Apr 29, 2024 04:33 UTC
  • Tuujue Uislamu (10)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

 

Katika sehemu ya 10 ya mfululizo huu juma hili tutaendelea kuzungumzia maudhui ya tawhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na kumtambua Mola Muumba wa ulimwengu huu na vilivyomo. Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Ulimwengu wa uumbaji ni kitabu kilicho wazi kwetu ambacho kinaweza kusomwa katika lugha yoyote. Kwa hivyo mtu yeyote kutoka kabila na rangi yoyote anaweza kusoma kitabu hiki na kufikiria yaliyomo. Kadiri ujuzi wa mtu juu ya siri za uumbaji unavyoongezeka, ndivyo ufahamu wake kuhusu muumba wa ulimwengu unavyoongezeka. Kwa maneno mengine ni kuwa, kuna uhusiano wa karibu kati ya "maendeleo ya sayansi (elimu)" na "imani juu ya Mwenye Ezi Mungu". Kulingana na mwanasayansi wa zama hizi na mwanabiolojia, Albert Winchester ni kuwa: Kila ugunduzi mpya unaofanyika katika ulimwengu wa sayansi huongeza nguvu ya imani yetu na kuondoa majaribu yaliyofichika ambayo yapo zaidi au kidogo katika mioyo na katika batini ya waumini na nafasi yake kuchukuliwa na mawazo ya juu ya theolojia na imani ya Mungu mmoja.

Kwa mtazamo huu, kila moja ya sayansi asilia kama vile fizikia, kemia, biolojia, fiziolojia, tiba, botania na kadhalika inaweza kuchukuliwa kama tawi la theolojia. Kwa sababu elimu hizi zote zinajadili kuhusu siri na sheria na mifumo ya ajabu ya uumbaji, mifumo ambayo uangalifu na uchunguzi ndani yake unamuonyesha mwanadamu ishara za muumbaji pekee wa ulimwengu. Bahari ni moja ya matukio ya asili ambayo yamekuwa ya kushangaza na ya ajabu machoni pa wanadamu. Baadhi ya siri na mafumbo ya bahari bado hayajafumbuliwa, licha ya maendeleo yote ya kisayansi na wanadamu hawadai kuwa wamepata siri zao zote. Mimea mdogo zaidi inayowezeka kuonekana kwa darubini tu pamoja na mimea mikubwa zaidi huota na kukua katika bahari. Kufikia sasa, hakuna njia iliyopatikana ya kujua idadi ya viumbe vya baharini na hata kukadiria idadi yao, ambayo ni katika mabilioni.  Kwa hakika haya yote ni mambo ya kushangaza ambayo bila shaka mwanadamu hawezi kufikia uhakika wake na kujua siri za ndani na zilizofichika baharini isipokuwa Muumba wa ulimwengu huu.

 

Katika kina kirefu cha bahari, kati ya miamba migumu na isiyo sawa, kuna samaki wanaishi ambao ni vipofu, lakini miili yao inabaki na kuwa na afya kati ya mawe na miamba mikali kwenye sakafu ya bahari. Hata samaki wawindaji hawajaweza kutokomeza kizazi chao. Je, samaki hawa wanaendeleaje kuishi? Inapasa kusema kwamba, Mungu amewapa samaki hawa vipofu uwezo wa ajabu wa kiakili. Miili yao ni nyeti sana kiasi kwamba bila kuona popote, wanaona hatari kwa mbali na kujilinda na mawindo ya adui. Wanapata chakula chao kutoka kwenye kina kirefu cha bahari. Chini kabisa ya bahari ambako hakuna mwanga, kuna wanyama wanaishi ambao wao wenyewe hutoa mwanga. Inawezekana kusema kwamba, huu ni mpango wa Muumba mwenye hekima wa ulimwengu ili wanyama wa baharini waweze kuishi kwa raha katika giza hilo. Mwili wa wanyama kama hao ni sugu na wenye nguvu sana kiasi kwamba wanaweza kuhimili mashinikizo makubwa ya maji kwenye kina cha bahari. Kama mnnavyojua, maji ya bahari yana chumvi. Nini kingetokea ikiwa maji ya bahari yangekuwa matamu? Imethibitishwa kisayansi kwamba, kukabiliana maji ya chumvi mambo ya uharibifu ni mkubwa zaidi kuliko ule wa maji matamu. Kama maji katika bahari yangekuwa matamu, hatari ya kuharibika kwa maji ingeongezeka. Katika mazingira haya hakuna athari ya viumbe hai ingebaki katika bahari. Kwa muktadha huo, sehemu kubwa ya mahitaji ya wanadamu, pamoja na vyanzo vyao vya chakula, vingeangamia. Kwa kuharibika maji ya bahari na bahari, maisha ya wanadamu na wanyama wengine wa nchi kavu pia yangekabiliwa na tishio na hivyo kuwa hatarini. Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa mpango wake wa busara. Hasa kwa kuzingatia kwamba, maji matamu na masafi ya kunywa yanatoka katika chanzo kingine kisicho cha bahari ambacho ni mvua.

