Jumatatu, tarehe Mosi Julai, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 24 Dhulhija 1445 Hijria sawa na tarehe Mosi Julai 2024.
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita kwa mujibu wa nukuu mashuhuri ya kihistoria Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na binti yake, Bibi Fatima (AS), mkwewe Ali bin Abi Twalib (AS) na wajukuu wake wawili Hassan na Hussain (AS) waliondoka Madina kwenda kufanya mdahalo na viongozi wa Wakristo wa eneo la Najran juu ya dini ya kweli.
Tukio hilo linaelezwa na Mwenyezi Mungu SW katika aya za 60 na 61 za sura ya Aal Imran. Wakati viongozi wa Najran walipoona Mtume amekuja katika mdahalo huo akiwa na watu wanne tu wa Nyumba yake tukufu walipigwa na mshangao na kuelewa kwamba, dua ya mtukufu huyo ya laana kwa atakayesema uongo itakubaliwa. Katika hali hiyo askofu wa Najran alisema: "Ninaziona nyuso ambazo iwapo zitamuomba Mwenyezi Mungu aung'oe mlima mkubwa zaidi mahala pake basi dua yao itajibiwa papo hapo. Kwa msingi huo si sahihi kufanya mdahalo na watu hawa watakatifu kwani yumkini kizazi chetu chote kikaangamia."
Baada ya hapo askofu huyo wa Najran alimuomba Mtume (SAW) kufanya suluhu na kusamehe. Tukio hilo la kihistoria lilidhihirisha haki na ukweli wa dini tukufu ya Kiislamu na utukufu na nafasi aali ya Ahlubait wa Mtume Muhammad (SAW).
Siku kama ya leo miaka 236 iliyopita alizaliwa Jean Victor Poncelet mwasisi wa uchambuzi wa maumbo.
Victor Poncelet aliyekuwa mtaalamu maarufu wa hisabati wa Ufaransa, alitambulika kuwa mwasisi wa uchambuzi wa maumbo. Poncelet alikuwa mmoja wa maafisa wa jeshi la Napolione na alitekwa nyara na Warusi wakati jeshi la Ufaransa lilipokuwa likirejea nyuma kutoka Urusi ya zamani.
Hata hivyo katika kipindi cha kutekwa alijiendeleza kielimu na kukamisha elimu yake ya uhandisi. Jean Victor Poncelet alifariki dunia tarehe 22 Disemba 1867.
Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, nchi ya Canada ilijitangazia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.
Canada iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na kuanzia wakati huo kwa zaidi ya karne mbili, Uingereza na Ufaransa zilikuwa zikishindana katika ardhi ya nchi hiyo kwa lengo la kupanua udhibiti wao. Ushindani huo ulipelekea kujiri vita kati ya mataifa hayo ya kikoloni ambapo mwaka 1689 vita hivyo vilidumu kwa karibu miaka 75 vilimalizika kwa kushindwa Ufaransa.
Kuanzia mwanzoni mwa karne ya 19 taratibu zilianza harakati za kupigania uhuru wa Canada ambazo zilizaa matunda mwaka 1867 katika siku kama ya leo.
Miaka 64 iliyopita katika siku kama ya leo, sehemu mbili za Somalia ya Uingereza na ya Italia ziliungana na kuunda nchi moja ya Somalia yenye kujitawala.
Karne kadhaa nyuma, Somalia iliwahi kujitawala kwa kipindi kifupi. Mwaka 1884 Uingereza iliiweka katika himaya yake sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Miaka mitano baadaye Italia nayo ikakoloni baadhi ya sehemu za Somalia.
Harakati za mapambano za Muhammad Abdullah Hassan dhidi ya Waingereza kuanzia mwaka 1901 hadi 1920 hazikuzaa matunda. Mwaka 1950 Umoja wa Mataifa uliitaka Italia iandae mazingira ya kujitawala na kuwa huru nchi ya Somalia.
Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, nchi ndogo ya Burundi ilijitangazia uhuru wake.
Kuanzia mwaka 1899 hadi 1917 Burundi pamoja na Rwanda ilikuwa sehemu ya makoloni ya Mjerumani huko Afrika Mashariki. Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kushindwa Ujerumani katika vita hivyo, Umoja wa Mataifa uliikabidhi Ubelgiji ardhi ya Burundi. Mwaka 1962 Burundi ilipata uhuru ikiwa na mfumo wa utawala wa kifalme.
Hata hivyo miaka minne baadaye wapigania jamhuri walimuondoa madarakani mfalme na kuanzisha mfumo wa serikali ya jamhuri.
Na siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, Rwanda ilipata uhuru.
Rwanda ina historia inayofanana na jirani yake wa kusini yaani Burundi ambapo kabla ya nchi hizo kujitangazia uhuru zilikuwa zikikoloniwa na Ubelgiji. Baada ya mapambano mtawalia ya wapigania uhuru wa Rwanda, hatimaye mnamo mwaka 1962, nchi hiyo ilipata uhuru na kabila kubwa la Wahutu likashika hatamu za uongozi wa nchi.
Mwaka 1973, Meja-Jenerali Juvenal Habyarimana alichukua madarakani baada ya kufanya mapinduzi yasiyo na umwagaji damu. Hata hivyo mwaka 1994 kulitokea mauaji ya kimbari ambapo zaidi ya watu laki 8 waliuawa wengi wao wakiwa ni wa kabila la Tutsi.