Jumatano, Agosti 7, 2024
Leo ni Jumatano Tarehe 2 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Agosti mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1324 iliyopita, aliuawa shahidi Zaid bin Ali bin Hussein mwana wa Imam Sajjad (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw).
Zaid bin Ali alisimama kupambana na dhulma za Banii Umayyah na kulinda matunda ya mapambano ya babu yake, Imam Hussein bin Ali (as). Baada ya mapambano ya kishujaa, Zaid bin Ali aliuawa shahidi katika mji wa Kufa nchini Iraq. Harakati ya mapambano ya Zaid ni miongoni mwa matunda ya mapambano ya Imam Hussein (as) katika medani ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria kwani baada ya mapambano ya siku ya Ashuraa kulijitokeza harakati nyingi baina ya Waislamu zilizopigana jihadi kwa lengo la kuuondoa madarakani utawala dhalimu wa Banii Umayyah.
Siku kama yale leo miaka 1176 iliyopita, sawa na tarehe pili Safar mwaka 270 Hijiria, harakati ya mapambano za Wazanji ilifeli baada ya kuuawa kiongozi wa harakati hiyo Sahib al-Zanj.
Ali Bin Muhammad maarufu kwa jina la Sahib al-Zanj ambaye alikuwa akijitambua kuwa mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) na Imam Ali bin Abi Twalib (as) alianzisha harakati ya mapambano mwaka 255 Hijiria akisaidiwa na wafuasi wake pamoja na watumwa weusi ambao walikuwa wakiitwa Wazanji, dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Bani Abbas huko kusini mwa Iraq. Sahib al-Zanj aliwaahidi watumwa hao weusi kuwaachilia huru kutoka katika minyororo ya utumwa na kuwapa haki zao za kijamii kama watu wengine suala ambalo liliwafanya watu wa jamii hiyo kuvutiwa na harakati yake. Mwaka 257 Sahib al-Zanj aliudhibiti mji muhimu wa Basra, Iraq na taratibu akaanza kutwaa maeneo mengine ya karibu na mji huo.
Katika kipindi hicho majeshi ya utawala wa Bani Abbasi yalifanya hujuma kadhaa dhidi ya Wazanji lakini hata hivyo hujuma hizo zilifeli kutokana na msimamo imara wa jamii ya watu hao weusi. Hata hivyo kutokana na matatizo ya ndani Wazanji walidhoofika sana na harakati yao iliyoendelea kwa kipindi cha miaka 15 ikasambaratika baada ya kuuawa kiongozi wao Sahib al-Zanj.

Siku kama ya leo miaka 701 iliyopita, alifariki dunia nchini Misri, Abu Hayyan Gharnatwi, malenga na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu.
Alizaliwa mwaka 654 Hijiria huko Andalusia 'Uhispania ya leo' na baadaye alifanya safari katika miji mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Mwaka 679 Abu Hayyan Gharnatwi, alielekea nchini Misri ambako aliishi hadi mwisho wa maisha yake. Akiwa nchini humo alijishughulisha na ufundisha na kuandika vitabu. Gharnatwi alikuwa mtaalamu wa elimu ya Qur'ani, Hadithi na sharia za Kiislamu, lakini alipata umashuhuri mkubwa katika utaalamu fasihi ya lugha ya Kiarabu.
Abu Hayyan Gharnatwi ambaye mwishoni mwa uhai wake alikuwa kipofu, ameacha turathi nyingi kama kitabu cha 'Al-Idraaku Lilisaanil-Atraak' 'Tadhkiratun-Nuhaat' 'Tafsirul-Bahril-Muhit' na diwani ya mashairi.

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita sawa na Agosti 7 1960 nchi ya Ivory Coast ilifanikiwa kujipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.
Wareno waliidhibiti nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika katika karne ya 16, lakini ulipofika mwaka 1891 Ufaransa iliidhibiti nchi hiyo, licha ya upinzani mkubwa wa wananchi wa Ivory Coast.
Hatimaye ulipofika mwaka 1960, Ivory Coast ikiwa pamoja na nchi nyingine kadhaa za Kiafrika zilizokoloniwa na Mfaransa zilijipatia uhuru wao.

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita mwafaka na tarehe 7 Agosti 1982, yalitiwa saini makubalino ya kuondoka vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) mjini Beirut Lebanon kati ya Marekani, Lebanon na PLO.
Makubaliano hayo yalitiwa saini kufuatia shambulio kubwa lililofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Lebanon mwezi Juni 1982 kwa shabaha ya kuwafukuza wapiganaji wa PLO nchini Lebanon. Ijapokuwa kuondoka wanamgambo wa PLO nchini Lebanon kulitoa pigo kubwa kwa harakati hiyo, lakini miaka ya baadaye Wazayuni maghasibu walikabiliwa na kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano wa harakati ya muqawama ya Lebanon, Hizbullah, na kulazimika kuondoka kwa madhila katika ardhi ya nchi hiyo mwaka 2000.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita mwafaka na tarehe 17 Mordad 1371 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Alhaj Sayyid Abul Qassim al Mussawi al Khoui, faqihi na marjaa mkubwa wa Kiislamu duniani, akiwa na umri wa miaka 96.
Mwanachuoni huyo mashuhuri alizaliwa katika mji wa Khoui ulioko kaskazini magharibi mwa Iran na akiwa katika umri wa ubarobaro, alifuatana na baba yake mjini Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Katika zama za umarjaa wake, Ayatullahil Udhma al Khoui alitoa fatwa inayosisitiza udharura wa kuilinda Palestina na kuikomboa Quds Tukufu kutoka mikononi mwa Wazayuni maghasibu.
Alimu huyo mkubwa ameacha vitabu vingi vikiwemo 'Jawaahirul Usuul', 'Muntakhabu Rasaail', 'al Bayaan Fii Tafsiiril Qurani' na "Misbahul Faqaha".
Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita vikosi vya jeshi la Georgia vikisaidiwa na serikali ya Marekani vililishambulia eneo linalopigania kujitenga la Ossetia ya Kusini huko kaskazini mwa nchi hiyo.
Mamia ya raia wasio na hatia wala ulinzi waliuawa na kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Siku moja baadaye, wanajeshi wa Russia waliingilia kati na kuamua kuwaunga mkono wapiganaji wanaopigania kujitenga wa Ossetia ya Kusini na kulilazimisha jeshi la Georgia kurudi nyuma.
Vikosi vya jeshi la Russia vilifanikiwa kuiteka bandari muhimu ya Patumi na kusonga mbele karibu na Tiblis mji mkuu wa nchi hiyo.
Jeshi la Russia liliondoka huko Georgia Agosti 12 kwa upatanishi wa Rais wa Ufaransa, na Moscow ikayatambua rasmi kuwa huru maeneo mawili yaliyokuwa yakipigania kujitenga yaani Ossetia ya Kusini na Abkhazia.
