Jumapili, 28 Julai, 2024
Leo ni Jumapili 22 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria mwafaka na 28 Julai 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 986 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi, ambaye ni mashuhuri kwa jina la Sheikhul Twaaifa. Sheikh Tusi alizaliwa katika mji wa Tus kaskazini mwa Iran na akaelekea Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu ya juu baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa Iraq na miaka kadhaa baadaye akaweka msingi wa chuo kikuu cha kidini cha Najaf. Kituo hicho cha kidini kina historia ya miaka elfu moja na ni moja ya vituo muhimu mno vya elimu ya Kiislamu. Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi sana katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani tukufu ya al Tibyan na vitabu vya hadithi na fiqhi vya al Istibsar na al Tahdhiib. ***

Miaka 295 iliyopita katika siku kama ya leo, harakati ya kwanza ya mapambano ya watumwa weusi wa Marekani ilianza huko kaskazini mwa nchi hiyo. Waanzilishi wa harakati hiyo ambao walikuwa watu 44 walimuua kila mzungu waliyekutana naye katika njia yao kutoka Carolina Kusini kuelekea Florida. Lakini walizingirwa na jeshi la Waingereza na kuuawa kabla ya kuingia Florida na kupata uhuru. Baada ya hapo watumwa weusi waliendeleza mapambano ya ukombozi na kupigania haki zao za kiraia. Watumwa weusi walikuwa wakitekwa nyara au kununuliwa kutoka Afrika tangu mwanzoni mwa karne ya 17 na kupelekwa Marekani kwa ajili ya kuuzwa na kufanyishwa kazi kwa mabwana zao. ***

Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, nchi ya Peru ilijipatia uhuru wake na siku hii hutambuliwa kuwa ni siku ya kitaifa nchini humo. Peru ilikuwa sehemu ya asili ya watu waliostaarabika wa Inca na tokea karne ya 12 hadi ya 16 ufalme wa watu hao ndio uliotawala kaskazini magharibi mwa Amerika ya Kusini. Mwanzoni mwa karne ya 16 wakoloni wa Uhispania waliingia Peru na baada ya mauaji ya kikatili dhidi ya Wahindi wekundu hatimaye ardhi ya Peru ikatawaliwa na wakoloni wa Uhispania. Wahispania waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi hiyo sambamba na kupora mali na raslimali za watu wa Peru hali iliyopelekea kupamba moto mapinduzi ya wapigania uhuru nchini humo. Peru iko kaskazini magharibi mwa Amerika ya Kusini, huku ikipakana na nchi za Ecuador, Colombia, Chile, Brazil na Bolivia. ***

Siku kama ya leo miaka 146 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Barlin, mwishoni mwa kongamano lililofanyika mjini humo kati ya wajumbe wa nchi za Russia, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Austria. Mkutano wa Berlin ulifanyika kwa ombi la kansela wa wakati huo wa Ujerumani Otto Von Bismarck. Kutiwa saini mkataba huo kuliifanya Ujerumani kuwa na satua ya kisiasa na kijeshi na kuandaa uwanja wa kujitanua zaidi nchi hiyo. Kimsingi kutiwa saini mkataba huo wa Berlin kulikuwa moja ya mambo yaliyoandaa uwanja wa kutokea Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. ***
Miaka 110 iliyopita, wakati wa kukaribia kuanza Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa kifalme wa Austria ulitangaza vita dhidi ya serikali ya Serbia kwa kisingizio cha kuuawa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo huko Serbia. Hata hivyo sababu kuu ya kutolewa tangazo hilo la vita ilikuwa ni upinzani wa wananchi wa Serbia dhidi ya uingiliaji wa Austria katika masuala ya ndani ya nchi yao na pia kufanyika uasi dhidi ya nchi hiyo. ***

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, tetemeko kubwa liliukumba mji wa Tangshan mashariki mwa China. Tetemeko hilo ambalo lilikuwa na ukubwa wa rishta 7.8, lilipelekea kuuawa watu wapatao laki sita na malaki kadhaa ya wengine kujeruhiwa sambamba na kuwa wakimbizi. Hata hivyo ripoti rasmi iliyotangazwa na viongozi wa China ilionyesha kuwa, idadi ya watu waliouawa katika tetemeko hilo ilikuwa laki mbili na 40 elfu. Hilo lilikuwa tetemeko kubwa zaidi kuwahi kuikumba China katika karne ya 20 na tetemeko kubwa kushuhudiwa tangu tetemeko la mwaka 1556 ambalo lilipelekea kuuawa kwa watu laki nane na elfu 30. ***

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Abul Hassan Bani Sadr, rais aliyeuzuliwa wa Iran alikimbia nchi akiwa pamoja na kiongozi wa kundi la Munafiqin la MKO, Mas'ud Rajavi. Siku 37 kabla yake Bani Sadr alikuwa ameuzuliwa cheo cha rais kutokana na kukosa ustahiki, kuzusha machafuko nchini na kushindwa kulinda nchi mbele ya hujuma za utawala wa Saddam Hussein. Bani Sadr alikuwa na matumaini kwamba, mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na kundi la MKO yangeweza kumrejesha tena madarakani. Hata hivyo kuchaguliwa Muhammad Rajai kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu kulimvunja moyo Bani Sadr ambaye aliamua kukimbilia Ufaransa akiwa amevaa nguo za kike. ***