Alkhamisi, 30 Mei, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Mfunguo Pili Dhulqaada 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 30 Mei 2024.
Miaka 280 iliyopita katika siku kama ya leo, Alexander Pope mshairi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiingereza aliaga dunia. Alizaliwa mjini London Mei 21 mwaka 1688 katika familia ya kitajiri. Hata hivyo kutokana na kuwa na ulemavu wa viungo, baba na mama yake walimlea nje ya mji katika nyumba moja. Alipofikisha umri wa miaka 15 Alexander Pope alikuwa tayari anazifahamu vyema lugha za Kigiriki, Kifaransa na Kitaliano. Alitoa mjumuko wake wa kwanza wa mashairi alipokuwa na umri wa miaka 23. ***
Siku kama ya leo miaka 246 iliyopita sawa na tarehe 30 Mei 1778, Francois - Marie Arouet maarufu kwa jina la Voltaire, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84. Katika maisha yake, Voltaire aliwahi kuwekwa mahabusu mara mbili na kubaidishwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Uingereza. Kitendo hicho kilimkasirisha sana Voltaire na kumfanya kuwa dhidi ya utawala wa Ufaransa. ***
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita inayosadifiana na tarehe 30 Mei 1981, aliuawa Ziaur Rahman, Rais wa Bangladesh baada ya kupigwa risasi katika mji wa Chittagong ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Rais Ziaur Rahman aliuawa baada ya kuchungulia dirishani kwenye nyumba ya wageni ya serikali katika mji huo. Watu wanane waliuawa kwenye shambulio hilo, wakiwemo wasaidizi na walinzi wa rais huyo. ***