May 17, 2024 03:41 UTC
  • Ijumaa, tarehe 17 Mei, mwaka 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 8 Mfunguo Pili Dhulqaada 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 17 Mei, 2024.

Siku kama ya leo miaka 1097 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Ali bin Zubair Kufi, mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa wakati huo.

Katika ujana wake Ibn Zubair alisoma kwa baba yake elimu muhimu tofauti za wakati huo. Baada ya baba yake kufariki dunia aliutumia utajiri wa baba yake huyo katika njia ya kutafuta elimu, kuasisi maktaba na kuwasaidia wanafunzi wa kidini waliokuwa na hali ngumu ya kimaisha.

Mbali na uhodari mkubwa katika uandishi, Ibn Zubair alikuwa na kipawa cha kuandika upya baadhi ya vitabu vya wasomi wengine na kuvisambaza.

Siku kama ya leo miaka 1066 iliyopita, alifariki dunia Abu Hamid Swaghani, mtaalamu wa nujumu na hesabati wa Iran.

Abu Hamid alizaliwa mjini Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran, na baadaye kuhamia mjini Baghdad Iraq. Msomi huyo alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika uga wa elimu ya nujumu na hisabati wa zama zake sanjari na kuasisi kituo cha unajimu mjini Baghdad. Msomi huyo ameacha vitabu vingi katika fani ya nujumu. 

Siku kama ya leo miaka 1060 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Ali bin Omar Dar-Qutni, mwandishi na mtaalamu wa sheria za Kiislamu.

Dar-Qutni alifanya safari nchini Misri na Sham na kupata elimu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo. Msomi huyo alikuwa hodari katika tafsiri ya Qur’ani Tukufu, fiq’hi, mashairi na fasihi ya lugha ya Kiarabu.

Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya ‘al-Sunan’, ‘Sunan Dar Qutni’ na ‘al-Mukhtalif Wal-Mu’talif.’ 

Miaka 275 iliyopita, katika siku kama hii ya leo alizaliwa Edward Jenner, tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (small pox). 

Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui tarehe 14 Mei mwaka 1796 akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Baada ya hapo ugonjwa huo wa ndui ulitibiwa kwa kutumia chanjo hiyo.

Maradhi hayo ambayo wakati huo yalikuwa yakichukua roho za watu bila ya huruma, yalitokomezwa kabisa duniani mwaka 1979. 

Edward Jenner

Miaka 159 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kimataifa katika uwanja wa mwasiliano huko Paris Ufaransa.

Utiaji saini huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 20 duniani. Kwa utaratibu huo kukawa kumepasishwa hati ya kuasisiwa Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana siku hii ikapewa jina la Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano.

Mwaka 1932 kwa mujibu wa maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano wa Madrid Uhispania, jina la Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu au Internatioanl Telegraph Union lilibadilishwa na kuwa, Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano au  International Telecomunication Union (ITU) na vipengee pamoja na sheria za jumuiya hiyo zikapitiwa upya.

Kuanzia mwaka 1947, taasisi hiyo ikawekwa rasmi katika faharasa ya asasi zilizoko chini ya Umoja wa Mataifa. 

Katika siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, dola la Uingereza ambalo Palestina ilikuwa chini ya mamlaka yake, lilitoa kitabu kilichopewa jina la "Kitabu Cheupe" (The White Paper) na hivyo kukawa kumepigwa hatua nyingine katika njia ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel. Wapalestina ambao walikuwa wakifahamu vyema himaya ya Uingereza kwa Wazayuni, waliukataa mpango uliokuwa umependekezwa katika kitabu hicho kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.