Jumanne, tarehe 30 Julai, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 24 Muharram 1446 Hijria sawa na Julai 30 mwaka 2024.
Miaka 174 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia Haj Mulla Muhammad Taqi Istarabadi. Mullah Muhammad Taqi bin Muhammad Ismail alikuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Alipata ruhusu ya daraja ya ijtihad katika elimu ya fiqhi kutoka kwa Muhammad Taqi bin Muhammad Rahiim Tehrani aliyekuwa maarufu kwa jina la Sahib Hidayatul Mustarshidiin na kupata elimu kwa wanazuoni wakubwa wa Najaf na Karbala nchini Iraq kwa kipindi cha miaka 14.
Mulla Muhammad Taqi Istirabadi alihamia Tehran mwaka 1271 Hijria na kabakia katika mji huo hadi alipoaga dunia.

Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita, alifariki dunia Otto von Bismarck, Kansela wa kwanza na mwanasiasa mkongwe wa Ujerumani.
Bismarck aliongoza vita vitatu ambavyo viliainisha mustakbali wa Ujerumani kama nchi huku akikabiliana pia na madola ya Ulaya wakati huo. Bismarck alikuwa rais wa Prussia akiwa na umri wa miaka 28 na kwa mara ya kwanza akawa pia Kansela wa Ujerumani. Mwaka 1862 aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Prussia na kuanzisha mpango wa Ujerumani moja. Ili kufikia lengo hilo hakuwa na njia nyingine ghairi ya kuiondoa Austria katika shirikisho la majimbo ya Ujerumani ya Kikatoliki sambamba na kulikomboa jimbo la Schleswig-Holstein kutoka udhibiti wa Denmark na kuhitimisha upenyaji wa Ufaransa katika majimbo ya kusini mwa Ujerumani.
Baada ya kujiimarisha kijeshi alipigana vita vitatu na kufikia malengo yake katika vita vyote hivyo. Kwa mujibu wa historia, Otto von Bismarck alizishinda nchi za Denmark, Austria na Ufaransa, kulikoenda sambamba na kuteuliwa kuwa kansela wa Ujerumani mwaka 1890.
Tarehe 30 Julai miaka 77 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa Kimarekani anayejulikana kama baba wa sekta ya utengenezaji magari wa nchi hiyo Henry Ford.
Alizaliwa tarehe 30 Julai 1863 katika familia ya kimaskini na tangu utotoni alikuwa na hamu kubwa ya masuala ya mekaniki. Siku moja Ford aliona gari likitembea barabarani bila ya kuvutwa na farisi na akaamua kutengeneza gari lake mwenyewe. Henry Ford alifanyia majaribio mkokoteni wa kwanza usiotumia farasi akiwa na umri wa miaka 12 tu.
Mvumbuzi huyo aliboresha zaidi mkokoteni huo na mwaka 1896 alifanikiwa kutengeneza gari lake la kwanza. Mwaka 1895 alipewa haki ya kutengeneza magari licha ya kwamba watu wengine pia walikuwa wanatengeneza chombo hicho na mwaka 1903 aliasisi kampuni ya magari ya Ford Motor.
Ford aliwapiku watengeneza magari wengine kwa kutengeneza magari mengi ya bei rahisi.
Tarehe 9 Mordad mwaka 1366 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 37 iliyopita kulitokea tukio la kusikitisha la Ijumaa ya Damu mjini Makka.
Siku hiyo mamia ya mahujaji wa Kiirani na mahujaji kadhaa wa nchi nyinginezo wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa serikali ya Saudi Arabia, walipokuwa wakitekeleza faradhi ya kujibari na kujiweka mbali na washirikina ndani ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu.
Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hutekeleza ibada hiyo kila mwaka wakati wa Hija, kutokana na mafunzo ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo sambamba na kutoa wito wa umoja na mshikamano baina ya Waislamu, hutoa tangazo la kujiweka mbali na maadui wa Uislamu hasa Marekani na utawala ghasibu wa Israel.
Siku hiyo askari wa Kiwahabi wa Saudia walishambulia mahujaji hao kwa risasi na kuua mahujaji 400 za Kiirani na kujeruhi wengine zaidi ya elfu moja.