tofauti ya nchi ambapo Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) na Baraza la Wanazuoni Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu ni miongoni mwa mabaraza hayo. ***