Jul 26, 2024 22:52 UTC
  • Jumamosi, 27 Julai, 2024

Leo ni Jumamosi 21 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria mwafaka na 27 Julai 2024.

Siku kama ya leo miaka 720 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Muharram 726 Hijria, alifariki dunia faqihi na msomi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu, Hassan bin Yussuf bin Mutahhari Hilli, maarufu kwa jina la Allamah Hilli. Allamah Hilli alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa kama Khaja Nasiruddin Tusi na anatajwa kama miongoni mwa wasomi wa kipekee wa zama zake. Aliandika zaidi ya vitabu mia moja katika taaluma mbalimbali za Kiislamu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni Tadhkiratul Fuqahaa' ambacho kinaelezea mitazamo mbalimbali za madhehebu ya Kiislamu, tafsiri ya Qurani Tukufu ya 'Nahjul Imaan' na 'Muntahaal Matwalib'.

 

Miaka 252 iliyopita, katika siku kama ya leo ulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kuigawa Poland kati ya madola matatu makubwa ya Ulaya katika karne ya 18. Poland ambayo hii leo ni moja ya nchi zilizo huru za mashariki mwa Ulaya, iligawanywa baina ya nchi tatu za Urusi, Austria na Prusssia kwa kutiwa saini makubaliano yaliyotajwa. Ni muhimu kuashiria hapa kwamba hadi sasa Poland imeshawahi kugawanywa mara nne kati ya nchi tofauti. 

Warsaw mji mkuu wa Poland

 

Miaka 200 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas. Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa. ***

Alexandre Dumas