Jun 22, 2024 00:35 UTC
  • Jumamosi, 22 Juni, 2024

Leo ni Jumamosi 15 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1445 Hijria mwafaka na 22 Juni 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1230 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Ali Naqi (AS) mashuhuri kwa lakabu ya al-Hadi, mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW, katika mji mtakatifu wa Madina. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Jawad AS, Imam Hadi alichukua jukumu zito la Uimamu na kuongoza Umma wa Kiislamu. Zama za Uimamu wake zilisadifiana na kipindi cha utawala wa ukoo wa Bani Abbas, na Mutawakkil ndiye aliyekuwa ameshika hatamu za uongozi wakati huo. Baada ya mtawala huyo kuhisi kuwa Imam Hadi (as) na wafuasi wake walikuwa hatari kwa utawala wake, aliamrisha Imam atolewe Madina na kuhamishiwa Samarra, Iraq ili amuweke chini ya uangalizi. Licha ya hayo yote, lakini Imam Naqi aliendelea kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu. ***

 

Miaka 391 iliyopita mnajimu, mtaalamu wa hisabati na mwanafizikia wa Italia Galileo Galilei alilazimika kukana itikadi zake za kisayansi na kielimu mbele ya viongozi wa Kanisa. Mwaka 1632 Galilei aliandika kitabu akijibu na kukosoa mitazamo ya Betlemosi kuhusu sayari ya jua na kutangaza kuwa dunia inazunguma jua. Mwaka mmoja baadaye Papa wa Kanisa Katoliki alimwita Galileo mjini Roma na kuitaja mitazamo hiyo ya kisayansi kuwa ukafiri. Kwa msingi huo, kanisa lilimlazimisha Galileo akane itikadi zake za kielimu la sivyo akabiliwe na adhabu ya kifo. Japokuwa msomi huyo alikana mitazamo yake hiyo ya kielimu kidhahiri tu lakini wakati alipotoka nje ya mahakama alipiga chini mguu wake na kuiambia ardhi: "Licha ya haya yote lakini wewe unazunguka."   ***

Galileo Galilei

 

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, katika Vita vya Pili vya Dunia, jeshi la Ujerumani ya Kinazi lilianza mashambulizi makubwa dhidi ya Urusi ya zamani kwa jina la Operesheni ya Barbarossa. Kwa utaratibu huo Adolph Hitler akaanzisha vita vingine katika upande wa mashariki mwa Ujerumani kwa shabaha ya kutimiza mipango yake ya kutaka kujitanua zaidi. Hadi wakati huo tayari dikteta huyo alikuwa ameteka nchi kadhaa za Ulaya. Katika operesheni hiyo, askari wa Ujerumani walisonga mbele na kufika katika viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo, Moscow. Hata hivyo jeshi la Ujerumani lilipata matatizo makubwa kufuatia kuanza kipindi cha baridi kali na hivyo likashindwa kusonga mbele. Wananchi na jeshi la Urusi katika miji mbalimbali ya nchi hiyo hususan Moscow, Leningrad na Stalingrad walipambana vikali na jeshi hilo vamizi na kulilazimisha kurudi nyuma. Mwezi Agosti 1944 jeshi la Urusi lilifika katika mipaka ya Ujerumani. ***

Operesheni ya Barbarossa

 

Katika siku kama ya leo miaka 49 iliyopita ilianzishwa Harakati ya Ukombozi wa Chad. Tangu mwishoni mwa karne ya 19 nchi ya Chad iliyoko katikati mwa Afrika ilikuwa chini ya udhibiti wa Ufaransa na ilipata uhuru mwaka 1960 baada ya kukoloniwa kwa kipindi cha karibu miaka 80. Hata hiyo iligawanyika katika sehemu mbili tofauti. Sehemu ya kaskazini iliyokuwa nyuma kimaendeleo na kiuchumi, na ya kusini iliyokuwa na suhula nyingi na makau makuu ya nchi ambayo ilidhibitiwa na Wakristo. Tarehe 22 Juni mwaka 1960 kuliundwa Chama cha Maendeleo ya Chad kwa lengo la kuunganisha tena nchi hiyo na kuimarisha umoja wa kitaifa na ustawi wa kiuchumi. Chama hicho kilivunjwa mwaka 1973 na nafasi yake ikachukliwa na Harakati ya Kitaifa ya Mapinduzi ya Kiutamaduni na Kijamii. ***

Bendera ya Chad