Jul 30, 2024 23:36 UTC
  • Jumatano, Julai 31, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 25 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria, sawa na 31 Julai 2024.

Siku kama ya leo miaka 1351 iliyopita, yaani tarehe 25 Muharram mwaka 95 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, alikufa shahidi Imam Ali bin Hussein, maarufu kwa lakabu ya Sajjad au Zainul-Abidin, mtoto wa Imam Hussein bin Ali (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (swa).

Imam Zainul Abidini alikufa shahidi mjini Madina akiwa na umri wa miaka 38. Baada ya mapambano makubwa ya baba yake katika jangwa la Karbala, Iraq Imam Sajjad alikuwa na jukumu zito la kufikisha ujumbe wa mwendelezo wa malengo ya baba yake, Imam Hussein (as).

Imam Sajjad alifanya juhudi kubwa za kufundisha utamaduni wa Kiislamu na kueneza mafundisho bora ya Qur'ani na Suna za Mtume Muhammad (saw), jambo ambalo lilikuwa sababu ya kubakishwa hai Qur'ani na Suna za Mtume. Imam Zainul-Abidin alikuwa mashuuhuri kwa uchamungu mkubwa na alikuwa mwingi wa kusujudu na kujipinda kwa ibada, na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya 'Sajjad' ikiwa na maana ya mtu mwenye kusujudu sana.

Tarehe 31 Julai miaka 218 iliyopita ardhi ya Cape huko kusini mwa bara la Afrika ilivamiwa na wanajeshi wa Uingereza.

Ardhi ya Cape au mji wa Cape Town ni sehemu ya kusini ya nchi ya Afrika Kusini iliyoko pembeni ya Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) ambayo ipo kati ya Bahari za Atlantic na Hindi.

Eneo hilo lina utajiri mkubwa wa dhahabu na almasi na ni kwa sababu hiyo ndiyo maana daima wakoloni wakawa wanalikodolea jicho la tamaa. 

Miaka 138 iliyopita aliaga dunia Franz Liszt mtunzi wa nyimbo wa Hungary.

Franz alizaliwa mwaka 1811. Franz Liszt pia alikuwa na kipawa na maarifa makubwa katika utungaji wa nyimbo. Nyimbo Hungarian Rhapsodies na shairi la Symphony ni miongoni mwa kazi za utunzi wa Franz Liszt.   

Franz Liszt

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita aliaga dunia Antoine de Saint-Exupery mwandishi na mwanaanga wa Kifaransa katika Vita vya Pili vya Dunia baada ya ndege yake kuanguka.

Exupery alizaliwa mwaka 1900 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwandishi Antoine de Saint Exupery alijishughulisha na masuala ya kusafiri angani kutokana na kupenda sana fani hiyo. Alijiunga na jeshi la Ufaransa katika Vita vya Pili vya Dunia na kuwa afisa wa masuala ya usafirishaji wa posta.

Siku hiyo Antoine de Saint Exupery alirusha ndege hewani akiwa katika kazi zake za kawaida, lakini ndege yake ilitoweka na mabaki ya mwili wake na ndege hiyo hazijaonekana hadi leo hii. Mwandishi huyo ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwao ni "The Little Prince", "Southern Mail" na "Night Flight." 

Antoine de Saint Exupery

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita kiongozi wa Waislamu weusi wa Marekani, Elijah Muhammad, alitoa wito wa kuundwa dola la watu weusi nchini Marekani chini ya usimamizi wa serikali ya Federali ya nchi hiyo.

Lengo la kutolewa fikra hiyo lilikuwa kukomboa Wamarekani weusi kutoka kwenye siasa za ubaguzi wa kimbari na kizazi nchini Marekani. Elijah Muhammad mwenyewe ambaye aliathiriwa na kiongozi mwingine wa Waislamu weusi wa Marekani kwa jina la la Wallace Fard Muhammad na kuwa Muislamu, alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa na taathira kubwa katika harakati hiyo ya kudai dola la Wamarekani weusi.

Elija Muhammad aliasisi chama cha Umma wa Uislamu (Nation of Islam) na kujenga misikiti na vituo kadhaa kwa ajili ya Waislamu wa Marekani. Hata hivyo baadhi ya wanachama wa harakati hiyo ya Waislamu weusi wa Marekani kama Malcolm X walikataa na kupinga baadhi ya itikadi za kidini na siasa za Elijah Muhammad.   ***

Katika siku kama hii ya leo miaka 3 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Mohammad Saeed Hakim, aliyekuwa marjaa na mwanazuoni mtajika wa Kiislamu. 

Alipata elimu kwa wanazuoni wakuwa wa Kiislamu kama babu yake, Sayyid Muhsin Hakim, Hussein Hilli na Sayyid Abulqasim al Khoei, na baada ya kifo cha Sayyid Khoei, alitambuliwa kuwa marejeo ya Waislamu katika masuala mbalimbali ya sheria na dini.

Licha ya kufungwa jela kwa miaka minane wakati wa utawala wa Saddam Hussein nchini Iraq, Sayyid Muhammad Saeed Hakim ameandika vitabu vingi katika masuala ya sheria, teolojia na masuala ya kijamii. 

Sayyid Muhammad Saeed Hakim alifariki dunia huko Najaf tarehe 25 Muharram 1443 Hijria na kuzikwa kwenye Haram ya Amirul Muuminin Ali (as) huko Najaf. 

Ayatullah Sayyid Mohammad Saeed Hakim