Jumatatu, 27 Mei, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 18 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1445 Hijria sawa na tarehe 27 Mei 2024.
Katika siku kama ya leo miaka 541 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82, Luca della Robbia, msanii mkubwa wa uhunzi wa Italia. Akiwa kijana alijifundisha kazi ya ufuaji dhahabu, hata hivyo aliachana na kazi hiyobaadaye na kujihusisha na uhunzi wa masanamu. Katika kipindi hicho alipata kuunda masanamu na athari mbalimbali za kale. Athari kadhaa za Luca della Robbia zipo katika majengo tofauti ya maonyesho duniani. ***
Miaka 187 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 27 Mei 1837, ulitiwa saini mkataba wa amani kati ya Ufaransa na Amir Abdulqadir wa Algeria kiongozi wa wapigania uhuru wa nchi hiyo. Tangu mwaka 1832 baada ya mashambulizi ya jeshi la Ufaransa nchini Algeria Amir Abdulqadir aliendesha mapambano dhidi ya wavamizi huko Algeria na kusimama kidete dhidi yao kwa miaka kadhaa na kujulikana kama kiongozi wa wanamapambano wa Algeria dhidi ya Ufaransa. Baada ya kufikiwa makubaliano hayo maeneo mengi ya Algeria yaliyokuwa chini ya Ufaransa yalipewa uhuru. ***
Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67 Robert Koch, mgunduzi wa vijidudu maradhi aina ya bakteria na tabibu mashuhuri wa Kijerumani aliyegundua chanzo cha maradhi ya kifua kikuu au TB.
Daktari Robert Koch alianza kutwalii na kufanya utafiti mkubwa juu ya sababu au vyanzo vya kutokea baadhi ya magonjwa kama vile kipindupindu, kimeta na kifua kifuu, baada ya kuhitimu masomo yake katika fani ya tiba. Mwaka 1882 Miladia, Robert Koch alifanikiwa kugundua vijidudu maradhi vinavyoitwa mycobacterium tuberculosis vinavyosababisha kifua kikuu. Ili kukamilisha uchunguzi wake tabibu huyo Mjerumani alisafiri katika nchi za Afrika Kusini, Misri na India na kutwalii magonjwa mengineyo maarufu katika maeneo hayo kama vile Malaria. Mwaka 1905 Robert Koch alitunukiwa Tunzo ya Nobel katika uwanja wa Tiba. ***
Miaka 98 iliyopita katika siku kama ya leo, harakati ya mapambano ya Riffi nchini Morocco dhidi ya mkoloni Muhispania na Ufaransa, ilipata pigo. Kwa miaka kadhaa Muhammad Abdul-Karim al-Khitwabi, maarufu kwa jina la Amir Muhammad Riffi, kiongozi wa harakati hiyo, alifanya mapambano mengi na wavamizi wa Uhispania huku akifikia ushindi kadhaa. Ushindi wake dhidi ya majeshi vamizi ya Uhispania uliitia khofu Ufaransa. Mwanzoni mwa mwaka 1924 Miladia askari wa Ufaransa waliingia Morocco kwa ajili ya kuwasaidia wenzao wa Uhispania dhidi ya harakati hiyo ya Riffi. Katika kipindi hicho askari hao wa Ufaransa walifanya mauaji makubwa dhidi ya raia wa nchi hiyo. Aidha baada ya askari vamizi wa Ufaransa na Uhispania kumtia mbaroni Muhammad Abdul-Karim al-Khitwabi walitekeleza jinai kubwa dhidi ya maelfu ya wafuasi Waislamu wa harakati ya Riffi. ***
Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Kiislamu Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa. Ayatullah Kashiful Ghitaa alizaliwa katika mji mtakatifu wa Najaf katika familia ya wasomi na wacha-Mungu na kuanza kutafuta elimu akiwa bado mtoto mdogo. Baada ya kukamilisha elimu ya msingi, Ayatullah Kashiful Ghitaa alihudhuria darsa za maulamaa wakubwa wa zama hizo na kukwea daraja za juu za elimu katika kipindi kifupi. Alifanikiwa kulea wasomi na maulamaa wakubwa na kufanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kueneza elimu na maarifa. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu pia alikutambua kushiriki katika masuala ya kisiasa na kutilia maanani masuala ya serikali na utawala kuwa ni katika mambo ya wajibu na alikuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha Harakati ya Kitaifa ya Iraq. Ayatullah Kashiful Ghitaa alishiriki vilivyo katika mapigano ya jihadi ya wananchi wa Iraq wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia dhidi ya jeshi vamizi la Uingereza. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.
Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, yaani tarehe saba Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsia duru ya kwanza ya Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (bunge) ilianza. Kufunguliwa duru hiyo ya Majlisi ya kutunga sheria ilikuwa hatua muhimu katika historia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Jukumu la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ni kutunga sheria na kusimamia kwa njia ya moja kwa moja utendaji kazi wa rais wa nchi na baraza lake la mawaziri. Hivi sasa Majlisi ina wajumbe 290 ambao huchaguliwa moja kwa moja na wananchi. Kila eneo hupata mbunge kwa kutegemea idadi ya watu wa eneo hilo. Idadi ya wafuasi wa dini za wachache hapa nchini, ingawa haiwezi kufikia kiwango kinachohitajika kwa ajili ya kutengewa mbunge, lakini katiba ya nchi inawapa fursa ya kuwachagua wawakilishi wao bungeni. Vikao vya wazi vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu hutangazwa moja kwa moja kwa njia ya redio na vile vile magazeti ya nchini hutoa ripoti kuhusu vikao hivyo.