 

Mvua ni zawadi ya Mwenyezi Ezi Mungu ambayo haiburudishi asili tu, bali pia roho ya mwanadamu. Matone ya mvua ya upole yanaonyesha uwezo na huruma ya Mungu isiyo na kikomo. Kwa mvua, kila kitu hupata harufu ya uhai, nishati na uzima. Misitu minene, nyasi laini, mashamba mazuri na bustani za maua zenye mandhari nzuri, zote zimeipamba dunia kutokana na mvua. Ndani ya Qur’ani, Mwenyezi Mungu ametaja ukuaji wa mimea na mboga na rutuba ya ardhi kwa kuashiria mwendo wa mawingu na kunyesha kwa mvua, na pia ametaja faida ya maji, jinsi yanavyohuisha ardhi kavu na iliyokufa.

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 39 ya Surat Fussilat:

Na katika ishara Zake (kwamba, Mungu yupo) ni kwamba, unaiona ardhi imedhalilika (kwa kukosa mvua), lakini tunapoiteremshia maji, mara unaiona inataharaki na kuumuka; bila shaka aliyeihuisha ndiye atakayehuisha waliokufa. Hakika Yeye ndiye mwenye uweza juu ya kila kitu.

Aidha Aya ya 10 ya Surat al-Nahl inasema:

Yeye ndiye anayekuteremshieni maji kutoka mawinguni; kwa hayo mnapata kinywaji na kwa hayo (inatoa) miti ambayo humo mnalisha (wanyama).

Wapenzi wasikilizaji, kwa mvua, mbegu ndogo ambazo zimefichwa ndani kabisa ya udongo, hatimaye hutoka kwa uzuri kutoka kwenye udongo na hupigwa na jua na upepo. Hatimaye, mbegu hizi hugeuka kuwa mimea na miti mikubwa na yenye nguvu. La kushangaza zaidi ni kuwa, matone ya mvua si makubwa sana kiasi kwamba yaharibu ardhi na kilimo, na si madogo kiasi kwamba yapotelee angani. Kwa hakika, Mungu hutuma mvua kwa kiasi fulani kulingana na neema yake.

Maji ya mvua hutiririka ndani ya mito na vijito au huhifadhiwa kwenye chemchemi za maji chini ya ardhi kama rasilimali za maji zitakazotumika. Hapana shaka kuwa, yote haya yanathibitisha juu ya kuweko Muumba na msimamizi mwenye hekima wa yote haya ambaye ni Muumba wa ulimwengu huu.

Tunahitimisha kipindi chetu cha leo kwa Aya ya pili ya Surat al-Furqan ambayo inaonyesha kwamba, Mwenyezi Mungu hana mwana wala mshirika katika mamlaka yake. Aya hiyo inasema:

(Mwenyezi Mungu) ambaye ni wake (peke yake) ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuzaa mtoto wala hana mshirika katika ufalme (wake), na ameumba kila kitu na akakikadiria kipimo chake.

 

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umemalizika hivyo sina budi kukomea hapa nikitaaraji kuwa mtajiunga nami juma lijalo siku na wakati kama huu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh