Jumatatu, tarehe 24 Juni, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 17 Dhulhija 1445 Hijria sawa na Juni 24 mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, Napoleone Bonaparte mtawala wa Ufaransa akiwa na kikosi cha askari 350,000 alianza kufanya mashambulio dhidi ya utawala wa Russia wa Tsar.
Miaka mitano kabla ya tukio hilo, nchi mbili hizo zilikuwa zimetiliana saini mkataba wa kutoshambuliana kijeshi. Hata hivyo taratibu uhusiano baina ya tawala mbili hizo ulianza kuharibika, na hivyo kumfanya Bonaparte afikie hatua ya kuandaa jeshi kubwa na kuishambulia Russia na kisha kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Moscow. Hata hivyo hali mbaya ya hewa yaani baridi kali na kutowafikia wanajeshi wa Kifaransa vifaa muhimu na suhula za kivita, kuliwafanya askari hao wakabaliwe na hali ngumu katika medani ya vita. Hali hiyo ilimlazimisha Bonaparte atoe amri ya kurejea nyuma vikosi vyake. Wakati wa kujiri zoezi hilo, askari jeshi wapatao 30,000 wa Kirusi waliwashambulia askari wa Bonaparte na kuwaua wengi miongoni mwao.
Akiwa amebakiwa na askari 30,000 tu, Bonaparte aliikimbia Russia na kufanikiwa kuwasili Paris Ufaransa Desemba mwaka 1812.
Katika siku kama ya leo miaka 181 iliyopita, tanuu za feleji maarufu kwa jina la tanuu za Bessemer zilivumbuliwa. Mvumbuzi wa tanuu hizo alikuwa Mwingereza Henry Bessemer. Tanuu hizo zilitumika huko Uingereza kwa mara ya kwanza na leo hii zinatumika katika masuala mbalimbali viwandani.
Tarehe 4 Tir miaka 61 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini alihamishiwa katika kambi ya kijeshi ya Eshtar-Abad baada ya kukamatwa na Shirika la Usalama Wa Taifa la Shah maarufu kwa jina la Savak.
Siku 40 baada ya kushikiliwa katika kambi hiyo, Imam Khomeini kwanza alipelekwa uhamishoni nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye akapelekwa Iraq.
Katika kipindi chote cha miaka 13 ya kubaidishiwa nje ya nchi, Imam aliongoza harakati zake za mapinduzi kupitia wanafunzi wake waliokuwa wakiwasilisha ujumbe zake kwa wananchi ndani ya Iran.
Februari mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alirejea nchini na kupokewa na watu milioni tano. Siku 10 baadaye Imam alifanikiwa kuuangusha utawala wa kifalme ulioiongoza Iran kwa kipindi cha miaka 2500.

Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita yaani tarehe 4 Tir 1367 Hijria Shamsia, ndege za utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq, kwa mara nyingine tena ziliwashambulia kwa mabomu ya kemikali wapiganaji wa Kiirani waliokuwa katika visiwa vya Majnun.
Mamia ya wanajeshi wa Iran waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Saddam.
Utawala wa zamani wa Iraq ulitumia silaha za maangamizi ya umati za kemikali tangu mwanzoni mwa vita vyake dhidi ya Iran mwaka 1359 Hijria Shamsiya, na kuzidisha matumizi ya silaha hizo sambamba na ushindi wa wapiganaji wa Iran.
