Jul 23, 2024 23:20 UTC
  • Jumatano, tarehe 24 Julai, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 18 Muharram 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 Julai 2024.

Siku kama ya leo miaka 242 iliyopita Simón Bolívar mwanasiasa na mwanamapinduzi maarufu wa Amerika ya Kusini alizaliwa huko Caracas mji mkuu wa Venezuela.

Simon Bolivar alikomboa ardhi kubwa ya Amerika ya Kusini kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kihispania. Vilevile alikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya Caracas na kufanikiwa kuiteka Bogota huko katikati mwa Colombia. Simon Bolivar aliteuliwa kuwa Rais na Congress iliyokuwa imeundwa kwa shabaha ya kuasisi Colombia Kubwa na alifanikiwa kuzikomboa ardhi za Colombia, Venezuela na Panama. Mwaka 1822, mapambano ya ukombozi yaliyokuwa yakiongozwa na Bolivar yalienea pia hadi Ecuador na nchi hiyo ikajiunga na Colombia Kubwa, baada ya kupata uhuru. 

Simon Bolivar

Miaka 222 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas.

Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa. 

Alexandre Dumas

Siku kama ya leo, miaka 153 iliyopita alizaliwa Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli, alimu mkubwa na mtaalamu wa fiqhi wa Kabul, Afghanistan.

Akiwa kijana mdogo Allamah Sardor Kabuli alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa enzi hizo kama vile, Mirza Hussein Nuri na Sayyid Swafiyyud-Din Hassan bin Hadi Kadhimi, sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwa maulama na maraajii watajika kama vile, Sayyid Hassan Sadr naHaji Sheikh Abbas Qumi, ambapo pia alipata ijaza (idhini) ya kunakili na kuandika riwaya na hadithi.

Mwaka 1310 Hijiria, Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli alielekea mjini Kermanshah, Iran na kujishughulisha na ufundishaji kwa wakazi wa mji huo sanjari na kuandika vitabu kadhaa. Aidha msomi huyo alipata kusomea lugha kadhaa za dunia, kama vile Kiarabu, Kingereza, Kiebrania na Urdu.

Kitabu cha ‘Tarjama ya Injili ya Barnaba’ na ‘Hadithi 40 katika fadhila za Amirul-Muuminin’ ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli alifariki dunia mwaka 1372 Hijiria, akiwa na umri wa miaka 79 na kuzikwa mjini Najaf, Iraq. 

Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli

Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kiislamu.

Akiwa na miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo.

Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa Swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Hadi mwisho wa uhai wake msomi huyo alisalia mjini Tehran na baada ya kufariki dunia akazikwa mjini Qum. 

Ayatullah Ahmad Khansari

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita Jumuiya ya Mataifa iliipatia mamlaka rasmi serikali ya Uingereza ya kuzidhibiti Palestina, Iraq na eneo la mashariki mwa Jordan, huku usimamizi wa Syria na Lebanon ukipewa serikali ya Ufaransa.

Hata hivyo Paris na London ziliafikiana katika Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya hapo juu ya kugawana utawala wa kifalme wa Othmania na uamuzi huo wa Jumuiya ya Mataifa ulihalalisha suala hilo. 

Miaka 80 iliyopita katika siku kama ya leo, kikosi cha anga cha jeshi la Uingereza kiliishambulia vikali bandari muhimu ya Hamburg huko kaskazini mwa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Mashambulizi ya anga ya Ujerumani na Uingereza yalianza mwanzoni mwa Vita vya Pili vya Dunia na kushadidi zaidi baadaye. Kwa kadiri kwamba raia wengi wa nchi mbili hizo waliuawa katika mashambulizi hayo.

Makumi ya maelfu ya raia wa kawaida waliuawa kwa umati katika mashambulizi ya kikosi cha anga cha Uingereza dhidi ya bandari ya Hamburg mbali na kuangamizwa taasisi kadhaa za kijeshi na kiuchumi. 

Shambulizi la Uingereza dhidi ya Bandari ya Hamburg

Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo mnamo tarehe 3 mwezi Mordad mwaka 1361 Hijria Shamsiya, alifariki dunia Dakta Hamid Inayat, mwandishi na mtarjumi mahiri wa Kiirani.

Dakta Hamid alielekea nchini Uingereza baada ya kupata shahada ya chuo kikuu nchini Iran na akiwa huko alihitimu shahada ya udaktari katika taaluma ya uchumi na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha London. Dakta Hamid Inayat baadaye alirudi Iran na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran.

Dakta Inayat ameandika na kutarjumu vitabu vingi vya falsafa na fikra za kisiasa. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni Uislamu na Usoshalisti na Fikra za Kisiasa za Magharibi.