Aug 01, 2024 23:04 UTC
  • Ijumaa, Agosti 2, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 27 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria sawa na tarehe Pili Agosti 2024 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Agosti 1934, alifariki dunia Field Marsha Paul von Hindenburg, rais wa zamani wa Ujerumani na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya majeshi ya nchi hiyo wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Hindenburg alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Ujerumani mwaka 1925.  *

Field Marsha Paul von Hindenburg akiwa kando ya Hitler

Tarehe Pili Agosti miaka 79 iliyopita, kongamano la Potsdam lilikamilisha kazi zake. Kongamano hilo la tatu na la mwisho la viongozi waitifaki walioshiriki katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, lilianza tarehe 17 mwezi Julai na kumalizika tarehe Pili Agosti 1945.

Kongamano hilo lililofanyika katika mji wa Potsdam karibu na mji mkuu wa Ujerumani, Berlin lilihudhuriwa na Joseph Stalin, Harry S. Truman na Winston Churchill, marais wa wakati huo wa Urusi ya zamani, Marekani na Uingereza. 

Kongamano la Potsdam

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, jeshi la Iraq liliishambulia na kuikalia nchi jirani ya Kuwait. Huo ulikuwa uvamizi wa pili wa Iraq kwa jirani zake baada ya ule wa Iran wa mwaka 1980.

Utawala wa Saddam ulikuwa ukidai kwamba, ardhi ya Kuwait ni sehemu ya ardhi yake. Mashambulio ya Iraq dhidi ya Kuwait yalikabiliwa na radiamali kali ulimwenguni. Nchi nyingi duniani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilaani uvamizi huo na kuvitaka vikosi vya Iraq kuondoka mara moja katika ardhi ya nchi hiyo.

Nchi kadhaa zikiongozwa na Marekani zilituma vikosi vyao vya kijeshi katika Ghuba ya Uajemi ili kuviondoa vikosi vamizi vya Iraq kutoka katika ardhi ya Kuwait na kuhitimisha uvamizi huo Februari 28 mwaka 1991.