Aug 12, 2024 08:37 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha 65 (58)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 65 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki. Ingawa hii ni sehemu ya 65 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoendelea kuichambua ni ya 58.

الْمَالُ مَادَّةُ الشَّهَوَاتِ.

Mali ni chanzo cha maasi na ufisadi.

Katika hikma hii ya 58 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatumia maneno machache sana kutoa tahadhari na kuzungumzia uhakika wa mambo kwa balagha ya hali ya juu. Anasema, mali ni chanzo cha ufisadi.

Ni wazi kwamba maana ya ufisadi hapa ni sifa yoyote aliyo nayo mmtu iliyochanganyika na hawa za nafsi na matamanio mabaya. Sifa hiyo inaweza kuwa inahusiana na hisia za kijinsia au kupenda jaha au anasa na starehe haramu za mambo ya kidunia na vitu kama hivyo.

Kupenda kujilimbikizia mali kwa njia haramu na kutotumia mali katika mambo ya kheri ndiyo sifa ya idadi kubwa ya watu duniani na kadiri pupa ya kujilimbikizia mali na kuzihesabu kama inavyosema Qur’ani Tukufu; kadiri mtu anavyokuwa na sifa hiyo ndivyo anavyozidi kutekwa na matamanio ya nafsi na kutumbukia kwenye ufisadi katika maana yake pana tuliyotangulia kuigusia hapo juu.

 

Vilevile mali huwa ni chanzo cha ghururi na majivuno, sifa ambayo ndiyo asili ya makosa na madhambi mengi. Aidha kadiri mtu anavyokuwa na mali nyingi, ndivyo akili yake inavyozidi kushughulishwa na mali hiyo na hivyo ile nafasi ya kumbukumbuka zaidi Allah ndani ya nafsi yake, inamezwa na kufikiria mali. Tunapozingatia maelezo hayo ndipo tutaweza kuelewa balagha kubwa na undani ya onyo hilo la Imam Ali AS katika hikma hii ya 58 ya Nahjul Balagha.

Ni jambo lililo wazi kwamba makusudio ya Imam Ali AS hapa si kwamba mali muda wote inakuwa hivyo. Hapana, bali katika hikma hii Imam anazungumzia aghlabu ya wakati huwa hivyo si mara zote. Mali ni wenzo na ni kitu kizuri kama kitatumiwa katika mambo mema. Ndio maana pia katika sehemu nyingi tu tunamuona Imam Ali anapiga vita umaskini mpaka kufikia kusema umaskini umekaribiana mno na ukafiri.

Qur’ani Tukufu nayo imejaa mifano ya namna hiyo. Kwa mfano katika kisa cha Qarun, aya ya 77 ya sura ya 28 ya al Qasas inazungumzia nasaha alizopewa Qarun kwa kusema: Na utafute, kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyokufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.

Naam, Qur’ani Tukufu inaonesha wazi kwamba kama mali haitotumiwa katika njia yake sahihi huwa ni chanzo cha ufisadi sawa kabisa na hali iliyomkumba Qarun ambaye alikaidi nasaha za Nabii Musa AS na mwishowe ikawa ni kudidimizwa ardhini yeye na jumba lake na mali yake.

Ziko aya nyingine mbalimbali pia zinazungumzia suala hilo kama aya ya 180 ya Suratul Baqara na aya ya 8 ya Suratul Aadiyat au Suratut Takathur n.k, lakini muda wetu umeisha kabisa.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags