Jun 02, 2024 02:24 UTC
  • Jumapili, Pili Juni, 2024

Leo ni Jumapili tarehe 24 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1445 Hijria sawa na tarehe Pili Juni 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1244 iliyopita Imam Ali bin Musa Ridha (a.s) alianza safari yake kutoka Madina kuelekea Marv huko Kaskazini Mashariki mwa Iran ya zamani. Imam Ridha (a.s) alifanya safari hiyo kwa kulazimishwa na kushinikizwa na Maamun, khalifa na mtawala wa saba wa ukoo wa Bani Abbas. Lengo la safari hiyo lilikuwa kumuweka Imam Ridha chini ya uangalizi. Maamun alitoa pendekezo kwa Imam huko Marv kwamba akubali kuwa mrithi wake. Maamun alifanya hivyo ili kujionyesha kuwa ni mtu mwenye mapenzi na Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad (s.a.w). Hata hivyo katika fursa mbalimbali Imam Ridha si tu kwamba alionyesha kuwa hakubali kushirikiana na  utawala wa Bani Abbas, bali pia aliutambua utawala huo kuwa ni wa kupenda makuu na wa kidhalimu.  ***

Katika iku kama hii ya leo miaka 142 iliyopita alifariki dunia Giuseppe Garibaldi kamanda mzalendo na kiongozi wa harakati ya kuleta umoja wa Italia. Giuseppe alizaliwa mwaka 180 na wakati wa ujana wake alifanya kazi mbalimbali na mwishowe kujiunga na jeshi. Baadaye alichaguliwa kuwa kamanda wa wanaharakati wa kupigania uhuru wa Italia na alifanya jitihada nyingi za kuleta umoja nchini humo. Kwa ajili hiyo alijulikana katika historia ya Italia kama shujaa wa taifa. ***

Miaka 61 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 3 Juni 1963, Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kwa mnasaba wa Ashura ya Imam Hussein (AS) alitoa hotuba kali na ya kihistoria dhidi ya utawala wa kiimla wa Kipahlavi. Hotuba hiyo ilitolewa mbele ya hadhara kubwa ya wananchi wakiwemo maulamaa na wanafunzi wa kidini wa chuo cha Fayziyyah katika mji wa Qom, licha ya vizuizi na vitisho vikali vilivyotolewa na utawala wa Shah. Katika hotuba yake, Imam Khomeini alikosoa vikali vitendo vya kihaini vya Shah na vibaraka wake na kufichua mbele ya wananchi Waislamu wa Iran usaliti waliokuwa wakifanya. Katika sehemu moja ya hotuba hiyo, Imam Khomeini alisema: "Hawa wanaupinga Uislamu wenyewe pamoja na mashekhe na wana nia ya kuuangamiza. Enyi watu, Uislamu wetu na nchi yetu viko hatarini. Tuna wasiwasi mkubwa na tunasikitikishwa na hali ya Iran na hali ya walioshika hatamu za utawala." ***

Tarehe Pili Juni ni Siku ya Taifa ya Uingereza. Nchi ya kisiwa ya Uingereza yenye eneo lenye ukubwa wa zaidi ya kilomitamraba 244,000 inapatikana upande wa Magharibi ya Ulaya na baina ya bahari za Atlantiki, Manche, bahari ya kaskazini na Bahari ya Ireland. Uingereza ina idadi ya watu wanaokaribia milioni 60. Mfumo wa utawala wa nchi hiyo ni wa kifalme, lakini mamlaka ya utendaji ya serikali yako mikononi mwa waziri mkuu. Akthari ya Waingereza ni wafuasi wa madhehebu ya Anglikana ambalo ni tawi la madhehebu ya Kikristo ya Protestanti. Uingereza imetokana na muungano wa Scotland, England, Wales na Ireland ya Kaskazini. Maeneo hayo kila moja lina mamlaka maalumu ya kujiendeshea mambo yake ya ndani. Tarehe Pili Juni, ambayo ni siku aliyozaliwa Malkia, inajulikana kuwa Siku ya Taifa ya Uingereza. ***

Tags