Hikma za Nahjul Balagha (49)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 49 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 49 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 42.
Siku moja Imam Ali AS alimwambia mmoja wa masahaba wake aliyekuwa mgonjwa kwamba:
جَعَلَ اللَّهُ مَا کَانَ مِنْ شَکْوَاکَ حَطّاً لِسَیِّئَاتِکَ فَإِنَّ الْمَرَضَ لَا أَجْرَ فِیهِ وَ لَکِنَّهُ یَحُطُّ السَّیِّئَاتِ وَ یَحُتُّهَا حَتَّ الْأَوْرَاقِ وَ إِنَّمَا الْأَجْرُ فِی الْقَوْلِ بِاللِّسَانِ وَ الْعَمَلِ بِالْأَیْدِی وَ الْأَقْدَامِ وَ إِنَّ اللَّهَ سُبْحَانَهُ یُدْخِلُ بِصِدْقِ النِّیَّةِ وَ السَّرِیرَةِ الصَّالِحَةِ مَنْ یَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ الْجَنَّةَ
Mwenyezi Mungu ameyafanya hayo unayoyalalamikia (yaani huu ugonjwa wako) yapunguze madhambi yako. Kwenye ugonjwa hakuna malipo, lakini ugonjwa hupukutisha madhambi kama yanavyopukutika majani makavu. Hakika malipo yanatokana na maneno yatokayo ulimini kwake na vitendo vya mikono na miguu yake. Na hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu atamwingiza peponi yeyote amtakaye katika waja Wake kwa nia yake njema na moyo wake safi.
Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa rehema na Mwenye kurehemu lakini pia rehema Zake hazina vifano kwa waja Wake. Rehema hizo zisizo na kikomo za Allah zinajidhirisha kupitia neema Zake kubwa sana kwa viumbe Wake wote, hata wale wasiomshukuru. Rehema za Allah zimekienea kila kitu. Kwa hivyo, mambo yote ambayo Mwenyezi Mungu huwateremshia waja wake yanatokana na huruma na rehema Zake iwe rehema hizo zitamfikia mja kwa njia inayompendeza au kwa sura isiyompendeza kama vile kuumwa na kuwa kwenye matatizo. Kanuni za kimaumbile duniani zimesimama kwenye msingi maalumu ambao unasema kuwa, maadamu mtu anaendelea kufanya juhudi za kujiletea ufanisi na furaha, suhula za kufikia lengo lake nazo zinaendelea kuwepo. Yumkini zikawa ziko mbali naye lakini maadamu hakati tamaa, hafanyi uzembe na anaendeleza juhudi, basi suhula za kumfanikishia mambo yake zinaendelea kuwepo tab'an kwa sharti la kufuata njia sahihi zinazotakiwa. Lakini mara tu anapoingia kwenye njia potofu, Mwenyezi Mungu humfungulia njia za matatizo na mabalaa ili kumzindua na kumshawishi arudi kwenye njia ya uongofu kwa kutubu na kufuata njia sahihi.
Moja ya faida anazopata mja wakati anapokuwa mgonjwa ni kwamba huwa wakati huo anamkumbuka sana Mwenyezi Mungu. Baadhi ya wakati pia hukumbuka kifo na madhambi aliyotenda na hufanya haraka kutubu na kurejea kwa Muumba wake. Wakati anapofanya hivyo, anapotubu na kurejea kwa Mola wake, Mwenyezi Mungu Naye humsamehe madhambi yake na kumuongezea rehema Zake. Katika khutba ya 143 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anaelezea sababu na madhumuni ya mitihani na dhiki zinazompata mja akisema: “Mwenyezi Mungu huwaadhibu waja Wake wanapofanya maovu, kwa kupunguza matunda ya miti, na kwa kutonyesha mvua, na kwa kuziba hazina za neema." ili kwa njiia hiyo mja mwenye moyo wa kutubu aweze kuachana maasi na kurejea kwenye njia sahihi. Wakati moyo wa mja mwema anayekubali nasaha, wanayekubali mawaidha na maonyo unapoacha maasi na kurejea kwa Mola wake, Mwenyezi Mungu humsamehe kwani Mlango wa toba na maghfira uko wazi muda wote.
Ugonjwa husababisha kupatikana msamaha wa madhambi lakini hauna jazaa wala malipo. Kwa sababu malipo yanahusiana na kitendo anachofanya mja; iwe amefanya kwa ulimi au kwa mikono na miiguu yake au kiungo kingine chochote cha mwili. Kitendo hicho kinapokuwa chema, malipo huwa mema na kinapokuwa kiovu, malipo huwa mabaya. Lakini mtu anapoumwa bila ya kutarajia, huwa hakufanya hivyo kwa matashi yake, bali huwa ni mtihani wa Mwenyezi Mungu ili amfungulie sababu mja Wake za kusamehewa makosa yake, kupandishwa daraja na kupewa ujira mkubwa kwa subira na imani yake.
Jambo la kuvutia zaidi hapa ni kwamba, Mwenyezi Mungu humlipa kheri mja Wake pale anapotia nia tu ya kutenda jambo jema. Sababu yake ni kuwa, nia njema ni ishara ya wema wa mja huyo na nia njema ni kitu cha kimaanawi kinachopendwa na Muumba. Lakini mtu anapotia nia ya kutenda jambo baya na ovu, Mwenyezi Mungu hamlipi kwa nia hiyo hadi pale anapokuwa ameitekeleza kivitendo njia yake hiyo ovu, na hii ni katika rehema zisizo na kikomo za Allah. Ni wazi kwamba njia njema huwa chanzo cha kuongezeka neema na baraka za Mwenyezi Mungu. Kwa kuzingatia hayo yote inabidi tuseme kwamba, matendo ya mwanadamu yanapimwa na kutathminiwa kulingana na nia yake, na ndio maana katika sehemu ya mwisho ya hikma hii ya 42, Imam Ali AS anasema: Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu atamwingiza peponi yeyote amtakaye katika waja Wake kwa nia yake njema na moyo wake safi.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.