Jumatano, Julai 3, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 26 Mfunguo Tatu Dhulhija 1445 Hijria mwafaka na tarehe 3 Julai 2024.
Siku kama ya leo miaka 886 iliyopita alizaliwa huko katikati mwa Iraq, Abul-Fadhail Amedi, fakihi na mwanafasihi wa Kiislamu.
Baada ya kusoma elimu za fiqhi, Usul Fiqhi, fasihi na hisabati katika mji wa Baghdad aliondokea kuwa mahiri katika elimu hizo.
Abul Fadhail Amedi alikuwa na mashairi yenye kubeba maana kubwa. Amedi aliaga dunia akiwa katika eneo alilozaliwa akiwa na umri wa miaka 49.

Katika siku kama ya leo miaka 120 iliyopita inayosadifiana na 3 Julai 1904, alifariki dunia Theodor Herzl, mwasisi wa harakati ya kimataifa ya Kizayuni.
Herzl alizaliwa mwaka 1860 huko Bucharest mji mkuu wa Hungary na kisha kuelekea Austria. Mnamo mwaka 1897 aliunda Taasisi ya Kimataifa ya Kizayuni kwenye kongamano lililofanyika nchini Uswisi.
Herzl alibuni mikakati ya kuasisiwa utawala ghasibu na wa Kizayuni wa Israel kwenye ardhi za Palestina, utawala ambao hadi leo unaendelea kufanya jinai kubwa na kusababisha maafa yasiyo na kifani dhidi ya raia madhlumu wa Palestina.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita yaani 13 Tir mwaka 1350 Hijria Shamsiya alifariki dunia mwalimu mkubwa wa fasihi wa Iran, Dakta Muhammad Muin, baada ya kufanya juhudi kubwa za miaka mingi katika nyanja za utamaduni na mila za Kifarsi.
Dakta Muin alizaliwa katika mji wa Rasht kaskazini mwa Iran. Alijifunza fasihi ya Kiarabu ujanani na baada ya kukamilisha masomo yake katika skuli ya Darul-Funun alielekea katika Chuo Kikuu cha Tehran na kujiunga na masomo katika kitengo cha fasihi na falsafa.
Mwaka 1321 Hijria Shamsiya Ustadh Muin alianza kufanya kazi ya kufundisha na utafiti katika Chuo Kikuu cha Tehran akiwa mhitimu wa kwanza wa shahada ya udaktari wa lugha na fasihi ya Kifarsi.
Na Tarehe 3 Julai miaka 11 iliyopita rais wa zamani wa Misri kutoka harakati ya Ikhwanul Muslimin, Muhammad Morsi aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoongozwa na jeshi la nchi hiyo.
Mapinduzi hayo yaliongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Sisi. Morsi alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Misri baada ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011. Hata hivyo mwanasiasa huyo hakuweza kutatua matatizo ya kisiasa na kiuchumi ya muda mrefu ya nchi hiyo. Vilevile licha ya kwamba alihesabiwa kuwa katika safu za wanaharakati wa Kiislamu lakini alidumisha uhusiano wa karibu na utawala haramu wa Israel na akatangaza kutambua rasmi mkataba ya Camp David na utawala huo haramu.
Muhammad Morsi alitekeleza siasa zisizo sahihi kuhusu baadhi ya nchi za Kiislamu na hatimaye akasalitiwa na nchi alizozitegemea ambazo ziliwaunga mkono na kuwasaidia wale waliomuondoa madarakani.